Wilaya ya Muheza
Wilaya ya Muheza ni kati ya wilaya 11 za Mkoa wa Tanga katika Tanzania yenye Postikodi namba 21400.
Makao makuu yapo mjini Muheza.
Mwaka 2012 ilikuwa na wakazi 204,461 walioishi katika kata 33 za wilaya hiyo. Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 238,260 [1].
Wilaya ya Muheza ina ukubwa wa eneo linalokadiriwa kufikia zaidi kilomita za mraba 1470.
Ukiwa katika wilaya hiyo unapata kufika kwenye mitaa na maeneo kama Magila (zamani iliitwa Mbwego), Kisiwani, Majengo Ndani, Majengo Nje, Michungwani, Mdote, Genge, Masimbani, Mbaramo, Masugulu, Shimoni na maeneo ya vijiji kadhaa kama Mkuzi, Mng'aza, Gobo, Bwembwera (Mambo leo, Kilulu, Tongwe, Misozwe, Manyoni, Kicheba, Ubembe, Magoroto (kwenye hifadhi za misitu asilia ya kupendeza), Amani (kwenye hifadhi za misitu asilia ya kupendeza), Moa, Mtimbwane, Mtindiro Mwakijembe, Ngomeni, Nkumba, Pande, Potwe, Songa, Tingeni, Zirai, Mkumbi, enzi, nk
Historia
haririWilaya ilianzishwa mnamo mwaka 1994 na, kama ilivyo kwa wilaya nyingine za mkoa wa Tanga, ina historia kubwa sana na ya pekee.
Wakazi wanaopatikana kwenye wilaya hiYO ni Wabondei (Wa-Mabondeni). Kama inavyoelezwa na baadhi ya wanahistoria, k.mf. wakina Nkondokaya, wakazi wa mwanzo, kabla ya ujio wa Wabondei, walikuwa Wadorobo waliokuwa wakiishi kwa kuwinda na kuokotaokota. Lakini miaka ya 1700, wakati Wazigua wanafika maeneo ya Ukilindi (kilimani), waliweza kugawanyika na kusambaa kwenye maeneo ya Muheza ambako ndiko leo wako Wabondei. Na hivyo mji wa Muheza kuwa makazi ya asilia kwa Wabondei.
Kwa upande wa wageni, wa kwanza kufika maeneo ya Muheza walikuwa Waarabu ambao walikuja kufanya biashara na wakazi wa maeneo hayo kuanzia miaka ya 1800. Licha ya kwamba Waarabu walifika Afrika Mashariki tangu miaka ya 700 BK, mahusianao yao ya kibiashara yalikuja kukua miaka ya 1800, hasa kile kipindi ambacho utawala wa Oman ulihamia kisiwani Zanzibar. Hivyo mji wa Muheza ukawa moja ya miji iliyopata kukua tangu miaka hiyo.
Wageni wa pili kufika kwenye maeneo ya Muheza, ni watu kutoka Ulaya. Kwanza kulikuwa na Wareno ambao walipata kufika maeneo hayo kwenye miaka ya 1490. Hao walitawala maeneo ya Afrika Mashariki, hadi kuondoshwa mnamo miaka ya 1690. Wageni wengine kutoka Ulaya walikuja kuanzia miaka ya 1840/1850, ambao ni wamisionari kama Ludwig Krapf na Johannes Rebmann. Kufikia miaka ya 1890, kipindi ambacho ukoloni unaanza barani Afrika, Tanganyika ilikabidhiwa kwa Wajerumani na baadhi ya ardhi kupewa Sultani wa Zanzibar. Muheza palikuwa moja ya maeneo ambayo wakoloni waliweza kuanzisha mashamba na shughuli za kidini.
Kipindi cha kudai uhuru maeneo ya Muheza na Tanga kwa ujumla ni kati ya maeneo ambayo wanaTANU walikumbana na changamoto nyingi sana. Changamoto zilitoka kwa watawala wa kikoloni, wakati huo Waingereza, na hata baadhi ya viongozi wa makabila yaliyokuwa yakipatikana Muheza na Tanga kwa wakati huo. Mara baada ya uhuru Muheza ilikuwa miongoni mwa majimbo, na kufikia mwaka 1994 jimbo la Muheza lilikuja kuwa Wilaya.
Asili ya jina
haririAsili ya jina muheza linahusiana sana na Wabondei. Inasimuliwa na baadhi ya wazee na wanahistoria kuwa, asili ya jina Muheza ni neno “Mheza”. Na masimulizi yanadai kuwa kulikuwa na vita kati ya Wabondei na Wadigo. Vita hivyo vilitokana na wale Wazigua waliokimbilia na kufika maeneo ya pwani ya Tanga wakitokea maeneo ya Ukilindi na ndio hao Wabondei. Ambapo mapambano yao yalianza pwani ya Tanga na kufika maeneo ya Muheza ya leo. Wabondei wakiwa pwani ya Tanga walionekna kuzidiwa na hivyo waliamua kukimbilia maeneo hayo ya Muheza na walipofika hapo walisema “Hanu Mheza” ikiwa na maana kuwa hapa mmekwisha.
Na ndipo Wadigo walipopigwa na Wabondei na kukimbilia maeneo ya Tanga mjini na maeneo yale kukaliwa na Wabondei. Wabondei wao walipaita Mheza lakini baadaye matamshi ya waswahili na wageni wengine waliweza kuweka matamshi mapya na kupata jina Muheza.[2]
Marejeo
hariri- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ Na Mwalimu Joseph Mayuni kama jinsi alivyofanya uchambuzi kuhusu "Muheza" kwa kutumia vitabu vya Nkondokaya. G (2003) Historia ya Waseuta na Abdallah. H. B. (2003) Dola Kongwe Ya Zanzibar.
Viungo vya Nje
haririKata za Wilaya ya Muheza - Mkoa wa Tanga - Tanzania |
||
---|---|---|
Amani | Bwembwera | Genge | Kicheba | Kigombe | Kilulu | Kisiwani | Kwabada | Kwafungo | Kwakifua | Kwemingoji | Kwemkabala | Kwezitu | Lusanga | Magila | Magoroto | Majengo | Makole | Masuguru | Mbaramo | Mbomole | Mhamba | Misalai | Misozwe | Mkuzi | Mlingano | Mpapayu | Mtindiro | Ngomeni | Nkumba | Pande Darajani | Potwe | Songa | Tanganyika | Tingeni | Tongwe | Zirai |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Wilaya ya Muheza kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |