Mwili wa Kristo ni namna ambayo Mtume Paulo na wengineo walichambua fumbo la Kanisa kama umoja wa waamini wote, ukiwa na Yesu kama kichwa chake[1]. Ndiye anayesadikiwa kuwa chemchemi ya ukombozi wa wanadamu wote pale alipolifia Kanisa na kuliachia sakramenti kuu ya Pasaka, yaani ekaristi takatifu.

Uanzishwaji wa Ekaristi, mchoro wa Nicolas Poussin, 1640.

Utakatifu wetu unategemea nguvu zinazomtoka mfululizo Kristo Mkombozi ambaye, kwa njia ya sakramenti na hata nje ya hizo, anatushirikisha neema alizotustahilia alipoishi duniani, kwa namna ya pekee wakati wa mateso yake.

Jinsi Mwokozi anavyoshirikisha neema alizotustahilia hariri

Yeye anafanya hivyo kama chombo hai kilichounganika moja kwa moja na umungu, chemchemi ya neema zote. “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema” (Yoh 1:16). Mwenyewe amesema, “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote… Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu” (Yoh 15:4-8).

Mtume Paulo alitoa mfano mwingine wa kushangaza, akisema Kristo ni kichwa kinachovishirikisha viungo vyote uhai wa roho; Kanisa ndio mwili wa fumbo wa Kristo, na Wakristo ndio viungo vya mwili huo. “Ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake” (1Kor 12:27). “Tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu mojamoja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo” (Ef 4:15-16).

Basi, Mwokozi anatushirikisha nguvu hai za neema kama vile kichwa kinavyovishirikisha viungo vyake uhai ambao roho ndiyo asili yake. Tofautishe umungu na utu wa Kristo. Kama Neno yeye anakaa pamoja na Baba na Roho Mtakatifu katika kiini cha roho yetu akiidumishia uzima wa kimaumbile na ule upitao maumbile; anaiongoza kufanya yale isiyoweza kufanya peke yake. Utu wa Mwokozi ndio chombo kilichounganika na umungu moja kwa moja ambacho tunashirikishwa neema zote; haukai rohoni mwetu, kwa kuwa mwili wake hauwezi kuwemo rohoni mwetu, ila uko mbinguni kwa namna ya mwili na umo katika ekaristi kwa namna ya sakramenti. Hata hivyo mwadilifu anapokea mfululizo nguvu za utu wa Yesu, kwa sababu kila neema inatolewa kwa njia yake tu. Kwa kuwa kila nukta tuna wajibu fulani, utu wake unatushirikisha neema ya msaada ya sasa hivi, kama vile hewa inavyoingizwa mfululizo mapafuni.

Mungu, asili ya neema, anatumia utu wa Mwokozi atujalie neema, kama vile mwanamuziki bora anavyotumia ala atushirikishe aliyonayo moyoni, au mwanafalsafa bora anavyotumia ufasaha wa lugha atokeze mawazo yake. Utu wa Yesu ni chombo bora, chenye kujua na kutaka kutumika, kilichounganika moja kwa moja na umungu ili kutushirikisha neema zote tunazojaliwa, ambazo zote alitustahilia msalabani. Kwake zinatoka neema zote za mwanga, mvuto, faraja na ushujaa, tunazozihisi na tusizozihisi. Ni nguvu ya mfululizo ambayo Mwokozi anachangia kila tendo linalostahili wokovu. Utendaji wake huo unawashirikisha wasioamini mianga ya imani, na Wakristo wakosefu neema ya kujuta inayowaalika kwenye kitubio. Lakini nguvu hiyo inapatikana hasa katika ekaristi, kwa kuwa sakramenti hiyo haina neema tu, bali inaye aliyetustahilia neema, tena ni sadaka yenye thamani isiyo na mipaka. Jambo hilo linatakiwa kusisitizwa, tunapoongelea chemchemi za maisha ya Kiroho kadiri ya Kanisa Katoliki.

Nguvu ya kutakasa inayotoka kwa Kristo katika Ekaristi hariri

Ili tufaidike na kumshukuru Bwana zaidi ni afadhali tufuate maneno ya Injili, tukikumbuka alivyowahi kutuahidia ekaristi kwa upendo; alivyotupatia katika karamu ya mwisho, alipoweka upadri; anavyoifanya upya kila siku katika misa; anavyobaki kati yetu kwa kudumisha uwemo wake halisi katika sakramenti; hatimaye anavyojitoa kwetu katika komunyo ya kila siku, hadi ile ya mwisho kabla hatujafa. Ukarimu wote huo wa Kimungu unatokana na upendo na kulenga ustawi wa utakatifu wetu.

Maneno aliyotuahidia ekaristi (taz. Yoh 6:26-69) yanatuonyesha kwa namna bora hizo nguvu hai za Mwokozi zinazotakiwa kutufanyia kazi na jinsi sisi tunavyotakiwa kuzipokea. Baada ya kuzidisha mikate, alisema, “Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani Mungu... Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima”. Basi wakamuambia, “Bwana, sikuzote utupe chakula hiki”. Yesu akawaambia, “Mimi ndimi chakula cha uzima... Lakini niliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini... Amin, amin, nawaambia: yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu... Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli... Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima”. Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena. Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Simoni Petro akamjibu, “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele”. Ahadi hiyo ya ekaristi inadokeza yale yote ambayo sakramenti kuu inakusudiwa kuzaa ndani mwetu.

Simulizi la kuiweka linatuonyesha uzito wa ahadi hiyo: “Walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, ‘Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu’. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, ‘Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi’” (Math 26:26-28). Maneno ya ahadi yanaangazwa na hayo yaliyomtuza Mtume Petro kwa sababu alisema kwa imani, “Wewe unayo maneno ya uzima wa milele”. Hakika karamuni Yesu alikuwa na neno lenye nguvu kuliko kawaida, neno lenye kugeuza dhati ya mkate kuwa mwili wake ili abaki kati yetu kisakramenti.

Papo hapo aliweka upadri ili kudumisha sadaka ya msalabani hadi mwisho wa nyakati. Kwa kusema, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk 22:19; 1Kor 11:24-25) aliwapa mitume uwezo wa kugeuza, wa kutolea sadaka ya ekaristi, ili watushirikishe matunda, stahili na malipizi yake mpaka mwisho wa dunia. Bwana wetu ndiye kuhani mkuu anayeendelea kujitoa, “maana yu hai sikuzote ili awaombee” (Eb 7:25). Anafanya hivyo hasa katika sadaka takatifu, ambayo ina thamani isiyo na mipaka, kutokana na kuhani mkuu anayeitoa, sadaka inayotolewa, na damu azizi inayomwagwa kisakramenti. Papo hapo Yesu anamtolea Baba yake ibada, dua, malipizi na shukrani zetu, yaani kwa jumla matendo yote ya Mwili wake wa fumbo yanayostahili wokovu.

Upendo wa Kristo umemfanya atupatie ekaristi si mara moja tu, bali kila siku upya. Angeweza kuamua misa iadhimishwe mara moja au mbili tu kwa mwaka mahali fulani patakatifu ambapo waamini waende kutoka nchi za mbali. Kumbe kila nukta misa kadhaa zinatolewa duniani kote. Hivyo analijalia Kanisa lake neema linazozihitaji kulingana na nyakati linazoishi, tuwe na nguvu ya kukabili hatari kubwa tulizonazo.

Kristo anarudi kila siku, kweli, kati yetu, si kwa muda wa saa moja, tunapoadhimisha sadaka ya ekaristi, bali kusudi abaki nasi mfululizo katika tabenakulo kama mwenzetu hapa uhamishoni, akitungojea kwa hamu ya kutusikiliza, na kumtolea daima Baba yake ibada yenye thamani isiyo na mipaka.

Hatimaye komunyo ni utimilifu wa kujitoa zawadi. Wema kwa jinsi ulivyo unaelekea kuenea; unavutia na kujishirikisha. Hiyo ni kweli hasa kwa wema mwangavu wa Mungu na Kristo wake. Katika komunyo Mwokozi anatuvuta kwake na kujitoa kwetu, si sote kwa jumla, bali tukitaka kwa kila mmoja wetu, tena tukiwa waaminifu kwa ndani zaidi na zaidi. Anajitoa si kusudi alingane nasi bali sisi tuzidi kulingana naye. “Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?” (1Kor 10:16). Tunaupokea uhai wenyewe.

Ushirika huo unatakiwa kutuunganisha na Kristo zaidi na zaidi, ukikuza ndani mwetu unyenyekevu, imani, tumaini na hasa upendo, ili moyo wetu ulingane na ule wa Mwokozi aliyekufa kwa kutupenda. Kwa maana hiyo komunyo zetu zinatakiwa kuwa na upendo mwingi zaidi na zaidi, kwa kuwa kila mojawapo inatakiwa si tu kutunza, bali kustawisha upendo wa Mungu ndani mwetu na hivyo kutuandaa kumpokea Bwana kesho yake kwa utashi motomoto zaidi (umotomoto wa hisi ni wa ziada tu: tunaweza kupokea vizuri ekaristi katika ukavu mkubwa wa hisi, kama ilivyokuwa bora sala ya Yesu bustanini). Inatakiwa kuwa kama mbio ya kumuendea Mungu ambayo izidi kuwa ya kasi kadiri tunavyomkaribia na kuvutiwa naye, kama vile vitu vinavyoanguka kwa kasi kadiri vinavyokaribia ardhi inayovivuta.

“Ninakuabudu Mungu wangu, / unayejificha altareni. / Ninakutolea moyo wangu, / usiofahamu siri yako... / Ewe Yesu nipe pendo lako, / tumaini kwako na imani. / Umeteswa nini, Bwana mwema, / kwa kunipa mkate wa uzima? / Yesu unifiche ndani yako, / ili nilionje pendo lako. / Yesu pelikane nitazame, / na kwa damu yako nitakase. / Tone moja ndilo linatosha, / na dunia yote yaokoka. / Ndani ya mafumbo Yesu yumo. / Atafumbuliwa kwangu lini? / Nikuone, Yesu, uso wako, / nishiriki nawe heri yako” (Thoma wa Akwino). Mtu akiiishi hivyo ekaristi kila siku, atafikia urafiki wa ndani naye, na kuzama zaidi na zaidi katika fumbo kuu la altare, chemchemi ya neema mpya daima, ambamo vizazi vyote vinatakiwa kutuliza kiu yao na kupata nguvu ya kufikia mwisho wa safari ya kuelekea uzima wa milele. Nabii Eliya alipoishiwa nguvu alizipata upya kwa kula mkate kutoka mbinguni, akatembea mpaka mlima Horebu, unaomaanisha kilele cha ukamilifu. Kristo anatuambia kama alivyomuambia Augustino, “Ndimi mkate wa watu wazima... Kua, nawe utanila; lakini hutanigeuza ndani mwako, kama chakula cha mwili wako; bali wewe utageuzwa ndani mwangu”. Anayemshiriki kweli Kristo anazidi kuunganishwa naye, hata akaishi kwa mawazo yake na kwa upendo wake akaweza kusema, “Kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida” (Fil 1:21), kwa sababu ni mlango wa uzima usio na mwisho.

Kuungana na Kristo zaidi na zaidi na utakatifu hariri

Kadiri ya watakatifu, mafundisho hayo kuhusu kuungana na Kristo zaidi na zaidi yatamfaidisha ajabu anayeamua kuyaishi.

Kwanza, ili tufie dhambi na matokeo yake tukumbuke kwamba “tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake… ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena” (Rom 6:4-6); “hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake” (Gal 5:24). Ndiyo hatua ya kufia dhambi kwa ubatizo na toba.

Pili, kwa mwanga wa imani na uvuvio wa Roho Mtakatifu, tunatakiwa kuvaa “utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba... Basi... jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu… Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu” (Kol 3:10-14). Ndiyo hatua ya mwanga ya wanaomuiga Yesu kwa kujipatia misimamo yake, roho ya mafumbo yake: ya mateso, kifo na ufufuko. “Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo” (Fil 3:8).

Tatu, njia hiyo waliyoifuata watakatifu wote inafikishia kuungana na Mwokozi kama kwa kudumu: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu” (Kol 3:1-3). Hapo amani yake itamtawala mtu anayependa kumuambia, “Bwana, nipe nafsi yako, pokea nafsi yangu”. Elekeo la roho yetu kwake linamjulisha hamu yetu, likimtolea udhaifu wetu, nia yetu njema, azimio letu la uaminifu, kiu yetu ya nafsi yake. Ndiyo hatua ya kuzama kwa upendo katika mafumbo, kama utangulizi wa heri ya kuonana na Mungu uso kwa uso.

Wengi wanadanganyika wataweza kufikia muungano naye pasipo kumkimbilia mfululizo Bwana Yesu: hao watafikia tu ujuzi wa mbali wa Mungu, si ule ujuzi mtamu ambao unaitwa hekima na ni kama kumng'amua yeye na maongozi yake hata katika mambo madogo. Tusiache kamwe kwa makusudi kuzingatia utu wa Mwokozi katika sala: kwa kuwa ndiye njia ya kufikia umungu wake. Tufikirie mara nyingi utajiri wa Kiroho wa Yesu katika akili, utashi na hisi zake, ili tuzidi kuelewa neno lake: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima” (Yoh 14:6).

Tanbihi hariri

  1. Mystici corporis Christi, a papal encyclical issued by Pope Pius XII, sections 60–62

Marejeo hariri