Ruge Mutahaba

(Elekezwa kutoka Ruge mutahaba)


Ruge Mutahaba (Brooklyn, New York, Marekani, 1 Mei 1970 - Afrika Kusini, 26 Februari 2019) alikuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Vipindi wa Clouds Media Group [1] nchini Tanzania.[2][3] Pia alikuwa mwanzilishi wa nyumba maarufu ya kukuza vipaji vya sanaa iitwayo Tanzania House of Talents (THT)[4] iliyolea na kukuza vipaji vingi vya muziki kama Diamond Platnumz, Barnaba Classic, Mwasiti, Linah, Ditto, Ray C na kadhalika.

Rugemalila Mutahaba
Amezaliwa Ruge Mutahaba
1 Mei 1970
Brooklyn, New York, Marekani
Amekufa 26 Februari 2019 (miaka 49 )
Afrika Kusini
Nchi Tanzania
Majina mengine Ruge
Kazi yake Mwanzilishi-mwenza wa Clouds Media Group
Cheo Mkurugenzi wa vipindi Clouds Media Group
Chama cha kisiasa Chama Cha Mapinduzi
Dini Mkristo
Ndoa Hakufunga
Rafiki Joseph Kusaga
Watoto 5

Ruge alikuwa mtu mwenye msukumo wa kuisaidia jamii kuupokea ujumbe wa maendeleo. Kati ya miradi yake mikubwa iliyoacha alama kuwa kwa vijana Tanzania ni Mradi wa Fursa alioufanya kwa kushirikiana na Clouds Media Group na wadau wengine wa maendelea kama UN Tanzania[5], Brela[6], SIDO[7], Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu[8], Wizara ya Afya kupitia mradi wake wa Nyumba ni choo na mashirika mengine binafsi.

Katika kupambana na ukosefu wa ajira[9] kwa vijana waliohitimu elimu ya juu, Ruge alianzisha darasa maalumu aliloliita School of Excellence and Innovation akishirikiana na msanii maarufu Nikki wa Pili na Hassan Ngoma[10] ambao wote ni wakuu wa wilaya kwa sasa. Darasa hilo lilijikita kufundisha ujuzi laini wa lazima kwa wahitimu wa elimu ya juu ambao haukufundishwa darasani lakini ni wa lazima kuwasaidia kupata ajira au kuanzisha biashara zao binafsi ifikapo mwaka 2020[11] kama ulivyopendekezwa na taasisi ya kimataifa World Economic Forum[12]. Ujuzi huo ulihusisha Utatuzi wa Changamoto Tata (Complex Problem Solving), Ushirikiano na Wengine (Coordinating with Others), Kufikiri kwa Kina (Critical Thinking), Usimamizi wa Watu (People Management), Majadiliano (Negotiation), Ubunifu (Creativity), Usimamizi wa Viwango (Quality Control) n.k.

Ruge alipenda kushiriki ujuzi wake na watu wengine, na kabla ya kufikwa na mauti alianza kuandika kitabu alichokiita "Jibu Rahisi sio Jibu Jepesi" alichokiandika akishirikiana na mwanafunzi wake Elias Tryphone [13].

Ruge ni mtoto wa kwanza wa profesa Gelase Mutahaba na Christina Mutahaba; alipata elimu yake ya shule ya msingi mkoani Arusha darasa la kwanza hadi la sita, kisha akahamia Shule ya Msingi Mlimani ambako alihitimu elimu yake ya msingi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani mkoani Dar es Salaam na kuhitimu kidato cha nne, na kidato cha sita katika shule ya sekondari Pugu. Alihitimu shahada ya Masoko kisha Shahada ya Sanaa katika Uchumi Chuo Kikuu cha San Jose huko Kalifornia, Marekani[14]

Taaluma

hariri

Aliporejea Tanzania kutoka Kalifornia ambako alihitimu masomo yake, Ruge alianza kutambulika kwenye jamii baada ya kuanza kufanya kazi na rafiki yake Joseph Kusaga ambaye alikuwa akiendesha Klabu yake ya usiku almaarufu kama disko iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Clouds Disco. Ushirikiano wao ulipelekea kuanzishwa kwa Clouds Media Group mjini Arusha ambayo, licha ya kuwa chombo cha habari na burudani kwa jamii, hasa vijana, ilifanya kazi ya kuhamasisha vijana wadogo wa Kitanzania kujiingiza katika kutafuta fursa na ujasiriamali ili kujiinua na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla wake.[14] Tokea maisha ya utotoni Ruge alikuwa mpenada muziki, lakini kipaji chake hakikuwa kwenye muziki peke yake. Alikuwa mchezaji mpira wa miguu (soka), alipewa majina mengi kwa kipaji hicho akicheza timu za mtaani, za Chuo Kikuu kuanzia Adanco na Summer Rangers na alifikia hatua ya kuchaguliwa katika timu ya mkoa wa Dar es salaam ya UMISETA. Pia alikuwa na kipaji cha kuandika. Vipaji vingine vyote havikuweza kunawiri kwani alikuwa na mapenzi na muziki zaidi.

Familia

hariri

Ruge Mutahaba hakuwahi kufunga ndoa rasmi lakini alikuwa na mahusiano na Zamaradi Mketema na walipata watoto wawili.[14] Pia alizaa wengine watatu na kufanya jumla ya watoto watano [15]

Maradhi na kifo

hariri

Ruge Mutahaba alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na tatizo la figo akapelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu, ambayo pia rais wa Jamhuri ya Tanzania John Magufuli alimchangia shilingi milioni hamsini [16], hadi mauti yalipomfika tarehe 26 Februari 2019.[3][17][18]

Watanzania wengi waliopokea habari za kifo chake, akiwemo Rais John Pombe Joseph Magufuli[17], walishtushwa na habari za mauti yake na kutuma jumbe za kuguswa kutokana na mchango mkubwa wa Ruge katika tasnia ya habari na burudani, ubunifu katika mipango mikakati, kuendeleza vipaji vya vijana wa Tanzania, kuhamasisha ari ya ufanyaji kazi kwa bidii katika jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.[3]

Marejeo

hariri
  1. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2019-12-16. Iliwekwa mnamo 2019-12-28.
  2. "Ruge Mutahaba". ONE. 16 Agosti 2017. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2019-02-27. Iliwekwa mnamo 26 Februari 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. 3.0 3.1 3.2 "Ruge Mutahaba afariki dunia, Rais Magufuli amlilia". Mwananchi. Iliwekwa mnamo 26 Februari 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. "Tanzania House of Talents – Tanzania House of Talents" (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  5. "United Nations in Tanzania". tanzania.un.org (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  6. "BRELA | Mwanzo". www.brela.go.tz. Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  7. "SIDO | Small Industries Development Organization". www.sido.go.tz. Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  8. "PMO-LYED | Home". www.kazi.go.tz. Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  9. "Ukosefu wa ajira kwa vijana", Wikipedia, kamusi elezo huru, 2022-09-18, iliwekwa mnamo 2023-06-07
  10. "Download HASSAN NGOMA ASIMULIA MAISHA YA MIAKA MIWILI BILA RUGE BILA YEYE YAWEZEKANA RAISI ASINGENIONA" Mp3 and Mp4 (07:57 Min) (10.92 MB)". MP3 Music Download (kwa American English). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2023-06-07. Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  11. "The 10 skills you need to thrive in the Fourth Industrial Revolution". World Economic Forum (kwa Kiingereza). 2016-01-19. Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  12. "The World Economic Forum". World Economic Forum (kwa Kiingereza). 2023-06-06. Iliwekwa mnamo 2023-06-07.
  13. https://www.linkedin.com/in/eliastryphone/
  14. 14.0 14.1 14.2 "Ruge Mutahaba Biography, Career, Family". 12 Februari 2018. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2019-02-27. Iliwekwa mnamo 26 Februari 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  15. https://www.mwananchi.co.tz/habari/Makala/Familia-ya-Ruge-nje-ya-Mutahaba/1597592-4995480-9i1ld1/index.html iliangaliwa tar 15 Machi 2019
  16. https://www.jamiiforums.com/threads/rais-magufuli-atoa-dola-20-000-kusaidia-matibabu-ya-ruge-mutahaba-mkurugenzi-wa-cmg.1511074/page-8
  17. 17.0 17.1 "Tanzania: Clouds Media Group programmes director Ruge Mutahaba dies in South Africa". Thecitizen.co.tz. Iliwekwa mnamo 26 Februari 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  18. "TANZIA: Ruge Mutahaba afariki Dunia! Rais Magufuli aungana na Watanzania kuomboleza". JamiiForums. Iliwekwa mnamo 26 Februari 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ruge Mutahaba kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.