Akili bandia (kwa Kiingereza: Artificial Intelligence) ni nadharia na uundaji wa mifumo ya kompyuta yenye uwezo wa kutekeleza kazi ambazo kikawaida zinahitaji akili ya kibinadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha.

Kismet, kichwa cha roboti chenye uwezo wa kutambua na kuiga hisia za kibinadamu.

Teknolojia ya akili bandia inatumika kwa kiwango kikubwa viwandani, serikalini, na kwenye tafiti za kisayansi. Baadhi ya matumizi yenye wasifu mkubwa ya akili bandia ni pamoja na Injini za utafutaji wa tovuti (kama injini ya utafutaji ya Google), mifumo ya mapendekezo (inayotumika kwenye programu tumishi za YouTube, Tiktok, Amazon, na Netflix), kwenye utambuzi wa hotuba za binadamu (kama Google Assistant, Siri na Alexa), kwenye magari yanayojiendesha (kama Waymo), kwenye mifumo mikubwa ya lugha (inayotumika kwenye roboti za mazungumzo kama ChatGPT na Bard), kwenye mifumo ya uzalishaji picha kama DALL-E na michezo ya kimkakati (kama chess na Go) [1].

Akili bandia kama taaluma ya sayansi ilianza rasmi mwaka 1956, neno "Akili bandia" lilitungwa na John McCarthy, mwanasayansi wa kompyuta wa kimarekani katika mkutano wa kwanza wa Akili bandia uliofanyika kwenye chuo cha Dartmouth [2].

Tafiti mbalimbali za akili bandia zina malengo tofauti na hutumia njia tofauti kufikia malengo hayo. Malengo yaliyozoeleka ya tafiti ya akili bandia ni pamoja na ufikiriaji, uwasilishaji wa maarifa, upangaji, kujifunza, usindikaji wa lugha asili, utambuzi, na usaidizi wa roboti. Akili ya jumla (uwezo wa kukamilisha kazi yoyote inayowezwa fanywa na binadamu) ni moja kati ya malengo ya mda mrefu ya taaluma hii.

Ili kufikia malengo hayo, watafiti wa akili bandia wametumia na kuunganisha njia mbalimbali za kutatua matatizo, ikiwemo utafutaji na uboreshaji wa kihisabati, mantiki rasmi, mitandao ya neva bandia, na njia nyingine zinazotegemea takwimu, utafiti shughuli na uchumi. Akili ya bandia pia inategemea elimunafsia, isimu, falsafa, sayansi neva na nyanja nyingine.

Marejeo hariri

  1. AlphaGo (en). Google DeepMind (2020-12-23). Iliwekwa mnamo 2024-01-02.
  2. Artificial Intelligence (AI) Coined at Dartmouth | Dartmouth (en). home.dartmouth.edu. Iliwekwa mnamo 2024-01-02.

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya teknolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hiyo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.