Spageti (kwa Kiitalia: Spaghetti) ni chakula cha tambi chenye asili ya Italia Kusini. Ni tambi ya ngano yenye umbo jembamba kama kamba na urefu wa sentimeta 40.

Spageti katika sufuria: maji ya chumvi yenye mafuta kidogo
Spageti alla Napoletana ni pamoja na mchuzi wa nyanya na jibini iliyosagwa juu yake
Spageti iliyoungwa kwa nyama na jibini.

Hupikwa katika maji kwa dakika chache na kuliwa kwa uma baada ya kuongeza michuzi mbalimbali.

Spageti ni aina mojawapo ya chakula cha pasta na neno linatumiwa wakati mwingine kutaja pasta kwa jumla.

Kutoka Italia chakula hicho kimeenea duniani kote kwa sababu hupikwa haraka, inaleta shibe nzuri na kuna njia nyingi za kubadilisha ladha yake.

Kwa njia ya utani zimekuwa ishara ya utamaduni wa Italia, jinsi inavyoonekana katika filamu za Spaghetti Western.

Michuzi

hariri

Kati ya michuzi ya kawaida ya spageti kuna hasa aina mbili:

  • "alla Napoletana" au kufuatana na kawaida ya Napoli: ni mchuzi mzito wa nyanya na viungio kama vitunguu, vitunguu saumu na majani ya kuongezea ladha. Juu yake humwagwa jibini iliyosagwa. Wengine huongeza vipande vidogo sana vya nyama iliyokaangwa pamoja na vitunguu katika supu hii.
  • "alla Bolognese" au kufuatana na kawaida ya Bologna: ni mchuzi wa nyama iliyosagwa na kukaangwa katika sufuria pamoja na viungio.

Kuna aina nyingine nyingi kama vile "alle vongole" (na kome za bahari) au "alla carbonara" (mchuzi wa jibini, vipande vidogo vya nyama na yai) au "all'aglio e olio" (vitunguu saumu vilivyokaangwa kwa mafuta tu).