Afyuni (kwa Kiarabu أفيون) ni dawa asilia inayopatikana kutokana na utomvu uliokauka wa maua ya mpopi (jina la kisayansi: Papaver somniferum - kwa Kiingereza: Opium poppy). Ndani yake mna kemikali mbalimbali ambazo ni kati ya dawa kali kabisa zenye uwezo wa kutuliza maumivu lakini zinasababisha pia ulevi unaozoesha watu haraka na kuwafanya wasiweze kuacha ulevi huo.

Shamba la mpopi chanzo cha afyuni.
Afyuni bichi kutoka nchini Afghanistan

Uwezo na hatari za afyuni

hariri

Afyuni hutuliza maumivu, kuondoa mikakamao, inapunguza hisi ya njaa na husimamisha kuhara. Inasababisha pia ndoto zinazopendwa na watu na kutokana na uwezo huo afyuni ina hatari ya kuzoesha watu kuitumia.

Ikitumiwa mno inaweza kuua watu wanaoacha kula au kwa kusimamisha kazi ya mapavu. Hatari zake ni hasa upande wa roho kwa sababu watu wanaotegemea matumizi yake hawawezi kuiacha tena. Inapunguza uwezo wa akili na kunia kitu na kufuatilia mipango.

Siku hizi afyuni hutumiwa hasa kwa kutoa kemikali ndani yake na kutengeneza dawa kama morfini na heroini yanayotumiwa kama tiba lakini zaidi kama madawa ya kulevya ambayo ni hatari na haramu kote duniani yakitumiwa nje ya tiba.

Mavuno ya afyuni

hariri
 
Tumba la mpopi limekatwa na utomvu mweupe unatoka nje; baada ya masaa utaganda kuwa kama mpira kahawia-nyeusi.

Utomvu wa mpopi ni majimaji meupe yanayoganda haraka hewani kuwa dutu yenye rangi ya kahawia-nyeusi inayofanana na mpira. Katika hali hii huitwa afyuni bichi na ilitumiwa tangu kale kama dawa ya kutuliza maumivu likawezesha waganga wa Wahindi, Wachina na Waroma wa Kale kutekeleza upasuaji wa watu. Pamoja na matumizi hayo ilijulikana pia kama dawa la kulevya lakini hii ilikuwa matumizi ya pembeni tu hadi karne ya 15 BK.

Tangu karne ya 15 nchini China watu walianza kutumia afyuni bichi kama dawa la burudani wakilenga ulevi wake. Lakini matumizi hayo yalipatikana mara chache tu kutokana na uhaba na gharama za afyuni huko.

Historia ya usambazaji wake kama dawa la kulevya

hariri

Waingereza ndio walioanza kulima mpopi na kutengeneza afyuni kwa wingi katika makoloni yao huko Uhindi walipoona soko lake huko China. Wakasambaza afyuni kwa bei ndogo katika nchi nyingi za Asia hasa China. Upatikanaji huu wa afyuni ulisababisha matumizi yake na watu wengi waliozoeshwa nayo na kuitegemea.

Serikali ya China iliona hasara ya biashara hiyo kwanza kwa sababu ya hatari kwa afya ya wananchi, pili kwa sababu ya hasara kwa uchumi kutokana na watu kupoteza muda kwa ulevi na pia gharama za kununua afyuni kutoka nje. Serikali ilipokataa kuingizwa kwa afyuni, Uingereza ilishambulia China katika vita ya afyuni (1840 na tena 1858) ikailazimisha kukubali biashara hii.

Mwaka 1912 robo ya wanaume wote nchini China walitegemea matumizi ya afyuni ya mara kwa mara. Tatizo hili liliendelea hadi kukomeshwa kwa biashara yake chini ya utawala wa Wakomunisti wa Mao Dzedong.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia matumizi ya afyuni yalipungua lakini matumizi ya madawa yanayotolewa ndani yake kama heroini yamezidi duniani.

Mengineyo

hariri

Nchini Uturuki kuna mji wa Afyonkarahisar lililopata jina lake kutokana na kilimo cha mipopi na utengenezaji wa afyuni.