Zubani Junubi (kwa Kilatini na Kiingereza Zubenelgenubi; pia α Alfa Librae, kifupi Alfa Lib, α Lib) ni kati ya nyota angavu katika kundinyota la Mizani (Libra).

Zubani Junubi
(Alfa Librae, Zubenelgenubi)
Kundinyota Mizani (Libra)
Mwangaza unaonekana α1 5.15 'α2': .2.74 –
Kundi la spektra α1 F3 V
Paralaksi (mas) α1: 43.52 ± 0.43 α2 : 43.03 ± 0.19
Umbali (miakanuru) α1: 74.9 α2 : 75.8
Mwangaza halisi α1: +3.35 α2 : +0.92
Masi M☉ α1: 2 α2: 1.5
Nusukipenyo R☉ α1 : 1.48 α2: 2.78
Mng’aro L☉ α1: 3.9 α2 : 36
Jotoridi usoni wa nyota (K) α1: 6770 α2 : 8730
Majina mbadala α1 Lib: 8 Librae, BD–15 3965, FK5 1387, HD 130819, HIP 72603, HR 5530, SAO 158836.

α2 Lib: 9 Librae, BD–15 3966, FK5 548, HD 130841, HIP 72622, HR 5531, SAO 158840

Zubani Junubi ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [1]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaotumia neno الجنوبي الزبان al-zuban al-janubi kwa maana ya « koleo la kusini » yaani koleo la nge. Maana yake nyota hii pamoja na nyingine za Mizani zilihesabiwa zamani kuwa sehemu ya Akarabu (Nge) na kutazamwa kama makoleo yake. Hivyo kundinyota lote la Mizani bado liliitwa “Χηλαι” (helai - makoleo) na Klaudio Ptolemaio katika Almagesti. Kwa nyota aliita “ile angavu kwenye ncha ya koleo la kusini”[2].

Kwa matumizi ya kimataifa UKIA ulikubali jina la Kiarabu na kuorodhesha nyota ya Lib α² kwa tahajia ya "Zubenelgenubi" [3]. Maana Zubani Junubi ni nyota maradufu na azimio la Ukia linahusu nyota kuu katika mfumo huu.

Alfa Librae ni jina la Bayer; Alfa ni herufi ya kwanza katika alfabeti ya Kigiriki lakini Zubani Junubi ni nyota angavu ya pili na hii ni mfano ya kwamba Bayer hakufuata mwangaza kamili wakati wa kuorodhesha nyota.

α alfa Librae iko kwa umbali wa miakanuru 77 kutoka Jua letu. Ni nyota maradufu inayoonekana kwa darubini kuwa na nyota mbili ndani yake zinazoitwa α1 Librae na α2 Librae. α2 ni nyota angavu zaidi na umbali kati ya sehemu hizi mbili ni vizio astronomia 5.400. Vipimo vya spektra vinaonyesha ya kwamba kila moja ni nyota maradufu tena kwa hiyo Zubani Junubi ni mfumo wa angalau nyota nne zinazozungukana kwa namna ya jozi mbili za nyota.

Tanbihi

hariri
  1. ling. Knappert 1993
  2. Kigiriki: τῶν ἐπ´ ἂκρας τῆς νοτίου χηλῆς ὁ λαμπρός toon ep akras tes notiou heles ho lampros, Heiberg (1903) uk. 106
  3. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA), iliangaliwa Novemba 2017

Marejeo

hariri
  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 437 (online kwenye archive.org)
  • Caballero, J. A. (May 2010), "Reaching the boundary between stellar kinematic groups and very wide binaries. II. α Librae + KU Librae: a common proper motion system in Castor separated by 1.0 pc", Astronomy and Astrophysics, 514: A98 online hapa
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • J.L. Heiberg: Claudii Ptolemaei opera quae extant omnia Vol. I, Syntaxis Mathematica, Pars II libros VII-XIII continens; Leipzig, Teubner 1903 (Maandiko yote yaliyopo ya Klaudio Ptolemaio)

Viungo vya Nje

hariri
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Zubani Junubi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.