Teknolojia ya nano
Teknolojia ya nano ni neno la teknolojia mpya inayohusu matumizi ya vitu vidogo sana na miundo yake ambayo inapimwa kuwa kati ya nanomita 1-100.
Maana ya nano
haririAsili ya neno ni kipimo cha nanomita ambayo ni sehemu ya bilioni moja ya mita. Hii inamaanisha vitu ambavyo ni vikubwa kuliko atomi na vidogo mara 1000 kuliko upana wa unywele.
Hivyo teknolojia ya nano inalenga kupanga atomi na molekuli moja kwa moja na pia nje ya hali jinsi zilivyoweza kupangwa hadi sasa.
Pale ambapo wataalamu wanafaulu kushughulikia mata yenye vipimo hivi vidogo sana, vinapatikana vitu vingi vinavyoonyesha tabia mpya ambavyo havikujulikana bado. Au vitu vinaweza kutegengenezwa ambavyo vimetazamwa kiasili hapa na pale lakini haikuwezekana kuvitengeneza kwa matumizi ya binadamu.
Mifano ya kiasili
haririWatu walishangaa tangu kale kuona ni namna gani wadudu wanaweza kutembea kwenye uso wa ukuta bila kuanguka. Watungaji wa hadithi za katuni kama Spiderman waliwaza ya kwamba labda mtu angeweza kutumia mbinu ileile lakini hii ilitazamwa kama ndoto tupu.
Tangu wataalamu wametambua siri hii ya nzi inajulikana ya kwamba uwezo wao unatokana na nywele nyingi ndogo zenye urefu wa nanomita kadhaa ambazo zinaongeza sana eneo la uso wa miguu linalogusana na uso wa ukuta.
Kadiri ya uwezo unapatikana kutengeneza nyuzi nyembamba kiasi hiki kuna tayari makadirio kwa vifuniko kwa miguu na mikono vitakavyowezesha watu kutambaa ukutani.
Mfano mwingine ni majani ya mimea mbalimbali ambayo hayawezi kuloweshwa kwa maji. Muundo wa uso wa majani hayo unakataa maji kukaa juu yake.
Wanasayansi wameanza kuiga muundo huu na tokeo lake ni nyuso za vitu visivyochafuka. Kutokana na maua ya yungiyungi tabia hii inaitwa "tabia ya yungiyungi" (kwa Kiingereza lotus effect).