Mnyamawamtuka moyowamkia
Dinosauri | ||||||||||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Umbo la Sauropoda, pamoja na Mnyamawamtuka
| ||||||||||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||||||||||
|
Mnyamawamtuka moyowamkia ni aina ya dinosauri ambaye visukuku vyake viligunduliwa kuanzia mwaka 2004 katika bonde la mto Mtuka upande wa kusini wa Ziwa Rukwa, karibu na kata ya Galula nchini Tanzania.
Jina
haririJina la Mnyamawamtuka linarejelea mahali ambako mifupa yake iligunduliwa yaani bonde la mto Mtuka. Sehemu ya pili ya jina „mkiawamoyo“ imechaguliwa kutokana na umbo la mifupa ya mkia wake inayofanana na moyo.
Mnyamawamtuka m. ni kati ya aina chache za dinosauri zenye majina ya Kiswahili, pamoja na jenasi ya Shingopana.
Tabia
haririTabia kadhaa ya mnyama huyo zinaonekana kutokana na mifupa yake yaliyopatikana kama visukuku. Mwili wake ulifanana kiasi na mjusi lakini alikuwa mkubwa sana, akiwa na kiwiliwili kikubwa, shingo ndefu, kichwa kidogo na mkia mrefu. Titanosauri walikula majani.
Mnyama aliyepatikana kwenye mto Mtuka alikuwa kijana bado ambaye hakufikia vipimo vya mkubwa. Alikuwa na uzito wa takriban tani 1.5, urefu wa mita 1.5 kiunoni na urefu wa mita 7.6 kuanzia kichwani hadi mwisho wa mkia wake. [1]
Ugunduzi
haririMwaka 2004 visukuku vya mifupa mikubwa viligunduliwa kwenye mtelemko mkali wa korongo la mto Mtuka. Ilionekana haraka mifupa ilikuwa ya aina ya dinosauri. Ugumu wa kufika kwenye mabaki hayo uliwalazimisha wagunduzi kuendelea na kazi hii miaka kadhaa. Uchimbaji uliongozwa na wataalamu wa Chuo kikuu cha Ohio wakishirikiana na wenyeji wa Tanzania.
Tangu mwaka 2009 sehemu kubwa ya kiunzi cha mifupa ilipatikana. Utafiti uliofuata ulichukua tena miaka hadi wagunduzi walipoweza kuonyesha matokeo yake mwaka 2019.
Uainishaji
haririMnyama huyo aliishi takriban miaka milioni 70-100 iliyopita. Mifupa yake inaonyesha alikuwa mmoja wa Titanosauria, kundi kubwa la Sauropoda waliokuwa na wanyama wakubwa zaidi walioishi kwenye nchi kavu.
Kuna tabia zinazofanana na Malawisauri aliyepatikana kisehemu kwenye Malawi ya kaskazini.
Tanbihi
hariri- ↑ Linganisha makala ya Geggel kwenye livescience.com
Marejeo ya Nje
hariri- Eric Gorscak , Patrick M. O’Connor: A new African Titanosaurian Sauropod Dinosaur from the middle Cretaceous Galula Formation (Mtuka Member), Rukwa Rift Basin, Southwestern Tanzania, 13 Februari 2019, jarida ya PLOS
- New dinosaur with heart-shaped tail provides evolutionary clues for African continent, tovuti ca Chuo Kikuu cha Ohio, tar 13 Februari 2019
- Laura Geggel: Titanosaur the Size of a School Bus Had Heart-Shaped Tail Bones, tovuti ya livescience.com, tar 13-02-2019