Michael Servetus
Michael Servetus (kwa Kihispania Miguel Serveto y Reves, kwa Kifaransa Michel Servet; 29 Septemba 1509 au 1511 [1] huko Villanueva de Sigena ( Huesca ) katika Ufalme wa Aragón (Hispania)[2], 27 Oktoba 1553 huko Champel - Geneva ) alikuwa tabibu kutoka Hispania, msomi wa fani nyingi na mwanatheolojia aliyepinga Utatu. Alichomwa moto kama mzushi kwa uchochezi wa Calvin.
Servetus alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Toulouse. Pamoja na msafara wa Kaizari Karolo V (1500–1558) alitokea Hispania hadi Dola Takatifu la Kiroma, maana aliajiriwa kama mtumishi kutoka 1526 hadi 1530 [3] katika huduma ya padre muungamishi wa mfalme Juan de Quintana († 1534). Walipokaa Bologna (Italia) mwaka 1530 alishuhudia jinsi Papa Klementi VIII alivyomweka wakfu Karolo V kama kaizari wa Dola Takatifu. Servetus alishtuka alipoona fahari na anasa alizoonyesha Papa kwenye nafasi hiyo. Hapo Servetus aliamua kuhamia upande wa matengenezo ya Kiprotestanti. Aliondoka katika msafara wa Kaizari akaenda Basel (Uswisi) alipokaa karibu na Yohane Oekolampadus, wakati ule kiongozi wa kanisa la Basel, mji uliowahi kuhamia Uprotestanti. Mwaka uliofuata 1531 alikutana na viongozi wengine wa Uprotestanti mjini Strasbourg.
Mwaka uleule alichapisha kitabu chake De trinitatis erroribus (Kuhusu makosa ya Utatu) ambako alipinga mafundisho ya Utatu wa Mungu. Kitabu hicho kilipingwa na Wakatoliki na Waprotestanti sawia, halmashauri ya mji wa Basel iliagiza kukusanya nakala zake na kuzichoma.
Servetus alitaka kuthibitisha zaidi maoni yake katika kitabu Dialogi de trinitate (1532, "Majadiliano kuhusu Utatu").
Baada ya kuona upinzani dhidi ya maandiko yake yaliweza kuhatarisha uhai wake, alirudi Ufaransa akabadilisha jina na kujiita "Michel de Villeneuve". [4]
Servetus alijisomea habari za tiba, unajimu na hisabati. Alijipatia pia jina kama mwanajiografia kwa kutafsiri na kuchapisha kitabu cha mtaalamu wa kale Klaudio Ptolemaio. Kuanzia 1536 alisoma tiba kwenye Chuo Kikuu cha Paris. Wakati wa kusoma alipata ruzuku yake kwa kufundisha hisabati na unajimu. Hatimaye alihamia Montpellier alipohitimu shahada ya uzamivu katika tiba.
Kutoka huko alihamia mji wa Vienne na kuanza kazi ya tiba. Alikuwa daktari mashuhuri akatibu wakubwa wengi pamoja na maaskofu Wakatoliki na maafisa wa serikali. Aliandika kuhusu mzunguko wa damu. [5] [6] Wakati ule alianza kuwasiliana kwa njia ya barua na Calvin, kiongozi wa matengenezo ya Kiprotestanti huko Geneva.
Mnamo 1553 Servetus alitunga tena kitabu Christianismi Restitutio (Jinsi ya Kurudisha Ukristo) ambako alipinga mafundisho ya utatu pamoja na nadharia kuwa Mungu anateua tangu utotoni wengine kuingia mbinguni na wengine kuingia jehenam (predestination). Servetus alisisitiza kuwa Mungu hamhukumu yeyote asiyewahi kujihukumu mwenyewe kwa mawazo, maneno au matendo yake. Alituma nakala kwa Calvin aliyeona maandiko hayo kama shambulio dhidi ya imani ya Kikristo tangu siku za Imani ya Nikea. Calvin alimtumia nakala ya kitabu chake cha Institutio Christianae Religionis kama jibu na kumwambia anapinga mafundisho yake kabisa. Baada ya kubadilishana barua mara kadhaa Calvin alisitisha mawasiliano yake na Servetus.
Mwaka uleule wa 1553 rafiki wa Calvin, Mprotestanti Mfaransa, alimshtaki Servetus kwa njia ya barua aliyotuma Ufaransa. Baraza la Uchunguzi wa Imani la Ufaransa lilianza kumchunguza; Servetus akakamatwa na kushtakiwa kama mzushi, kosa chini ya sheria katika nchi za Ulaya wakati ule. Kwenye msingi wa nakala za barua za Calvin alihukumiwa kuwa mzushi afe kwa kuchomwa moto pamoja na vitabu vyake.
Servetus alifaulu kutoroka gerezani akaelekea Italia. Njiani alipita Geneva akaenda kusali kanisani alipohubiri Calvin. Baada ya ibada alitambuliwa akakamatwa. Baraza la Uchunguzi wa Imani la Ufaransa lilitaka akabidhiwe kwao kwa utekelezaji wa hukumu. Calvin aliyetazamwa pia kuwa mzushi na Wakatoliki alitaka kujionyesha kuwa mteteaji wa imani alisisitiza kesi ya Servetus iangaliwe na korti ya Geneva, mji wa Kiprotestanti. Calvin aliamini kwamba Servetus alistahili kuhukumiwa afe. Mahakama ya Geneva alimhukumu afe kwa kuchomwa moto kwa makosa mawili ya kukana Utatu wa Mungu na kukataa ubatizo wa watoto wadogo. Calvin -aliyekubali hukumu ya kifo- aliomba mahakama utekelezaji wa hukumu ubadilishwe iwe kwa kukata kichwa badala ya kuchomwa hai, lakini ombi halikupokewa.
Tarehe 27 Oktoba 1553 alifungwa juu ya fungu la kuni na kuchomwa akiwa hai pamoja na idadi ya vitabu vyake. Maneno yake ya mwisho yalikuwa "Yesu mwana wa Mungu wa milele, unihurumie".
Viungo vya Nje
hariri- Michael Servetus Institute – Museum and centre for Servetian studies in Villanueva de Sigena, Spain
- Michael Servetus Center Ilihifadhiwa 14 Agosti 2022 kwenye Wayback Machine. – Research portal on Michael Servetus run by servetians González Ancín & Towns, also including multiple works and studies by servetian González Echeverría.
- Center for Philosophy and Socinian Studies
- Works at Open Library
- Christianismi Restitutio – Full text, digitalized by the Spanish National Library.
- De Trinitatis Erroribus – Full text, digitalized by the Spanish National Library.
- Hanover text on the complaints against Servetus
- Hospital Miguel Servet, Zaragoza (Spain)
- Michael Servetus Ilihifadhiwa 6 Oktoba 2006 kwenye Wayback Machine., from the Dictionary of Unitarian and Universalist Biography
- Michael Servetus – A Solitary Quest for the Truth
- PDF; 64,1 MiB on Michael Servetus in Basel & Alfonsus Lyncurius and Pseudo-Servetus
- Michael Servetus Institute: Christianismi Restitutio. Comments and quotes.
- New opera: 'Le procès de Michel Servet'
- Reformed Apologetic for Calvin's actions against Servetus
- SERVETUS: HIS LIFE. OPINIONS, TRIAL, AND EXECUTION. Phillip Schaff, History of the Christian Church, Vol. 8, chapter 16.
- Thomas Jefferson: letter to William Short, 13 April 1820 – mention of Calvin and Servetus.
Marejeo
hariri- ↑ Ana Gómez Rabal: Vida de Miguel Servet. In: Turia, Nº 63–64, Teruel, S. 209–210.
- ↑ kufuatana vyanzo vingine alizaliwa huko Tudela (Navarra, Hispania)
- ↑ Barbara I. Tshisuaka: Servetus, Michael. In: Werner E. Gerabek, Bernhard D. Haage, Gundolf Keil, Wolfgang Wegner (Hrsg.): Enzyklopädie Medizingeschichte. De Gruyter, Berlin/ New York 2005, ISBN 3-11-015714-4, S. 1322 f.; hier: S. 1322.
- ↑ Wolf-Dieter Müller-Jahncke: Michael Servetus. In: Wolfgang U. Eckart, Christoph Gradmann (Hrsg.): Ärztelexikon. Von der Antike bis zur Gegenwart. 1. Auflage. 1995 C. H. Beck’sche Verlagsbuchhandlung, München 1995, S. 329, 330 (2. Aufl. 2001, S. 288; 3. Aufl. Springer Verlag, Heidelberg / Berlin / New York 2006, S. 299, 300. Ärztelexikon 2006), .
- ↑ Henri Tollin: Die Entdeckung des Blutkreislaufs durch Michael Servet, 1511–1553, 1876 (Volltext).
- ↑ John C. Hemmeter: Michael Servetus – Discoverer of the pulmonary circulation: his life and work. In: Janus 20, 1915, S. 331–364 und Tafel I–IX.