Unitatis Redintegratio
Kurudisha umoja kati ya Wakristo wote ni lengo kuu mojawapo la Mtaguso wa pili wa Vatikano.
Matengano yaliyokata vipandevipande mwili wa Kristo ni kinyume cha matakwa yake na yanakwaza ulimwengu usiweze kuamini.
Mtaguso uliona siku hizi Mungu amewahurumia Wakristo na kuwatia hamu ya umoja hata ukatokea tapo la ekumeni.
Ndiyo sababu tarehe 21 Novemba 1964 (kwa kura 2137 dhidi ya 11) ilitolewa hati maalumu inayoitwa kwa Kilatini "Unitatis Redintegratio" (yaani "Urudishaji wa Umoja").
Kwa hati hiyo Kanisa Katoliki linawajibika kushirikiana na madhehebu yoyote ya Kikristo lisije likazuia kazi hiyo ya Roho Mtakatifu.
Sura ya kwanza
haririSura ya kwanza inaeleza msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu ekumeni.
Imani yake ni kwamba Kanisa ni moja tu, nalo limekabidhiwa kwa waandamizi wa mitume chini ya waandamizi wa Petro.
Mtaguso unakiri kuwa mafarakano yaliyotokea kati ya Wakristo yalisababishwa na makosa ya pande zote.
Waliolelewa Kikristo nje ya Kanisa Katoliki hawawezi kulaumiwa, tena ni Wakristo halisi na ndugu za Wakatoliki, ingawa ushirika wao si kamili.
Wakatoliki wawaheshimu pamoja na mema yao mengi ambayo yanatokana na Mungu na kuelekea ujenzi wa Kanisa.
Makanisa yao au jumuia zao vinatumiwa na Mungu kama vyombo vya wokovu, ila katika Kanisa Katoliki tu unapatikana ukweli mzima na vifaa vyote vya wokovu.
Hata hivyo Mtaguso ulikiri kwamba Wakatoliki hawatumii vizuri neema hizo hata wanawakwaza wenzao; basi, wanapaswa kulenga ukamilifu wa Kikristo ili Kanisa ling’ae mbele ya wote.
Mbali ya matendo ya kupendana ni muhimu pia majadiliano ya kiteolojia na mikutano ya sala ya pamoja.
Sura ya pili
haririSura ya pili inaeleza utekelezaji ikisisitiza kuwa unawapasa waamini wote, kwa njia ya kurekebisha Kanisa, kuongoka, kusali, kushirikishana sakramenti, kufahamiana, kueleza imani kwa usahihi na bila ya kudharau madhehebu mengine, kushirikiana katika kutetea haki na amani na kuleta maendeleo.
Sura ya tatu
haririSura ya tatu inaeleza kifupi historia ya mafarakano kwa kutofautisha sana yale yanayohusu Waortodoksi na yale yanayohusu Waprotestanti, hasa kutokana na makundi hayo mawili kudumu kuwa au kutokuwa na daraja halisi na hivyo kuwa au kutokuwa na sakramenti ya ekaristi. Kwa msingi huo kiteolojia baadhi yanastahili kuitwa "Makanisa", baadhi "jumuia za Kikanisa" tu.
Uhusiano wa Wakatoliki na makundi hayo ni tofauti, na uwezekano wa kushirikiana katika sakramenti ni mkubwa kwa Waortodoksi, bali ni mdogo kwa Waprotestanti.
Mwishoni hati hii inakiri kuwa ekumeni inapita uwezo wa binadamu, kwa hiyo tegemeo lote ni katika sala ya Yesu kwa Kanisa, katika upendo wa Baba na katika uwezo wa Roho Mtakatifu.