Ukamilifu wa Kikristo


Ukamilifu wa Kikristo ni jina la mafundisho mbalimbali katika Ukristo yanayofafanua mchakato wa kulenga ukomavu wa kiroho. Lengo ni kuungana na Mungu kwa upendo kamili ambao ndio utakatifu.[1][2]

Yesu katika Maneno ya Buriani aliahidi kumtuma Roho Mtakatifu kwa wanafunzi wake; mchoro wa Duccio, 13081311.

Mizizi ya mafundisho hayo ni maandishi ya Mababu wa Kanisa, hasa Irenei,[3] Klementi wa Aleksandria, Origen, halafu Makari wa Misri na Gregori wa Nisa.[4]

Hata hivyo baadhi ya madhehebu ya Kiprotestanti, kama Walutheri na Wakalvini, wanaona mafundisho ya namna hiyo hayapatani na yale juu ya wokovu kwa njia ya imani tu. (Rom 7:14–25; Fil 3:12)[5][6].

Ukamilifu ulivyofikiriwa hariri

Lengo la maisha ya Kiroho, si lengo kuu ambalo ni uzima wa milele, bali lile linaloweza kufikiwa duniani, ni ukamilifu ambao Kikristo unapatikana hasa katika upendo. Tukumbuke kwa ufupi dhana nyingine mbili za zamani, tukitambua sura zilizonazo siku hizi. Hivyo tutaweza kuthamini zaidi ubora wa jibu la Injili, pia kwa sababu hizo mbili zina chembe za ukweli ambazo chini ya upendo zinapata thamani.

Zamani watu wasiostaarabika waliona ukamilifu wa binadamu unategemea nguvu, moyo, uhodari, tunavyoona katika hadithi zao. Mtazamo huo umechanganyikana na kiasi kikubwa cha kiburi, na pengine cha utovu wa haki. Kuna waamini motomoto wanaosafisha dhana hiyo na kuihamishia upande wa roho wakijiona askari wa Kristo na kujali mno kifodini. Kumbe ubora wa kifo hicho hautegemei kuwa tendo la nguvu, bali kuwa ishara angavu ya upendo mkuu. Karne tatu za dhuluma za Kanisa la mwanzoni zilikuwa za uhodari, lakini hasa za upendo: ndio unaotofautisha wafiadini wa Kikristo na mashujaa wa Kipagani.

Kwa mtazamo wa namna hiyo wengine wanaona ukamilifu umo hasa katika ugumu wa maisha (mafungo, makesha n.k.): huo unaweza kuhitajiwa na utawa unaokusudia zaidi sala na sadaka, lakini si lengo bali njia tu ya ustawi. Maisha makamilifu zaidi si yale magumu zaidi, bali yale yenye lengo bora na njia za kufaa zaidi kulifikia. Maisha ya Kiroho yanahusu uadilifu kuliko ugumu. Kwanza si kila tendo gumu ni adilifu: pengine ni juhudi ya ushupavu tu. Halafu uadilifu ni mgumu mara nyingi, lakini si daima: vitendo kadhaa vya upendo vinatendeka pasipo shida, kwa msukumo mkubwa wa roho, hata hivyo vina stahili kubwa kwa kuwa vinatokana na upendo mkubwa. Nguvu ni sifa muhimu ya askari, lakini si ukamilifu wa mtu kama mtu na wa Mkristo kama Mkristo. Inahitajika kwa ukamilifu, lakini juu yake kuna haki kuhusu wengine, kuna busara inayoongoza maadili yote ya kiutu, na hasa kuna maadili yanayomlenga Mungu moja kwa moja: imani, tumaini na upendo. Basi, hatuwezi kukubali kwamba ukamilifu umo hasa katika nguvu, kwa kuwa hiyo si ukamilifu wa akili yetu kuhusu ukweli mkuu, wala si ukamilifu wa utashi wetu kuhusu wema mkuu, ila ni adili linaloshinda hofu tu ili tuzidi kufuata njia nyofu hata kwenye shida na hatari.

Ikiwa ukamilifu haumo hasa katika nguvu, je, utapatikana katika hekima? Ndivyo walivyodhani wanafalsafa wengi, wakisema binadamu anatofautiana na viumbe vilivyo chini yake kwa akili aliyonayo; kwa hiyo ukamilifu wake ni hasa ule wa akili yake, yaani hekima au ujuzi mkuu. Hakika hekima inahitajika kwa ukamilifu, lakini si kweli kwamba kumjua Mungu kinadharia kunafuatwa daima na upendo kwake. Mwanafalsafa, hata kama ana akili na wazo sahihi kuhusu Mungu kama asili na lengo kuu la ulimwengu, anaweza akawa mwovu. Ukweli ni ukamilifu wa akili, lakini si ukamilifu wa mtu mzima, wala si jema pekee la binadamu. Elimu inaweza kuwepo pasipo upendo kwa Mungu na kwa jirani; hapo “huleta majivuno” (1Kor 8:1). Ukamilifu wa mtaalamu kama mtaalamu si ule wa binadamu kama binadamu, wala ule wa Mkristo kama Mkristo. Tusichanganye ukamilifu wa akili na ule wa mtu mzima unaohitaji kunyosha utashi uelekee lengo kuu. Tofauti na sanaa na sayansi, uadilifu unadai utashi unyoshwe: hapo tu mtu ataitwa mtu mwema, si tu mchoraji, mjenzi au mganga stadi. Hatimaye hapa duniani kumpenda Mungu ni bora kuliko kumjua. Ujuzi unamvuta kwetu na kumbana ndani ya mipaka ya mawazo yetu finyu; kumbe upendo wa Mungu unatuvuta kwake na kutufanya tupende ndani mwake hata yale tusiyoweza kuyajua sawasawa, kwa sababu tuna hakika ya kuwa maisha yake ya ndani yaliyofichika kwetu yanapendeza kupita kiasi.

Dhana ya kuwa hekima ndiyo ukamilifu inajitokeza leo katika wale wanaojali elimu kuliko yote. Hata baadhi ya Wakristo wanaelekea kudhani inawezekana kuufikia ukamilifu haraka kwa kusoma maandishi mengi ya watakatifu, bila kujitahidi zaidi kutekeleza maadili yao, wala kukumbuka kwamba sala ya kuzama katika mafumbo inatakiwa kujaa upendo upitao maumbile na kujikana. Sala hiyo si ukamilifu hasa, na kuwa huo umo katika kuungana na Mungu kwa upendo; ila kumtazama kwa upendo ni njia iliyounganika na lengo hilo kwa sababu kunatuandaa moja kwa moja tuungane naye. Hivyo tusilenge hasa sala hiyo, bali Mungu mwenyewe ambaye apendwe kuliko yote.

Basi, ukamilifu unahitaji kweli nguvu na hekima, lakini pia maadili yote ya Kimungu na ya kiutu, pamoja na vipaji saba vya Roho Mtakatifu. Basi, ukamilifu umo katika jumla ya maadili, mradi jumla hiyo iwe imepangwa vizuri kama muundo hai, na kati ya maadili liwepo moja lenye kuyatawala, kuyaongoza na kuyahuisha yote na kuelekeza juhudi zake zote kwenye lengo kuu. Kama ni hivyo, ukamilifu umo hasa katika adili hilo kuu ambalo mengine yote yanapaswa kulisaidia. Lenyewe ni upendo.

Ukamilifu kadiri ya Biblia hariri

Mungu amefunua kwa namna mbalimbali kwamba amri inayotawala maagizo na mashauri yote ni ile ya upendo iliyotajwa tayari katika Agano la Kale: “Mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote” (Kumb 6:5). “Umpende jirani yako kama nafsi yako. Mimi ndimi Bwana” (Law 19:18). Ndicho kipeo kikuu kuliko nguvu na hekima, chenye nguvu ya aina nyingine, na hekima ya kweli na ya juu zaidi. “Kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusameheana… Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu” (Kol 3:12-14)”. Upendo ndio kifungo cha ukamilifu kwa sababu unatuunganisha na Mungu na kudumu milele; ndio unaohuisha maadili yote yawe na stahili kwa kuyalengesha kwa Mungu mpendwa kuliko yote.

Mtume Paulo alikuwa na hakika kwamba upendo ni bora kuliko maadili mengine, vipaji vya Roho Mtakatifu na karama mbalimbali: “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu” (1Kor 13:1-3). Pasipo upendo karama hazisaidii kitu kwa uzima wa milele, kwa sababu nisipopenda sitekelezi amri ya kwanza ya Mungu, silinganishi matakwa yangu na ya kwake, napotoka mbali naye katika njia isiyoelekea moyo wake. Basi, katika wokovu “kama sina upendo, si kitu mimi”, sistahili kitu ingawa kwa mahubiri na miujiza ninaweza nikasaidia watu waokoke.

Kwa maana hiyo Augustino alisema, “Penda, halafu tenda lolote utakalo”, nalo litakustahilisha uzima wa milele. Lakini uwe na upendo halisi, kwa sababu hakuna lililo baya kuliko upendo bandia (unaofumba macho usitimize wajibu wake dhidi ya maovu: huo ni udhaifu au ni miguso ya kibinadamu tu inayotaka kukubaliwa na upendo halisi na kuuambukiza). Kati ya mapambano makuu ya leo, mojawapo ni lile kati ya upendo halisi na upendo bandia, ambao unatukumbusha Makristo wa uongo wanaozungumziwa na Injili. Uharibifu mbaya zaidi ni ule unaohusu yaliyo bora, kama vile upendo ulio adili kuu. Kwa kuwa yale yanayoonekana tu mema ni ya hatari kadiri ya ubora wa mema halisi yanayoigizwa nayo (k.mf. kipeo cha wanaotaka kuunganisha madhehebu ya Kikristo kwa kupunguza kweli za imani). Ikiwa kwa upumbavu au woga wale wanaotakiwa kuwakilisha upendo halisi wanayakubali kwa namna moja au nyingine yale yanayoficha upendo bandia, yanaweza yakatokea mabaya yasiyopimika, makubwa kuliko yale yanayosababishwa na watesi waliojitokeza wazi.

Tofauti na upendo bandia, ule halisi una maadili yote ndani yake na chini yake hivi kwamba yanaonekana kama namna au sura mbalimbali za upendo kwa Mungu na kwa jirani. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote; hutumaini yote, hustahimili yote” (1Kor 13:4-7).

Kwa upendo huo tunakuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Kadiri tunavyompenda Mungu tunamfahamu na kama kumng’amua kwa ujuzi upitao maumbile unaoitwa hekima ya Kimungu. “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef 3:17-19).

Mafundisho hayohayo tumepewa na Mtume Yohane: “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake… Yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake” (1Yoh 4:16,21). Mtume Petro aliandika vilevile, “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana, kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi” (1Pet 4:8). Alivyowahi kusema Yesu, “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).

Kadiri ya mafundisho hayo, ukamilifu haumo hasa katika unyenyekevu, ufukara wala ibada, bali katika upendo unaofanya matendo ya maadili mengine yote yastahili. Ufukara si ukamilifu, ila ni njia ya ukamilifu. Basi, njia haitafutwi kwa ajili yake, bali kwa ajili ya lengo, nayo ni bora si kadiri ya ukubwa wake, bali kadiri inavyolingana na lengo, kama vile daktari mzuri ni yule anayeponya, si anayetoa matibabu mengi zaidi. Ni vivyo hivyo kuhusu unyenyekevu unaotuinamisha mbele ya Mungu ili tupokee kwa mikono miwili msaada wake ambao utuinue hadi kwake. “Unyenyekevu ni adili la msingi kwa kuwa unaondoa kizuio kikuu, yaani kiburi, lakini umo chini ya maadili ya Kimungu yanayotuunganisha na Mungu” (Thoma wa Akwino). Hata adili la ibada, linalompatia heshima inayotakiwa, halistahili lisipohuishwa na upendo. Si adili la Kimungu kwa sababu halimhusu moja kwa moja yeye, ila ibada kwake. Tukisahau hayo tunaweza tukazingatia liturujia kuliko Mungu mwenyewe, mifano kuliko ukweli, namna ya kusali Baba Yetu kuliko maana yake: hapo utumishi wa Mungu ungepiku upendo wake.

Maelezo ya teolojia ya Kikatoliki kuhusu ukamilifu hariri

“Kila kiumbe ni kamili kadiri kinavyofikia lengo lake ambalo ndio ukamilifu wake wa mwisho. Sasa, lengo kuu la maisha ya binadamu ni Mungu, na upendo ndio unaotuunganisha naye, kadiri ya neno la Mt. Yohane: ‘Kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye’. Basi, ukamilifu wa maisha ya Kikristo umo hasa katika upendo” (Thoma wa Akwino). Imani na tumaini si kiini cha ukamilifu, kwa sababu vinaweza kuwepo katika mtu ambaye kwa dhambi ya mauti amepotosha utashi wake mbali na Mungu. Vinabaki ndani mwake kama mzizi wa mti uliokatwa na ambao unaweza kuchipua tena.

Thoma akaongeza, “Ukamilifu umo hasa katika upendo kwa Mungu, halafu katika upendo kwa jirani, kwa kuwa ndio amri kuu za sheria ya Kimungu”. Hatutaweza kamwe kusisitiza mno neno la Bwana: “Amri mpya nawapa: Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yoh 13:34-35). Ndiyo dalili kuu ya ustawi wa upendo wa Mungu mioyoni mwetu: “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa… Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake” (1Yoh 3:14-15).

Tusisitize neno moja la Thoma wa Akwino, la kwamba hapa duniani "Kumpenda Mungu ni bora kuliko kumjua". Yeye alikiri kuwa akili ni bora kuliko utashi unaoongozwa nayo, kuwa ndiyo kipawa cha kwanza kinachomtofautisha binadamu na mnyama, tena kuwa mbinguni heri itatokana hasa na akili kumuona Mungu moja kwa moja, kwa kuwa ndiyo njia ya kumpata milele: kuzamisha akili yetu katika vilindi vya maisha yake ya ndani yakiwa wazi tu. Mungu atajitoa kwetu moja kwa moja, nasi tutajitoa kwake; tutakuwa naye kama mali yetu, nasi tutakuwa mali yake, kwa kuwa tutamfahamu kama anavyojifahamu na anavyotufahamu. Upendo wenye heri utatokana na huo mtazamo wa moja kwa moja wa umungu, tena utakuwa tokeo la lazima, kwa kuwa utashi wetu utavutwa na uzuri wa Mungu moja kwa moja. Tutaona wema wake mkuu kwa namna wazi hivi hata tusiweze kutompenda; hatutaona kisingizio chochote cha kusimamisha kwa nukta moja tendo hilo la upendo lililo juu kuliko hiari yetu, na ambalo halitapimwa na muda, bali na umilele tulioshirikishwa, ile nukta pekee isiyokwisha kamwe ya Mungu kuwepo pasipo badiliko. Upendo kwake na furaha ya kuwa naye kama mali yetu vitatokana kwa lazima na heri ya kumuona.

Pamoja na hayo, mwalimu huyo alisema ukamilifu wa Kikristo hapa duniani umo hasa katika upendo ambao ni adili la utashi, si upande wa akili. Ni kwamba kipawa fulani kinaweza kuwa bora kuliko kingine kwa umbile, lakini tendo fulani la hicho cha pili linaweza kuwa bora kuliko mojawapo la hicho cha kwanza. Kwa mfano uwezo wa kuona ni bora kuliko ule wa kusikia, na upofu ni ulemavu mkubwa kuliko uziwi; lakini kusikiliza muziki bora kuna thamani kuliko kuona vitu vya kawaida. Vivyo hivyo, ingawa kwa umbile akili ni bora kuliko utashi, hapa duniani kumpenda Mungu ni bora kuliko kumjua, hivi kwamba mtakatifu ambaye hana elimu lakini ana upendo mkubwa kwa hakika ni mkamilifu kuliko mwanateolojia mkuu mwenye upendo mdogo. Jambo hilo, ambalo Wakristo wote wanalielewa kwa urahisi, tukilifikiria kwa makini tutaliona ni ukweli wa thamani unaoweza kuthibitishwa na madondoo mengi ya Biblia na ya walimu wa Kiroho.

Huo ubora wa upendo hapa duniani unatokana na kwamba “kazi ya akili yetu inafanyika kwa kujichorea ukweli uliojulikana, kumbe utashi wetu unavutwa na upendo ukiendee kilichopendwa jinsi kilivyo. Alivyosema mwanafalsafa, wema ulio lengo la utashi umo ndani ya vitu, kumbe ukweli umo hasa katika roho yetu” (Thoma wa Akwino). Kwa hiyo tunapomjua Mungu, kwa namna fulani tunambana ndani ya mipaka ya mawazo yetu finyu ili tujichoree alivyo; kumbe tunapompenda, sisi ndio tunaovutwa naye na kuinuliwa kwake jinsi alivyo kweli. Basi, duniani na toharani upendo kwa Mungu ni bora kuliko kumjua; unahitaji kumjua kwanza, lakini unapita ujuzi huo. Tena tokea hapa duniani upendo wetu unamfikia Mungu na kuambatana naye moja kwa moja: “Ujuzi wetu unamuinukia Mungu kupitia viumbe, kumbe upendo wetu unawashukia viumbe kutoka kwa Mungu” (Thoma wa Akwino). Hatimaye, sisi tunapenda ndani ya Mungu hata yale tusiyoyajua, kwa sababu tuna hakika ya kuwa ndiye wema wenyewe. Hivyo tunaweza kumpenda kuliko tunavyomfahamu; tena ndani mwake tunapenda zaidi yale yaliyofichika, kwa kuwa tunaamini ndiyo maisha yake ya dhati yanayopita uwezo wowote wa kujua. Basi, hapa duniani upendo kwa Mungu unashinda ujuzi unaomhusu. Hilo ni ajabu linalotuonyesha upendo ulivyo mkuu kuliko imani na tumaini, kuliko ujuzi wowote tunaoweza kuwa nao duniani, na hata kuliko tendo la kuzama katika sala, kwa kuwa hilo pia halifikii kumpata Mungu jinsi alivyo, na utamu ulilonalo unatokana na upendo unaoliongoza. Ndiyo sababu upendo ni kifungo cha ukamilifu: hakuna adili linalotuunganisha na Mungu kwa undani kuliko hili wala pasipo hili.

Pamoja na mapokeo yote ya Kanisa Katoliki tukariri kwamba ukamilifu wa Kikristo umo hasa katika upendo wa vitendo ambao unatuunganisha na Mungu katika ukavu kama katika faraja, na kuzaa kila aina ya vitendo vyema. Kwa usahihi zaidi ukamilifu haumo hasa katika adili lenyewe la upendo, bali katika utekelezaji wake ambao kwa waliokamilika ni wa kudumu. Hii ni kwa sababu lengo la adili ni kutekelezwa, na ukamilifu umo katika muungano wa kudumu na Mungu. Kumbe Watulivu walikataa utendaji wowote kwa kisingizio cha kumuachia Mungu tu kutenda; hali yao ya kutotenda ilikuwa ya kujitakia, si ya kujaliwa: hivyo walifuta juhudi wakasinziasinzia tu! Kinyume chao, wengine wanapindua mpangilio wa upendo wakidhani ukamilifu umo katika kusaidia watu, wakati upendo kwa Mungu ni wa juu kuliko ule kwa jirani ambao ni ishara na tunda lake tu. Wengine tena, wanaozingatia zaidi maisha ya Kiroho, wanazidisha matendo ya ibada badala ya kulenga sala sahili ya mapendo ambayo ni kama tendo moja tu linalodumu kwa muda fulani.

Basi, rohoni mwetu upendo ushike nafasi ya kwanza, juu kuliko hamu ya ujuzi na ya maendeleo yoyote ya kibinadamu; hapo utazidisha nguvu zetu zote kwa kumtumikia Mungu na jirani.

Pamoja na hayo, hapa duniani upendo hauwezi kudumu kama mbinguni. Ni kwamba Mungu tu anaweza kujipenda anavyostahili, kama vile yeye tu anavyoweza kujifahamu kikamilifu; lakini watakatifu wa mbinguni, bila kumpenda anavyostahili, wanampenda kwa nguvu zao zote, kwa upendo wa kudumu moja kwa moja. Hiyo haiwezekani duniani, hasa kutokana na usingizi. Ukamilifu unaowezekana hapa ni ule unaozuia yale yote yanayopingana na upendo wa Mungu (yaani dhambi za mauti) au yanayofanya upendo usimuelekee kikamilifu. Wanaoanza maisha ya Kiroho na wale wanaoendelea wanalenga huo muungano na Mungu ambao ni maalumu wa waliokamilika: upendo wao hauzuii tu dhambi za mauti na dhambi nyepesi za makusudi, bali pia kasoro za hiari, k.mf. juhudi pungufu katika kumtumikia Mungu na mazoea ya kutenda kwa namna pungufu (kulingana na talanta zao) na ya kupokea sakramenti pasipo utashi kuitamani zaidi.

Upendo wa waliokamilika kwa jirani unaenea si kwa wote jumla tu, bali ikipatikana nafasi kwa kila mtu, hata adui. Tena ndani mwao upendo wa kidugu una nguvu ya kujitolea hata mali na uhai, kwa kuwa Bwana ametuambia, “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yoh 15:12). Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika, “Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu” (2Kor 12:15). Ili tufikie hatua hiyo vinahitajika: kazi kubwa juu ya nafsi zetu, juhudi halisi, moyo wa kujikana na kujikatalia hivi kwamba mapendo yetu yaache kuteremkia vitu vya dunia au ubinafsi, na badala yake yazidi kumuinukia Mungu kwa usafi na nguvu. Roho ikiacha kushuka, inapanda kwa Mungu: haiwezi kubaki pale ilipo; sheria yake, kama ile ya moto, ni kupanda, si kushuka.

Hapa duniani upendo wa waliokamilika, ingawa haudumu moja kwa moja kama ule wa mbinguni, unatenda karibu mfululizo na kwa namna ya ajabu: “Upendo ni jambo kubwa sana; ni jema kushinda mema yote. Upendo peke yake hugeuza mazito kuwa mepesi, hubeba magumu kwa urahisi… Upendo una hamu ya kupaa, hautaki kuzuiwa na mambo ya chini… Upendo umetoka kwa Mungu, hauwezi kutulia isipokuwa kwa Mungu pekee, mbali na viumbe vyote. Mwenye upendo huenda kama kwa kuruka, huenda mbio kwa furaha, yu huru, hazuiliki, hutoa yote kusudi apewe yote; katika mambo yote yeye hupata yote, kwa sababu humtegemea yule aliye juu kabisa, ndiye asili ya mema yote… Mara nyingi upendo haujui kiwango, huchangamka kupita kiasi… Upendo hukesha unapolala, haupatwi na usingizi; unapochoka haupumziki… Kama moto unaoteketea, kama mwenge unaowaka huruka juu, hupenya kila mahali” (Kumfuasa Yesu Kristo III,5:3-5).

Ndiyo maisha ya watakatifu, na ndiyo wito wetu, kwa kuwa tunaitwa mbinguni, ambako kuna watakatifu tu. Ili tufike huko tunapaswa kutakasa kila tendo la siku zetu, tukikumbuka kwamba juu ya mfululizo wa matukio ya kila siku (ya kupendeza na ya kuchukiza, yaliyotarajiwa au la) kuna mfululizo sambamba wa neema za msaada tunazojaliwa nukta kwa nukta ili tufaidi upeo matukio hayo. Hapo tutayaona si tu upande wa hisi au wa akili iliyopotoshwa na umimi, bali upande wa roho kwa imani. Yatakuwa mafundisho yanayotekeleza yale ya Injili, na polepole maongezi kati ya Bwana na sisi yataelekea kufululiza: ndiyo maisha halisi ya Kiroho na mwanzo wa uzima wa milele.

Ukamilifu wa Kikristo unadai upendo mkubwa hariri

Baadhi ya wanateolojia walijiuliza kama ukamilifu unadai upendo mkubwa au unaweza kupatikana pasipo kiwango kikubwa cha adili hilo. Jibu la hakika ni kwamba, kama vile utu uzima unadai nguvu za mwili nyingi kuliko za mtoto (ingawa kwa nadra mtoto mwenye afya ana nguvu kuliko watu wazima kadhaa), hata ukamilifu unadai upendo mkubwa kuliko ule wa wanaoanza (ingawa mwanzoni mwa maisha ya Kiroho, anayeitiwa utakatifu mkuu, anaweza akawa tayari na upendo mkubwa kuliko baadhi ya waliokamilika). Kanisa Katoliki linafundisha hivyo kwa kuwa ukamilifu unapatikana tu baada ya kutekeleza maadili kwa muda mrefu, na kwa utekelezaji huo maadili yanastawi zaidi na zaidi. Ikiwa mwanzoni “upendo wa kiwango cha chini unaweza kushinda vishawishi vyote” (Thoma wa Akwino), baadaye unavishinda kweli na kuzidi kuwa na nguvu. Haiwezekani kumfikiria Mkristo mkamilifu, aliye juu kuliko wanaoanza na wanaoendelea, asiye na upendo mkubwa, ingawa kupima kiwango kinachotakiwa ni kazi ya Mungu tu.

Msingi mwingine wa fundisho hilo ni kwamba upendo unastawi kwa nguvu kuliko kwa uenezi. Viwango vitatu vya upendo vinavyowafaa wanaoanza, wanaoendelea na waliokamilika, ni viwango vya nguvu ya adili hilo, ambalo linazidi kuzuia dhambi nyepesi na kututenganisha na malimwengu ili tuambatane na Mungu. Hata hivyo mtu mmoja anaweza akakwepa dhambi hizo kuliko mwingine mwenye kiwango kilekile cha upendo, kwa sababu kwa wakati huo ana juhudi nyingi zaidi au halazimiki kupambana zaidi na tabia yake, uchovu na upinzani. Teresa wa Yesu alipokuwa nje ya monasteri katika nafasi zisizotazamiwa ilimtokea kutenda dhambi nyepesi nyingi zaidi, lakini pia kujipatia stahili nyingi zaidi kutokana na majaribu aliyoyashinda. Ni kama mtu ambaye akipanda mlima mrefu, inamtokea kuanguka kuliko anapotembea mahali tambarare, lakini ana stahili ya kutenda kazi ngumu ya kupanda.

Basi, ukamilifu unadai upendo mkubwa unaopatikana tu kwa kushinda kwanza vishawishi vingi na kujipatia stahili nyingi. “Ukamilifu umo katika kumpenda kikamilifu Mungu na kujidharau... Kuna watu wanaoridhika na aina yoyote ya kukusanya mawazo na ya kuongoka; wengine wanaishia katika kutekeleza maadili kwa ukamilifu mkubwa au mdogo, na kuwa waaminifu katika sala na kujinyima. Wanachokikosa ni kujishusha, kuwa mafukara au kujikana na kuwa safi Kiroho… Wanakwepa msalaba ambao ungewalinganisha na Bwana wetu Yesu Kristo. Wanajifanya lengo ndani ya Mungu, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha upendo… Ningependa kuwa na uwezo wa kuwathibitishia watu wote wa Kiroho ukweli huu: kwamba njia ya Mungu si kuzidisha mawazo, mbinu na maonjo, ingawa kwa namna fulani wanaoanza wanahitaji vitu hivyo. Ila jambo moja tu ni la lazima kabisa, yaani kuweza kujikana moja kwa moja, kwa ndani na kwa nje, kujitoa mhanga kwa Yesu Kristo kama sadaka kamili ya kuteketezwa. Katika zoezi hilo tu tutayakuta hayo mengine yote na mengi zaidi tena. Kumbe, tukipuuzia zoezi hilo, ambalo ni muhtasari na mzizi wa maadili, tutakuta tu vitu visivyo muhimu, na maendeleo yatakwama, hata tukiwa na mawazo na neema za kimalaika… Mtu wa Kiroho akifaulu kujiangamiza, yaani kutekeleza unyenyekevu kamili, hapo muungano wake na Mungu utatimia, nao ndio hali bora tena kuu tunayoweza kuifikia katika maisha haya” (Yohane wa Msalaba).

Mafundisho hayo yanalingana na yale ya Thoma wa Akwino alipoeleza ukamilifu kuwa “hali ya wale ambao wanalenga hasa kuambatana na Mungu na kumfurahia, na ambao wanatamani kufa ili kuishi na Kristo”, wakikabili magumu kwa utukufu wa Mungu na wokovu wa watu. Basi, pasipo juhudi kubwa haiwezekani kufikia upendo mkubwa, hata kwa miaka ya kukomunika kila siku na kutenda mema mapungufu. Kwa njia hizo tunaweza kujidumisha katika neema inayotia utakatifu au kuinuka mapema baada ya kutenda dhambi ya mauti, lakini hatutafikia kamwe upendo mkubwa.

Ukamilifu unadai ushujaa katika maadili yote hariri

Ikiwa upendo kwa nchi yetu unatudai ushujaa inapopatwa na hatari, zaidi ukamilifu wa Kikristo unadai ushujaa katika maadili, walau upande wa nia. Kwa msaada wa Mungu, kila Mkristo anapaswa kuwa tayari auawe kwa ajili ya imani, kama atajikuta analazimika kuchagua aikane au kuteswa. Padri aliyewekwa wakfu awachunge watu anapaswa kuhatarisha uhai wake ili kuwaletea sakramenti wakiwa na shida kubwa nazo (k.mf. kwenda kuwaungamisha wenye tauni). Zaidi tena askofu, katika nafasi kadhaa anapaswa kutoa uhai wake kwa ajili ya kundi lake. Tunapaswa pia kuwapenda maadui wetu na kuwasaidia wakiwa na shida kubwa. Ushujaa huo wa lazima kwa wokovu unadaiwa zaidi na ukamilifu.

Mkristo akiwa mwaminifu katika wajibu wowote wa kila siku, awe na hakika kwamba Bwana atamsaidia kulingana na ugumu wa wajibu mkubwa wa dharura: “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia” (Lk 16:10). “Msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ileile yawapasayo kuyasema” (Lk 12:11-12). Vipaji vyake ni vya lazima kwa wokovu ili tupokee kwa dhati na kwa mikono miwili uvuvio wake wa pekee pale ambapo maadili hayatoshi, kwa kuwa nafasi ni ngumu zaidi. Lakini kuwa tayari rohoni kutekeleza maadili kwa ushujaa ni tofauti na kuwa nayo kwa kiwango cha ushujaa.

Tena ukamilifu unadai Mungu atakase hisi na roho ili kufuta kasoro za wanaoanza na za wanaoendelea. Yohane wa Msalaba alifafanua matakaso hayo yanavyowatokea wanasala wanaoitiwa ukamilifu mkuu kwa njia ya mkato; lakini mambo ya namna hiyo yanawatokea wengine pia ambao kwao matakaso hayo ya ndani yanaendana na huzuni na shida za utume. Mara nyingi katika majaribu hayo mtu anatakiwa kushinda kishujaa vishawishi dhidi ya usafi wa moyo na subira, halafu dhidi ya imani, tumaini na upendo. Hapo unadaiwa ushujaa fulani katika maadili, ambao baadaye unaweza na kutakiwa uongezeke.

Hatimaye, upendo wa Kikristo, kwa kuwa unalenga kutulinganisha na Mwokozi aliyesulubiwa kwa ajili yetu, unatakiwa kulenga ushujaa katika maadili. Hiyo inatokana na yale tuliyoyasema kwanza: tendo la kishujaa linalompasa Mkristo yeyote linalingana na lengo la upendo, yaani kumpenda Mungu kuliko yote. Kwa umbile lake, upendo huo unampenda kuliko uhai wa mwili, kwa hiyo unapaswa uwe tayari kumfia. “Upendo wa Mungu unafanya tutende bila kukoma na tuvumilie bila kuchoka” (Bernardo wa Clairvaux) hasa katika tabu za ndani na za nje ambazo watumishi wa Mungu wanapaswa kustahimili kwa utakaso wao na kwa kuchangia pamoja na Yesu wokovu wa watu.

Mtu anaweza akapinga mafundisho hayo akisema eti! Yangekuwa kweli Wakristo wanaofikia ushujaa wangekuwa wengi zaidi. Thoma alijibu hivi hoja ya namna hiyo kuhusu idadi ya wateule, “Jema linalolingana na umbile la binadamu wote kwa kawaida linafikiwa; lakini sivyo kuhusu jema linalopita umbile hilo”. Ni adimu kudumu maisha yote katika neema inayotia utakatifu, bila kutenda dhambi ya mauti baada ya ubatizo. Hata hivyo kwa mfumo wake neema inayotia utakatifu inalenga uzima wa milele, kwa hiyo idumu milele isiangamizwe kamwe na dhambi ya mauti. Ila tumepokea hazina hiyo katika chungu cha udongo, hivyo tamaa na kiburi vinaweza kufanya tuipoteze. Wengi wanaishi kijuujuu tu wakifuata hisi, na wachache tu wanafuata akili nyofu; hata hivyo kwa umbile lao wana akili, nayo neema inatakiwa kuwafanya waishi Kimungu. Vivyo hivyo upendo ni mbegu ya uzima wa milele, hivyo kwa mfumo wake unalenga ushujaa ili kudumu mwaminifu kwa Mungu.

Utakatifu mkubwa unadhihirishwa hasa na ulinganifu wa maadili yote, hata yale yaliyo mbalimbali zaidi. Kiumbile mmoja anaelekea nguvu, lakini si upole; mwingine ni kinyume. Kwa namna fulani umbile linaelekea daima upande mmoja, hivi kwamba linahitaji kukamilishwa na maadili tofauti. Kuunganisha nguvu kubwa na upole kamili, kupenda motomoto ukweli na haki pamoja na kuhurumia waliopotoka, kunathibitisha muungano wa dhati na Mungu, kwa kuwa yaliyogawanyika katika ulimwengu huwa yameunganika katika ufalme wake, na hasa ndani mwake mwenyewe. Utakatifu ni mfano mzuri wa umoja wa sifa mbalimbali zisizo na mipaka ndani ya ukuu wa Umungu.

Tanbihi hariri

 1. "Living a holy life". methodist.org.uk (kwa Kiingereza). Methodist Church of Great Britain. Iliwekwa mnamo 7 Januari 2020. John Wesley taught about 'Christian perfection.' He believed that a mature Christian can reach a state where the love of God reigns supreme in our heart.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 2. Oden, Thomas C. (2008). Doctrinal Standards in the Wesleyan Tradition: Revised Edition (kwa Kiingereza). Abingdon Press. uk. 190. ISBN 978-1-4267-6124-9.
 3. Against Heresies (Book IV, Chapter 39)
 4. Burnett, Daniel L. (15 Machi 2006). In the Shadow of Aldersgate: An Introduction to the Heritage and Faith of the Wesleyan Tradition (kwa Kiingereza). Wipf and Stock Publishers. ku. 116–117. ISBN 978-1-62189-980-8. The doctrine of entire sanctification has been present from the very beginnings of the Christian faith. Since the focus of the first few centuries was on the battle against Christological heresies, a systematic doctrine of sanctification did not emerge during that period. Its roots, however, were clearly present in such Early Church Fathers as Irenaeus, Clement of Alexandria, and Origen. By the fourth century the highly regarded writings of Gregory of Nyssa and Macarius the Egyptian... advocated understandings of entire sanctification that sound very Wesleyan.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 5. "WELS vs Assembly of God". WELS Topical Q&A. Wisconsin Evangelical Lutheran Synod. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-09-27. Iliwekwa mnamo 29 Jan 2015. {{cite web}}: More than one of |accessdate= na |access-date= specified (help); More than one of |archivedate= na |archive-date= specified (help); More than one of |archiveurl= na |archive-url= specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
 6. "Justification / Salvation". WELS Topical Q&A. Wisconsin Evangelical Lutheran Synod. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-09-27. Iliwekwa mnamo 29 Jan 2015. {{cite web}}: More than one of |accessdate= na |access-date= specified (help); More than one of |archivedate= na |archive-date= specified (help); More than one of |archiveurl= na |archive-url= specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)

Marejeo hariri

   . ISBN 9780192802903
   . http://www.oxfordreference.com/view/10.1093/acref/9780192802903.001.0001/acref-9780192802903-e-3298.

Marejeo mengine hariri

Ya Kikatoliki hariri

Ya Kimethodisti hariri

Ya Kilutheri hariri