Historia ya teknolojia
Historia ya teknolojia ni historia ya ubunifu wa vifaa na mbinu za kutumia vifaa hivi katika uzalishaji wa mahitaji, bidhaa na huduma katika jamii.
Kuna mbinu mbalimbali kupanga historia hii na kutambua ngazi za maendeleo ndani yake.
Teknolojia ya kwanza: Zana za Mawe
haririKati ya mifano ya kwanza ya teknolojia ya binadamu ni matumizi ya mawe kama vifaa pamoja na matumizi ya moto. Tangu kupatikana kwa vifaa vya mawe wanahistoria wanahesabu kipindi hiki kama Zama za Mawe.
Watu walitengeneza pia vifaa kwa kutumia mifupa na mbao. Lakini mabaki ya vifaa vya mawe yamehifadhiwa kwa vingi hadi leo tofauti na vifaa vya ubao au mifupa vilivyooza mara nyingi.
Kuna mifano ya ncha za mawe kwa ajili ya mishale ya kuwinda tangu mwaka 64,000 KK lakini pinde za kwanza ambazo ni ubao zilipatikana tu tangu mwaka 8,000 KK.
Watu wa kwanza walikuwa wawindaji na wakusanyaji. Walipata maisha kwa kuvinda wanyama na kukusanya matunda, wanyama waliokufa, mayai ya ndege, kuvua samaki au kuchimba mizizi iliyofaa kama chakula. Kwa kawaida hawakuishi mahali pamoja muda wote isipokuwa mahali pasipo na watu wengi lakini windo nyingi.
Watu walijifunza kuchagua mawe ya kufaa na kuyapasua ili kupata kona kali. Vile "visu vya mawe" vilitumiwa kwa kukata nyama ya wanyama waliowindwa, kusafisha ngozi za wanyama kwa matumizi ya mavazi, kuchimba mizizi ya kuliwa ardhini au kushikwa mikononi kama silaha. Mifano ya kale kabisa iligunduliwa Olduvai (Tanzania) na mtindo wa huko huitwa teknolojia ya Olduvai.
Baadaye watu waliboresha vifaa vya mawe kupata visu na shoka kamili. Waliweza kuunganisha visu hivi na fimbo kuunda mikuki au mishale ya pinde kama silaha za uwindaji. Kama walitumia mawe kama silaha bila kubadilisha umbo la jiwe hayawezi kutambuliwa.
-
Mifano ya vifaa vya kwanza ilivyopatikana pia Olduvai
-
Kisu cha mawe iliyoboreshwa kiasi
-
Jinsi gani kutumia kifaa cha mawe
-
Chaguo la visu vilivyoendelea (Marekani)
-
Chaguo la visu na shoka kutoka mwisho wa Zama za Mawe
Mahali mbalimbali duniani penye mawe ya kufaa wataalamu walitambua mabaki ya karahana ambako visu vya mawe vilitengenezwa kwa vingi. Mfano mmojawapo ni bonde la Isimila karibu na Iringa, Tanzania ambako mabaki mengi ya utengenezaji wa vifaa vimepatikana. Mafundi wa kale walipasua mawe na kuyapigapiga hadi kupata visu vikali. Vipande vidogo vilivyokatwa pamoja na visu visivyoridhika vilitupwa mahali pa kazi na hivyo wataalamu wamepata picha ya kazi zilizotekelezwa. Kwa kutazama mabaki kama yale ya Isimila katika pande zote za dunia inawezekana kupata picha ya maendeleo ya teknolojia ya kutengeneza vifaa vya mawe kwa kupata visu vyembamba na vikali zaidi. Karahana kama Isimila zinaonyesha uzalishaji kwa wingi kwa hiyo ni dalili ya biashara maana wataalamu wanahisi visu hivi vilibadilishwa kwa chakula au chumvi na watu walioishi katika sehemu pasipokuwa na mawe ya kufaa.
Zama za Mawe hupangwa katika vipindi mbalimbali kufuatana na maendeleo ya kuboreshwa kwa vifaa vya mawe ingawa mabadiliko haya yalikuwa tofauti sana kati ya maeneo mbalimbali. Kwa mfano tamaduni za Amerika zilitumia vifaa vya mawe vyenye kiwango cha juu hadi kufika kwa Wazungu katika karne ya 16 ingawa menginevyo wenyeji hao walikuwa na miji mikubwa kushinda miji ya Ulaya na maendeleo mengine.
Maendeleo mengine wakati wa Zama za Mawe
haririWatu wa kwanza waliishi katika Afrika penye hali ya hewa ya joto. Kadri walivyohama na kufika nchi baridi zaidi walihitaji mavazi ya kujikinga dhidi ya baridi. Inaaminiwa ya kwamba mwanzoni ngozi za wanyama zilitumiwa kama mavazi lakini rahisi kujua chanzo kamili kwa sababu tofauti na zana za mawe ngozi au vitambaa vinaoza. Lakini kuna sindano za kushona zilizotengenezwa kwna mifupa na ndovu zilizopatikana tangu miaka 30,000 KK. Hakuna uhakika ufundi wa ufumaji ulianza lini lakini kuna dalili katika makaburi ya kale zinazoonyesha uwezekano ya kwamba ufumaji ulianza kabla ya kilimo.
Hatua nyingine iliyotokea tangu milenia ya mwisho wa Zama za Mawe ilikuwa ufinyanzi. Mfano wa kale wa udongo uliofinyagwa na watu na kuchomwa motoni ni sanamu ndogo za wanawake wanaoamiiwa kuwa ushahidi wa dini za kale. Mfano wa kale kanisa limepatikana nchini Ucheki na kukadiriwa ulitengenezwa miaka 30,000 iliyopita ingawa mifano ya vyombo vya ufinyanti kama bakuli au chupa inapatikana tangu mwaka 1200 pekee.
Mapinduzi ya Kilimo
haririTangu takriban mwaka 12,000 KK badiliko kubwa lilitokea katika maisha ya watu walipogundua kilimo.
Badiliko hili lilikuwa harakati lililohitaji miaka elfu kadhaa likazidi kuenea polepole lakini likabadilisha maisha na utamaduni wa binadamu.
Hadi sasa kuna mahali pachache duniani palipogunduliwa kwamba ndipo watu walipoanza kulima. Kila mahali watu walianza kutambua uwezekano wa kutunza mbegu za mimea na kuzipanda tena na kuvuna palepale walipopanda; upande mwingine ulikuwa uwezo wa kufuga wanyama badala ya kuwawinda tu.
Hasa ujuzi wa kupanda mbegu ulisababisha badiliko kubwa la maisha. Tangu kugundua mbinu hiyo watu hawakuhitaji tena kuhama wakifuata windo na hali ya hewa lakini walipokuta ardhi njema, bali waliweza kupanda na kuvuna na kukaa mahali pamoja.
Hatua hii ilikuwa chanzo cha makazi ya kudumu, halafu vijiji na miji ya kwanza na pia binadamu akaanza kufuga mifugo mbalimbali kama mbwa, mbuzi na kadhalika.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya teknolojia kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |