Reli ya Tanganyika (pia: Reli ya Kati) ilikuwa jina la njia ya reli kuanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma kwenye Ziwa la Tanganyika iliyojengwa katika miaka 1905 hadi 1914 zamani za koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Njia za reli za Shirika la Reli Tanzania

Majina

Majina mengine yaliyotumika yalikuwa kwa Kijerumani "Mittellandbahn", baadaye kwa Kiingereza "Central line" (Reli ya Kati), au "Tanganjikabahn" (kwa Kiingereza Tanganyika Railway).

Tabia

Reli hii ilikuwa na urefu wa kilomita 1245.4 ikitumia geji (upana wa njia) ya mita 1[1].

Baada ya mwisho wa ukoloni wa Kijerumani eneo la Tanganyika lilitawaliwa na Uingereza kama eneo la kudhaminiwa la Shirikisho la Mataifa. Katika kipindi hicho Reli ya Tanganyika iliongezwa njia ya kando kutoka Tabora kwenda Mwanza. Tangu mwaka 1977 njia hii imetawaliwa na Shirika la Reli Tanzania (Tanzania Railways Limited - TRL).

Njia ya reli

Njia ya reli hii inaanza Dar es Salaam ikipitia Morogoro, Dodoma na Tabora hadi kufika Kigoma.

Kuna njiapanda ambako njia ya kati inaunganishwa na njia za kando.

Kilomita Kituo muhimu Mwungano na njia nyingine
0 Dar es Salaam
79.7 Ruvu
82.9 Ruvu Junction njia ya Tanga - Arusha
203 Morogoro
289.5 Kilosa kwenda njia ya TAZARA
455.5 Dodoma
585.6 Manyoni njia ya Singida
840.5 Tabora njia ya Mwanza
936.7 Kaliua njia ya Mpanda
1245.4 Kigoma

Tanbihi

  1. Siku hizi upana wa njia ya reli (gauge) wa kawaida ni mita 1.435