Wingu la Oort
Wingu la Oort (ing. Oort cloud) ni ukanda wa kudhaniwa angani unaozunguka mfumo wa Jua kwa umbali mkubwa nje ya mzingo wa sayari Uranus pia nje ya ukanda wa Kuiper. Ukanda huu unadhaniwa kuwa na magimba ya barafu na vumbi yaliyo na mwendo wa kuzunguka Jua kwa umbali kuanzia vizio astronomia 50,000 hadi 100,000 au zaidi (sawa na miakanuru 0.8 hadi 1.5). Kuwepo kwa wingu hili hakuthibitishwa kwa hiyo ni bado wingu la kinadharia. Nadharia hii ilitungwa na mwanaastronomia Mholanzi Jan Oort (1900 – 1992) aliyetafuta maelezo kwa asili na njia za nyotamkia zinazotokea katika mfumo wa Jua. Wingu la Oort linatazamiwa kuwa asili ya nyotamkia zenye obiti ndefu, ilhali zile zenye obiti fupi zinatoka katika Ukanda wa Kuiper.[1]
Kwa hiyo wingu la Oort liko kwenye mpaka wa nje wa mfumo wa Jua letu; linapoishia uko pia mwisho wa athari ya graviti ya Jua letu katika anga baina ya nyota.[2]
Nadharia ya Oort
haririJan Oort aliunda nadharia kuhusu wingu hili alipotafuta maelezo ya kuwepo kwa nyotamkia zenye obiti ndefu yaani zinazorudi baada ya miaka mingi. Kabla yake walikuwepo wengine waliowaza ya kwamba asili ya nyotamkia iko kwenye mipaka ya nje ya mfumo wa Jua. Oort aliwaza ya kwamba kuna magimba madogo mengi yanayozunguka Jua kwa umbali mkubwa. Kimsingi yapo katika obiti thabiti. Lakini mara kwa mara graviti ama ya nyota jirani -maana wingu linaenea hadi robo au nusu ya umbali kati ya Jua na nyota jirani ya Rijili Kantori (A Centauri)- na pia athari ya graviti ya sayari kubwa ndani ya mfumo wa Jua inaweza kuleta vurugu kwa obiti za magimba kadhaa na hivyo yanaanza kuvutwa na Jua na kuingia katika obiti itakayopita katika sehemu za ndani za mfumo wa Jua. Kama zinakaribia Jua zinapashwa moto, barafu ya miili yao inaanza kuyeyuka na "mkia" wa gesi inayoakisia nuru unaonekana.[3]
Asili na muundo
haririWingu la Oort inatazamiwa kuwa mabaki ya nje ya wingu lililozunguka Jua letu mwanzoni na kuwa pia asili ya sayari. Ila tu elementi nzito zilikusanyika katika sehemu zilizopo karibu zaidi na Jua na elementi nyepesi zilibaki kwenye sehemu za nje.
Magimba ya wingu la Oort yanafanywa na vipande vya barafu, vumbi au mwamba vilivyobaki wakati wa kutokea kwa sayari. Vipande hivi vilisukumwa na graviti ya sayari kubwa kama Mshtarii (Jupiter) au Zohali (Saturn) kuelekea mbali zaidi na Jua lakini hazikuondoka katika upeo wa graviti ya Jua. Athari ya nyota jirani ilisababisha vipande hivi kutoka kwenye bapa la ekliptiki ambako sayari na magimba mengine ya mfumo wa Jua letu huzunguka.
Marejeo
hariri- ↑ V. V. Emelyanenko; D.J. Asher & M.E. Bailey (2007). "The fundamental role of the Oort cloud in determining the flux of comets through the planetary system". Monthly Notices of the Royal Astronomical Society. 381 (2): 779–789. doi:10.1111/j.1365-2966.2007.12269.x. Iliwekwa mnamo 2008-03-31.
{{cite journal}}
: CS1 maint: multiple names: authors list (link) - ↑ "Kuiper Belt & Oort Cloud". NASA Solar System Exploration web site. NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-06-05. Iliwekwa mnamo 2011-08-08.
{{cite web}}
: External link in
(help)|work=
- ↑ Jan Oort (1950). "The structure of the cloud of comets surrounding the Solar System and a hypothesis concerning its origin" (PDF). Bull. Astron. Inst. Neth. 11: 91–110.