Mimar Sinan
Mimar Sinan (15 Aprili 1489 - 9 Aprili 1588) alikuwa msanifuujenzi maarufu wa Milki ya Osmani kwa muda wa miaka 50.
Alijenga zaidi ya majengo muhimu 360 kama misikiti, shule, hamamu (bafu), vyuo na kadhalika. Staili yake ya msikiti inarudiwa kama mfano kwa misikiti ya Kituruki hadi leo.
Maisha
haririAlizaliwa mnamo mwaka 1489 / 1490 katika familia ya Wakristo karibu na mji wa Kayseri. Alijifunza ujenzi kutoka kwa baba yake. Alipokuwa na umri wa miaka 20 alichukuliwa kutoka familia yake kwa kufuata mfumo wa "devshirme" ambako vijana Wakristo waliondolewa kwao na kufanywa wanajeshi Waislamu pamoja na kupewa jina la Kiislamu.
Alishiriki kama mwanajeshi katika vita za Waosmani kwenye nchi za Balkani na pia katika Shamu na Misri. Hapo aliweza kuona mifumo mbalimbali ya usanifu bora. Tangu miaka ya 1520 wakubwa wake walitambua uwezo wake kama mhandisi waampa kazi za ujenzi wa boma au madaraja.
Wakati wa vita dhidi ya Uajemi mwaka 1535 alipewa kazi ya kujenga mashua ya kubeba askari na mizinga kupitia Ziwa Van. Kutokana na mafanikio yake alikuwa mhandisi mkuu wa jeshi la Osmani. Mwaka 1539 alipandishwa cheo tena kuwa mjenzi mkuu wa milki yote akiwajibika kutengeneza barabara, madaraja na njia za usafiri kwa jumla.
Katika nafasi hii alipewa pia kazi ya kusanifisha majengo maalumu kama misikiti muhimu au makaburi ya wakubwa. Kati ya misikiti mingi aliyojenga ni hasa msikiti wa Şehzade na msikiti wa Suleymaniye mjini Istanbul na baadaye msikiti wa Selimiye mjini Edirne aliyotazama kama kazi kuu ya maisha yake.
Mfumo wa msikiti alioendeleza ulifuata mfano wa kanisa la Hagia Sophia la Konstantinopoli lenye kuba kubwa.
Hapa aliboresha mfumo huu na misikiti yake huwa na uwazi mkubwa chini ya kuba ya katikati.
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mimar Sinan kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |