Teknolojia
Teknolojia (kutoka Kiingereza: Technology ni elimu inayohusu uhandisi, ufundi, ujenzi, vifaa na mbinu za uzalishaji wa vifaa na huduma katika jamii.
Asili ya neno ni Kigiriki "τέχνη" (tamka: tékhne): „uwezo, usanii, ufundi".
Teknolojia inaweza kumaanisha:
- vifaa na mashine zinazotumika katika matengenezo au uzalishaji wa vitu
- elimu ya matumizi yake pamoja na mbinu na maarifa jinsi ya kutumia sayansi
- uwezo wa kubadili malighafi asilia na kuwa bidhaa yenye thamani inayoweza kukidhi mahitaji ya binadamu. Hapa bidhaa haimaanishi tu vitu kama magodoro, magari ya kutembelea, unga wa ngano n.k., la hasha: ni huduma yoyote inayotolewa kwa jamii, mfano huduma ya usafiri, huduma ya utalii, huduma ya chakula, na pamoja na vitu vyote vinavyozalishwa viwandani.
Teknolojia nyepesi kabisa ni ujuzi wa kutumia vyombo ili kurahisisha kazi. Kwa mfano, katika somo la historia, mwanadamu alivumbua teknolojia ya kuwasha na kudhibiti moto amabo ulimwezesha kupika. Vile vile, aliweza kutumia mawe kwa kulima na kuwinda. Kadri wakati ulivyoenda ndivyo teknolojia yake ilivyoboreka kwa mfano kwa uvumbuzi wa gurudumu lililorahisisha ukulima na kusafiri kwake.
Maendeleo ya teknolojia ya kale yalihusisha uvumbuzi wa chombo cha kupiga chapa, simu na mtandao ambazo zimefanya mawasiliano yawe rahisi.