Tanganyika (ziwa)
Ziwa Tanganyika ni moja ya maziwa makubwa ya Afrika ya Kati likienea mpakani mwa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia.
| |
Mahali | Afrika ya Mashariki |
Nchi zinazopakana | Burundi, Kongo, Tanzania, Zambia |
Eneo la maji | km² 32,893 kutegemeana na kiasi cha mvua |
Kina cha chini | kuanzia m 3.5 hadi 1,470 |
Mito inayoingia | Lufubu, Malagarasi, Ruzizi |
Mito inayotoka | Lukuga |
Kimo cha uso wa maji juu ya UB |
m 782 |
Miji mikubwa ufukoni | Bujumbura, Kalemie, Kigoma |
Ni ziwa kubwa la pili duniani kwa wingi wa maji matamu baada ya Ziwa Baikal (Siberia) kwa kuzingatia kiasi cha maji ndani yake na kina (hadi mita 1,470).
Kwa kulinganisha eneo lake (km² 32,893) ni la pili tu baada ya Viktoria Nyanza katika Afrika.
Maji yake hutoka kuelekea mto Kongo ha hatimaye katika Bahari Atlantiki.
Jina
haririHatuna uhakika jinsi gani wenyeji walioishi kando ya ziwa hilo waliliita kwa lugha zao mbalimbali. Kutokana na taarifa za wapelelezi Wazungu waliofika huko kwenye karne ya 19 na kushika yale waliyoelewa kutoka kwa wenyeji, kuna ushuhuda fulani kuhusu majina manne ambayo ni "Tanganika", "Liemba", "Kimana" na "Nsaga".
Jina la Tanganika limepokewa na Wazungu wa kwanza kutoka kwa wenyeji wa Ujiji. Henry Morton Stanley aliyetembelea ziwa mnamo mwaka 1876 aliandika ya kwamba watu wa Ujiji hawakuwa na uhakika kuhusu maana ya jina, ila tu kwamba lilimaanisha "ziwa kubwa"[1]. Maana waliita maziwa madogo "Kitanga", na waliita pia "ziwa la Usukuma" yaani Viktoria Nyanza kwa jina hilo "Tanganika". Wajiji walimwambia Stanley ya kwamba labda neno "nika" ilitokana na aina ya samaki walioitwa vile. Baadaye Stanley alikumbuka neno "nika" katika lugha nyingine za Kiafrika kwa maana ya "tambarare, eneo kubwa bapa" akahisi ya kwamba waliita ziwa kama "tambarare kubwa iliyotanda" [2].
Stanley alishika pia majina ya ziwa kwa makabila mengine: watu wa Marungu walisema "Kimana", wale wa Urungu "Iemba" na Wakawendi "Nsaga" kwa maana "ziwa lenye dhoruba". Alichoshika na watu wa Urungu, yaani "Iemba", inalingana na taarifa ya David Livingstone aliyekuta jina "Liemba" kuwa jina la sehemu ya kusini ya ziwa na jina hili linaendelea kutumiwa kwa meli ya MV Liemba inayosafirisha watu na bidhaa ziwani tangu mwaka 1914.
Jina la ziwa limekuwa pia jina la eneo lililokabidhiwa kwa Uingereza kama Tanganyika baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia tangu 1919.[3]
Jiografia
haririMaji ya Ziwa Tanganyika yanajaza ufa kubwa kwenye ganda la dunia ambalo ni sehemu ya bonde la ufa la Afrika ya Mashariki. Ni ziwa lenye kina kikubwa katika Afrika.
Vipimo
haririKina cha wastani ni m 570, ni kubwa zaidi katika sehemu ya kaskazini ambako vilindi vyake hufikia kina cha mita 1470. Kutokana na kina kikubwa kinashika kiwango kikubwa cha maji matamu kati ya maziwa yote ya Afrika (18,900 km³) na asilimia 16 ya maji matamu yote duniani.
Halijoto ya maji usoni mwa ziwa ni sentigredi 25 na uchungu wake ni pH 8.4 hivi.
Urefu wa ziwa ni kilomita 676 kutoka kaskazini hadi kusini na upana wake ni km 50 kwa wastani. Uso wa maji huwa na eneo la km2 32,900 na urefu wa pwani yake ni km 1,828. [4]
Kina kikubwa cha ziwa kimesababisha kuwepo kwa safu za maji zisizochanganya maana maji ya chini hayakorogwi kwa upepo au mikondo na maji ya juu, hivyo maji ya chini hayapokei oksijeni na kuwa na uhai kidogo. Samaki na viumbehai wengi hawawezi kuishi katika maji bila oksijeni.
Beseni
haririZiwa linapokea maji yake kutoka mito ya mazingira inayoishia humo. Beseni lake huwa na eneo la km2 231,000 (sq mi 89,000).
Mito miwili mikubwa na mito mingi midogo inaishia ziwani. Mto Lukuga hutoka ziwani na kupeleka maji yake kwenda beseni la Kongo.
Mto mkubwa zaidi unaoingia ni Ruzizi unaofika upande wa kaskazini kutoka Ziwa Kivu. Malagarasi, ambao ni mto mrefu wa pili nchini Tanzania, inaingia upande wa mashariki.
Kubadilika kwa kiasi cha maji
haririKutokana na mahali pake katika tropiki kwenye jua kali, Ziwa Tanganyika linapotewa na maji mengi kwa njia ya uvukizaji. Kwa hiyo kiasi cha maji ndani yake inategemeana na kiasi cha maji yanayoingia. Kwa sasa chanzo kikubwa ni maji ya Ziwa Kivu. Imegunduliwa ya kwamba uwiano wa ziwa ulibadilika sana katika historia. [5]
Mnamo miaka 200,000 iliyopita uso wa ziwa ulikuwa mita 600 chini ya uwiano wa leo. Wakati wa vipindi vya tabianchi yenye mvua nyingi zaidi uwiano ulipanda juu, na kupungua tena kwenye vipindi vya ukame. Vipindi hivi vya mabadiliko vilidumu mara kwa mara miaka elfu kadhaa.
Hali ya sasa imepatikana tangu miaka 12,000. Wakati ule volkeno za Virunga vililipuka na kuziba mto uliowahi kubeba maji ya Ziwa Kivu kuelekea mto Naili na baada ya kufikia uwiano wa leo maji ya Kivu yalianza kutoka upande wa Tanganyika kupitia njia ya Ruzizi.
Mabadiliko ya uwiano wa maji kwenye ziwa yalitazamwa pia katika historia ya miaka 200 iliyopita kwa kulinganisha kumbukumbu ya wakazi na taarifa za wapelelezi Wazungu walioandika taarifa juu ya safari zao. Baada ya mwaka 1800 maji yalikuwa chini sana, kabla ya 1900 yalikuwa juu sana, tangu 1900 yalishuka tena. Katika miaka ya 1960 ziwa lilijaa tena likabaki hivi hadi sasa.
Mabadiliko haya yanalingana na mabadiliko katika kiasi cha mvua inayopokewa katika beseni ya ziwa. [6]
Miji na nchi jirani
haririMiji mikubwa ziwani ni bandari za Kigoma kwa upande wa Tanzania na Kalemie kwa upande wa Kongo. Kila bandari ni pamoja na mwanzo wa njia ya reli. Mji mkubwa kabisa ni Bujumbura, mji mkuu wa Burundi.
Eneo lote la ziwa limegawiwa baina ya nchi jirani yaani Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia. Sehemu kubwa iko chini ya Tanzania (46%) na Kongo (40%).
Visiwa
haririKuna visiwa mbalimbali ndani ya ziwa Tanganyika. Vikubwa zaidi ni pamoja na
Biolojia
haririKuna spishi nyingi za samaki aina ya cichlidae zinazokadiriwa kuwa 250 na angalau spishi 75 za samaki wengine. Spishi nyingi wanaishi karibu na mwambao na hadi kina cha mita 180; chini yake kiwango cha oksijeni kinapungua mno. Lakini kiasi kikubwa cha samaki kinapatikana katikati ya ziwa, ila ni spishi chache tu, hasa spishi mbili za kapenta (inayoitwa pia dagaa) na spishi nne za sangala.
Cichlidae karibu spishi zote ni wenyeji wa ziwa yaani wametokea hapa. Pia sangala ni wenyeji wa Tanganyika, kwa hiyo hakuna matatizo kama huko Viktoria Nyanza ambako spishi ya sangala iliingizwa miaka 50 iliyopita na kuvuruga ekolojia ya ziwa.
Kutokana na mazingira ya pekee ziwa Tanganyika ni mahali pa kutazama matokeo ya mageuko_ya_spishi. [7]
Cichlidae wa ziwa Tanganyika wanapendwa kama samaki wa mapambo wakinunuliwa na kufugwa na wenye tangisamaki kote duniani.
Ziwani kuna pia spishi nyingi za pekee za konokono na kaa pamoja na crustacea nyingine.
Uvuvi
haririTasnia muhimu katika eneo la ziwa ni uvuvi. Inakadiriwa ya kwamba baina ya 25–40% za protini katika chakula cha milioni 1 ya watu wanaoishi kule ni kutoka samaki wa ziwani[8].
Mwaka 2015 kulikuwa na watu 100,000 hivi waliofanya kazi kuhusiana na uvuvi.
Samaki wa ziwani wanauzwa kote Afrika ya Mashariki. Katika miaka ya 1950 uvuvi wa kibiashara ulianzishwa ziwani ukasabisha kupotea kwa samaki: kufikia mwaka 1995 mavuno ya samaki yalipungua hadi tani 180,000. Kampuni nyingi za uvuvi zilizostawi katika miaka ya 1980 ziliporomoka.
Usafiri
haririUsafiri ni mgumu kufikia Ziwa Tanganyika kutoka miji mikuu ya nchi zao.
Kuna njia za reli zinazoishia
- Kigoma (Tanzania) kutoka Dar es Salaam, bado kwenye njia ya reli iliyojengwa zamani za ukoloni wa Kijerumani
- Kalemie (J.D. Kongo) kutoka Lumbumbashi
- Mpulungu (Zambia) - hakuna reli bado, ila kuna mipango ya kujenga njia hadi hapa hadi njia kuu ya TAZARA
Huduma iliyopo hadi sasa ni ngumu na hali za njia za reli si nzuri. Upande wa Tanzania treni zilichelewa mno, masaa hata siku, lakini hali ilianza kuwa afadhali kuanzia Julai 2016.[9]
Muhimu kwa ajili ya watu ziwani ni huduma ya feri. Kuna meli 2 zinazobeba abiria na mizigo ambazo ni MV Liemba baina ya Kigoma na Mpulungu halafu MV Mwongozo baina ya Kigoma na Bujumbura.
Marejeo
hariri- ↑ Habari zifuatazo kutoka HM Stanley, Through the Dark Continent Vol 2, p 16
- ↑ Tanganika, 'the great lake spreading out like a plain', or 'plain-like lake'. Maelezo tofauti kidogo ni kwamba jina Tanganyika limetokana na samaki wa aina mbili ndani ya ziwa, aina ya kwanza anaitwa Tanga na wa pili anaitwa Nyika, hivyo ziwa hilo kwa wakati huo wa hao samaki kupatikana katika ziwa hilo likaitwa ziwa la Tanga na nyika! Baadaye katika matamshi wenyeji wa eneo hilo wakawa wanaita Tanganyika na baadaye kuzaa nchi inayoitwa Tanganyika na baadhi ya sehemu kuitwa hivyo.
- ↑ Mwaka 1919 sehemu kubwa ya koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ilikabidhiwa rasmi mikononi mwa Uingereza kama eneo la kudhaminiwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa kulingana na kifungo 22 cha mkataba wa Versailles. Mwaka 1922 Shirikisho la Mataifa lilithibitisha hatua hiyo na kuamua masharti ya kukabidhi. Waingereza walihitaji jina jipya kwa ajili ya koloni hilo na tangu Januari 1920 wakaamua kuliita "Tanganyika Territory" kwa kutumia jina la ziwa kubwa upande wa mashariki wa eneo. [1]
- ↑ Viwango vyote vinatajwa kufuatana na "World Lake Database" Ilihifadhiwa 10 Februari 2018 kwenye Wayback Machine.
- ↑ tazama Christian Lévêque, Biodiversity Dynamics and Conservation: The Freshwater Fish of Tropical Africa, Cambridge University Press 1997, uk. 109 ff
- ↑ Historical and Modern Fluctuations of Lakes Tanganyika and Rukwa and Their Relationship to Rainfall Variability, Sharon E. Nicholson in: Climatic Change (1999) 41 (summary on springer.com, iliangaliwa Novemba 2016)
- ↑ African Cichlid Fishes: Model Systems for Evolutionary Biology Ilihifadhiwa 7 Novemba 2017 kwenye Wayback Machine., Kornfield, Ivy & Smith, Peter A., ktk Annual Review of Ecology and Systematics, Vol. 31: 163-196, Nov. 2000
- ↑ Lake Ecosystem Critical to East African Food Supply Is Threatened by Climate Change , taarifa ya National Science Foundation (NSF) kupitia tovuti ya www.mongabay.com, iliangaliwa 6 Novemba 2016
- ↑ TRC ilitangaza ya kwamba tarehe 23 Julai 2016 treni ya abiria kutoka Kigoma ilifika Dar es Salaam "on time" yaani kwenye saa na dakika iliyoandikwa katika ratiba yake. Tazama http://www.trl.co.tz/?p=1316 Ilihifadhiwa 16 Novemba 2016 kwenye Wayback Machine. tovuti ya TRC (iliangaliwa Novemba 2016)
Viungo vya nje
hariri- Food and Agriculture Organization of the United Nations Ilihifadhiwa 14 Machi 2008 kwenye Wayback Machine.
- Index of Lake Tanganyika Cichlids Ilihifadhiwa 17 Novemba 2011 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Tanganyika (ziwa) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |