Sisifos (kwa Kigiriki Σίσυφος , Sísyphos, kwa Kiingereza Sisyphus) alikuwa mhusika katika hadithi za mitholojia ya Kigiriki. [1]

Sisifos anayebeba jiwe lake, akiangaliwa na mungu Persephone; uchoraji kwenye jagi ya Kigiriki
Sisifos na kazi yake, taswira ya Tizian

Alikumbukwa kama mfalme wa Korintho mwenye hekima lakini pia mjanja aliyefaulu kudanganya miungu. Habari zake zilisimuliwa na mshairi wa Ugiriki ya Kale Homer, pia na waandishi mbalimbali wa Ugiriki na Roma ya Kale.

Kosa la Sisifos

hariri

Aliwahi kufichua siri moja ya mungu mkuu Zeu alipomwambia mungu wa mito Asopo kwamba Zeu alimwiba binti wake Aigina. Zeu alikasirika juu ya Sisifos akamtuma mungu wa mauti Thanatos kwake amchukue na kumpeleka kuzimu. Lakini Sisifo alifaulu kumpa Thanatos divai nyingi hadi akalewa kabisa akamfunga kwa minyororo. Tangu Thanatos alipofungwa, hakuna mtu aliyekufa tena. Mungu wa vita Ares alishangaa alipoona wapinzani hawakufa sasa vitani. Ilhali Ares alikosa furaha katika kazi yake alimtafuta Thanatos akamkuta na kumweka huru. Alimshika Sisifos akampeleka kuzimu na kumkabidhi kwa mungu wa kuzimu Hades. Lakini kabla ya kushikwa na Ares, Sisifos aliweza kuonana kifupi na mke wake akampa amri kutomtolea sadaka baada ya kifo chake.

Baada ya kufika kuzimu, Hades alishangaa kwa sababu hapakuwa na sadaka kwake Sisifos. Sisifos akamwambia Hades kwamba kama angemruhusu kurudi mara moja katika uhai, angemwambia mke wake kutoa sadaka hizo. Lakini alipopata kibali hicho, alirudi nyumbani akafurahia maisha na kumcheka mungu yule na ujinga wake. Hivyo Thanatos alipaswa kumchukua mara ya pili.

Adhabu ya Sisifos

hariri

Kwa amri ya Zeu alipewa adhabu ya pekee kwa ujanja wake. Alipaswa kusukuma jiwe kubwa juu ya mtelemko wa mlima kwenye kuzimu. Mara alipolifikisha juu, jiwe lilibiringika tena hivyo kazi ilianza upya.[2] Alilazimika kurudia hii tena na tena milele. [3] Katika lugha za Ulaya ambako hadithi hii imeendelea kusimuliwa, kazi isiyomalizika huitwa "kazi ya Sisifos" ("sisyphean" task).

Marejeo

hariri
  1. "Sisyphean," Oxford English Dictionary, 3rd ed., 2001; retrieved 2012-3-29.
  2. Littell, Robert S. (1849). The Living Age, Vol. 20, p. 53.
  3. Mythweb.com, "Sisyphus" Ilihifadhiwa 29 Machi 2021 kwenye Wayback Machine.; retrieved 2012-3-29.

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: