Tekenya
Mchoro wa jike la tekenya aliyejaa na mayai
Mchoro wa jike la tekenya aliyejaa na mayai
Jike la tekenya aliyetolewa katika mguu
Jike la tekenya aliyetolewa katika mguu
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Siphonaptera (Wadudu bila mabawa wenye kinywa kwa umbo wa mrija)
Familia: Hectopsyllidae
Jenasi: Tunga
Jarocki, 1838
Spishi: T. penetrans
Linnaeus, 1758

Tekenya, pia funza au susa, (Kisayansi: Tunga penetrans) ni aina ya kiroboto mdogo ambaye jike lake huchimba chini ya ngozi, k.m. katika vidole na wayo wa mguu wa watu. Asili yake ni Amerika ya Kusini na ya Kati, ambapo kuna spishi 12 nyingine, lakini spishi hii imewasilishwa bila kukusudia katika Afrika kusini kwa Sahara[1].

Mzunguko wa maisha wa tekenya

Utambulisho

hariri

Tekenya ndiye kiroboto mdogo kabisa anayejulikana katika awamu yake ya kuishi huru, akiwa na mm 1 tu. Anatambulika zaidi katika awamu ya udusio ya jike. Wakati amepachikwa chini ya tabaka la nje la ngozi, anaweza kufikia upana wa hadi sm 1. Wakati wa siku kadhaa za kwanza za shambulio kidusiwa anaweza kuhisi kuwashwa au usumbufu ambao hupita wakati eneo karibu na kiroboto limekuwa sugu na kukosa hisia. Tumbo la kiroboto linapovimba na mayai baadaye katika mzunguko, shinikizo linalosababiswa na uvimbe linaweza kushinikiza neva au mishipa ya damu ya jirani. Kulingana na mahali halisi, hii inaweza kusababisha hisia kutoka kwa usumbufu mdogo hadi mkubwa.

Mzunguko wa maisha

hariri

Mayai ya tekenya yana urefu wa mm 0.6 kwa wastani. Lava hutoka katika yai ndani ya siku moja hadi sita kwa masharti ya kuwa hali za mazingira (k. m. halijoto, unyevu n.k.) ni nzuri[2].

Baada ya kutoka kiroboto huendelea kupitia hatua mbili za lava. Hii ni ya kipekee kwa kuwa takriban viroboto wote hupitia tatu. Katika kipindi cha ukuaji huo, kiroboto kwanza hupungua kwa ukubwa kutoka saizi yake ya kutoka ya mm 1.5 hadi mm 1.15 (hatua ya kwanza) kabla ya kukua hadi mm 2.9 (hatua ya pili).

Siku sita hadi nane hivi baada ya kutoka lava huwa bundo na kujitengenezea kifukofuko. Kwa sababu huishi zaidi juu na chini ya uso wa mchanga, mchanga hutumiwa kuimarisha kifukifuko na kusaidia ukuaji wake. Usumbufu wa mazingira kama vile mvua au ukosefu wa mchanga umeonyeshwa kupunguza matukio ya tenkenya, inayosababishwa kwa uwezekano mkubwa na kupungua kwa hali za mazingira (yaani, mchanga na unyevu k.m.) ambazo kiroboto hutegemea ukuaji wa jumla[3]. Bila usumbufu wowote kwenye kifukofuko, kiroboto mpevu atatoka katika bundo baada ya siku 9-15[2].

Madume bado huendelea kutembea baada ya mlo wa damu kama vile viroboto wengine, lakini majike huchimba kichwa-kwanza kwenye ngozi ya kidusiwa na kuacha ncha ya fumbatio yake kuonekana kupitia tundu kwenye kidonda cha ngozi. Tundu hili linaruhusu kiroboto kupumua, kunya, kupandana na kutoa mayai huku akijilisha kutoka kwa mishipa ya damu. Huishi katika tabaka la dermis na chini ya dermis ya ngozi.

Vidonda vinavyosababishwa na matekenya hutokea takriban kila mara kwa miguu (97%), lakini vinaweza kutokea kwa sehemu yoyote ya mwili. Vidole vya miguu vinateseka zaidi ya 70% ya mara hizo na mikunjo inayozunguka kucha ni mahali panapopendekezwa.

Mara tu jike akiwa amechimba ndani ya ngozi ndipo uzazi unaweza kutokea, kwani dume na jike hawavutii porini[2]. Dume hufa baada ya kupandana, lakini jike huendelea kukuza na kutaga mayai. Katika muda wa wiki mbili zijazo tumbo lake huvimba kwa mayai mamia kadhaa hadi elfu moja ambayo huyatoa kupitia tundu la nyuma yakianguka chini tayari kutoa lava. Kisha kiroboto hufa na mara nyingi huwa chanzo cha maambukizo kwani mwili huoza chini ya magamba manene ambayo kemia ya mwili wake iliunda ili kumlinda. Mayai hukomaa na lava kukua mpaka viroboto wapevu ndani ya wiki tatu hadi nne na mchakato huanza upya.

Jenasi na vidusiwa

hariri

T. penetrans si ya kawaida baini ya spishi 13 zinazojulikana za jenasi Tunga. Kwanza, ina msambao mpana: baadhi ya nchi 88 katika Karibi, Amerika ya Kati na Kusini, Afrika ya kitropiki (kusini kwa Sahara), na Uhindi. Pili, inaweza kuathiri aina mbalimbali za vidusiwa: angalau spishi 26 katika zaidi ya oda 5 za mamalia. Kinyume chake, spishi nyingine za Hectopsylidae ziko katika nusutufe ya magharibi pekee na kila moja inalenga tu vidusia 1-2 mahususi wenye damu moto[4][5].

Spishi saba za Tunga hushambulia wagugunaji tu. Mbili zinajitolea kwa armadilo, moja kwa mvivu na moja nyingine anapendelea ng'ombe tu. Ni mmoja tu, Tunga trimamillata, ambayo pia amepatikana akiambukiza watu na ng'ombe vilevile, lakini katika Peru na Ekwado tu[6].

Vidusiwa wa tekenya

hariri

Marejeo

hariri
  1. Cestari TF, Pessato S, Ramos-e-Silva M Tungiasis and myiasis. Clin Dermatol. 2007 Mar-Apr;25(2):158-64.
  2. 2.0 2.1 2.2 Nagy, N.; Abari, E.; D’Haese, J.; Calheiros, C.; Heukelbach, J.; Mencke, N.; Feldmeier, H.; Mehlhorn, H. (2007). "Investigations on the life cycle and morphology of Tunga penetrans in Brazil". Parasitology Research. 101 (Suppl 2): S233–42. doi:10.1007/s00436-007-0683-8. PMID 17823833. S2CID 23745194.
  3. Heukelbach, Jörg; Wilcke, Thomas; Harms, Gundel; Feldmeier, Hermann (2005). "Seasonal variation of tungiasis in an endemic community". The American Journal of Tropical Medicine and Hygiene. 72 (2): 145–9. doi:10.4269/ajtmh.2005.72.145. PMID 15741550.
  4. Beaucournu, J.-C.; Degeilh, B.; Mergey, T.; Muñoz-Leal, S.; González-Acuña, D. (2012). "Le genre Tunga Jarocki, 1838 (Siphonaptera: Tungidae). I – Taxonomie, phylogénie, écologie, rôle pathogène". Parasite. 19 (4): 297–308. doi:10.1051/parasite/2012194297. ISSN 1252-607X. PMC 4898135. PMID 23193514. Kigezo:Open access
  5. Linardi, Pedro Marcos; Beaucournu, Jean-Claude; de Avelar, Daniel Moreira; Belaz, Sorya (2014). "Notes on the genus Tunga (Siphonaptera: Tungidae) II – neosomes, morphology, classification, and other taxonomic notes". Parasite. 21: 68. doi:10.1051/parasite/2014067. ISSN 1776-1042. PMC 4270284. PMID 25514594. Kigezo:Open access
  6. Linardi, Pedro Marcos; de Avelar, Daniel Moreira (2014). "Neosomes of tungid fleas on wild and domestic animals". Parasitology Research. 113 (10): 3517–3533. doi:10.1007/s00436-014-4081-8. PMC 4172993. PMID 25141814. Kigezo:Open access