Umaru Musa Yar'Adua (16 Agosti 19515 Mei 2010) alikuwa mwanasiasa kutoka nchini Nigeria na rais wa 13 wa nchi hiyo tangu 2007 hadi kifo chake hapo 2010. Ni rais wa kwanza mwenye shahada katika historia ya Nigeria.

Umaru Yar'Adua (2007)

Familia yake

hariri

Yar'Adua alikuwa Mwislamu kutoka familia ya Wafulbe katika Nigeria ya Kaskazini. Baba yake Musa Yar'Adua alikuwa waziri katika serikali ya kwanza ya nchi baada ya uhuru. Kaka yake jenerali Shehu Musa Yar'Adua alikuwa makamu wa rais chini ya Olusegun Obasanjo kati ya 1976 hadi 1979 akafungwa jela chini ya udikteta wa Sani Abacha.

Elimu yake

hariri

Umaru Yar'Adua alisoma kemia tangu mwaka 1972 kwenye Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello mjini Zaria akawa mwalimu kwenye vyuo mbalimbali. Tangu 1983 akaacha kufundisha akijishughulisha na kampuni mbalimbali.

Gavana

hariri

Mwaka 1999, baada ya serikali ya Abacha, alichaguliwa kuwa gavana wa jimbo la Katsina akarudishwa mwaka 2003.

Mwanasiasa asiye na rushwa?

hariri

Yar'Adua alisifiwa kwa sababu alitangaza mali zake kabla ya uchaguzi wa 1999 na 2003. Anasemekana alikuwa gavana aliyekataa rushwa. Alikuwa kati ya magavana wachache wasiochunguzwa na mamlaka ya kupambana na rushwa "Economic and Financial Crimes Commission".

Gavana na shari'a

hariri

Alipingwa kwa sababu alishiriki katika tangazo la muundo wa shari'a ya Kiislamu kuwa sheria ya jimbo wakati yeye ni gavana; Katsina ilikuwa jimbo la tano katika Nigeria iliyotangaza shari'a. Pia kesi ya mama Amina Lawal ilitokea chini ya ugavana wake. Mama huyo alishtakiwa chini ya shari'a kuwa alimzaa mtoto ilhali hakuolewa akahukumiwa auawe kwa kupigwa mawe. Baada ya watu wengi kote duniani kuleta maombi na serikali ya kitaifa kupinga hukumu hiyo, mahakama ya juu ilifuta hukumu na kumuokoa Amina. Yar'Adua anasemekana hakujaribu kumtetea wala kuzuia adhabu ya kifo.

Uchaguzi wa rais

hariri

Mwezi wa Desemba 2006 Umaru Yar'Adua aliteuliwa kuwa mgombea wa chama cha PDP kwa uchaguzi wa Aprili 2007. Rais Olusegun Obasanjo alimfanyia kampeni akapata kura nyingi na kumchagua kama makamu wake Goodluck Jonathan (gavana wa Jimbo la Bayelsa kusini mwa Nigeria).

Kura ya 21 Aprili ilipingwa na watazamaji wengi wa kitaifa na kimataifa kwa sababu ya udanganyifu ulioonekana mahala pengi. Hata hivyo Yar'Asdua alitangazwa kuwa mshindi aliyepata asilimia 70 za kura zote.

Wapinzani walidai uchaguzi urudiwe lakini Yar'Adua alikataa akiwakaribisha vyama vyote kuingia katika serikali ya umoja wa kitaifa na kusahihisha sheria ya uchaguzi.

Tarehe 29 Mei 2007 akaapishwa kuwa rais mpya wa Nigeria. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi ya kuwa maraisi wawili waliochaguliwa wamefuatana bila kungilia kwa jeshi.