Anania wa Damasko (jina kwa Kigiriki ni Ἀνανίας, kutokana na Kiebrania חנניה, Hananiah, yaani, "Aliyefadhiliwa na Bwana"[1]) alikuwa Myahudi wa karne ya 1 anayejulikana katika kitabu cha Matendo ya Mitume (9:10-19 na 22:12-16).

Anania akiponya macho ya Mt. Paulo, mchoro wa Pietro da Cortona, 1631.

Humo tunasikia kwamba alikuwa mwanafunzi wa Yesu na kwamba, akiwa Damasko (Siria), alikuwa na sifa ya "mtu wa ibada kadiri ya sheria, aliyeheshimiwa na Wayahudi wote" (Mdo 22:12)[2].

Miaka 6 hivi baada ya kufufuka, alitokewa naye na kuagizwa kwenda kwa Saulo wa Tarso, nyumbani mwa Yuda kwenye Njia Nyofu, ili kumponya upofu na kumuelimisha katika dini mpya iliyoitwa baadaye Ukristo.

Alipopata agizo hilo, Anania alisita kwa kuwa alimuogopa Saulo kutokana na juhudi zake dhidi ya Wakristo, lakini Yesu alisisitiza aende, akieleza kwamba mtu huyo ni "chombo kiteule kwake, ili kufikisha jina lake kwa mataifa, kwa wafalme na kwa wana wa Israeli". (Mdo 9:15).

Anania alipotii, alimwekea Saulo mikono kichwani na kufanya magamba ya machoni mwake yadondoke. Kisha kumuelimisha kidogo, alimbatiza nyumbani humo (Mdo 9:18; 22:16).

Baada ya tukio hilo, hakuna habari za hakika juu ya Anania. Kadiri ya mapokeo, Anania alifia dini huko Eleutheropolis.[3]

Anaheshimiwa kama mtakatifu tarehe ya sikukuu ya Wongofu wa Mtume Paulo, 25 Januari[4].

Habari zake katika Mdo 9

hariri
 
"Barabara iliyonyoka", Mtume Paulo alipobatizwa na Anania wa Damasko, ilivyo leo.

1 Wakati huo Saulo alikuwa akizidisha vitisho vikali vya kuwaua wafuasi wa Bwana. Alikwenda kwa Kuhani Mkuu,

2 akaomba apatiwe barua za utambulisho kwa masunagogi ya Kiyahudi kule Damasko, ili akikuta huko wanaume au wanawake wanaofuata Njia ya Bwana, awakamate na kuwaleta Yerusalemu.

3 Lakini alipokuwa njiani karibu kufika Damasko, ghafla mwanga kutoka angani ulimwangazia pande zote.

4 Akaanguka chini na kusikia sauti ikimwambia: "Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?"

5 Naye Saulo akauliza, "Ni nani wewe Bwana?" Na ile sauti ikajibu, "Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.

6 Lakini simama sasa, uingie mjini na huko utaambiwa unachopaswa kufanya."

7 Wale watu waliokuwa wanasafiri pamoja na Saulo walisimama pale, wakiwa hawana la kusema; walisikia ile sauti lakini hawakumwona mtu.

8 Saulo aliinuka, na alipofumbua macho yake hakuweza kuona chochote; hivyo wale watu wakamwongoza kwa kumshika mkono mpaka mjini Damasko.

9 Saulo alikaa siku tatu bila kuona, na wakati huo hakula au kunywa chochote.

10 Basi, huko Damasko kulikuwa na mfuasi mmoja aitwaye Anania. Bwana akamwambia katika maono, "Anania!" Anania akaitika, "Niko hapa, Bwana."

11 Naye Bwana akamwambia, "Jitayarishe uende kwenye barabara inayoitwa Barabara ya Moja kwa Moja, na katika nyumba ya Yuda umtake mtu mmoja kutoka Tarso aitwaye Saulo. Sasa anasali;

12 na katika maono ameona mtu aitwaye Anania akiingia ndani na kumwekea mikono ili apate kuona tena."

13 Lakini Anania akajibu, "Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kutoka kwa watu wengi; nimesikia juu ya mabaya aliyowatendea watu wako huko Yerusalemu.

14 Na amekuja hapa akiwa na mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu kuwatia nguvuni wote wanaoomba kwa jina lako."

15 Lakini Bwana akamwambia, "Nenda tu, kwa maana nimemchagua awe chombo changu, alitangaze jina langu kwa mataifa na wafalme wao na kwa watu wa Israeli.

16 Mimi mwenyewe nitamwonyesha mengi yatakayomlazimu kuteswa kwa ajili ya jina langu."

17 Basi, Anania akaenda, akaingia katika hiyo nyumba. Kisha akaweka mikono yake juu ya Saulo, akasema, "Ndugu Saulo, Bwana ambaye ndiye Yesu mwenyewe aliyekutokea ulipokuwa njiani kuja hapa, amenituma ili upate kuona tena na kujazwa Roho Mtakatifu."

18 Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka macho ya Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa.

19 Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko.

20 Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

21 Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, "Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!"

22 Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa.

Habari zake katika Mdo 22

hariri

Miaka 22 baadaye, huko Yerusalemu, Paulo alijitetea hivi:

1 "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!"

2 Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema,

3 "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti Sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama ninyi wenyewe mlivyo hivi leo.

4 Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata Njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani.

5 Kuhani Mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.

6 "Basi, nilipokuwa njiani karibu kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwangu mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote.

7 Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: `Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?`

8 Nami nikauliza: `Nani wewe, Bwana?` Naye akaniambia: `Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.`

9 Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami.

10 Basi, mimi nikauliza: `Nifanye nini Bwana?` Naye Bwana akaniambia: `Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.`

11 Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.

12 "Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii Sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko.

13 Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema: `Ndugu Saulo! Ona tena.` Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia.

14 Halafu Anania akasema: `Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea.

15 Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia.

16 Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama ubatizwe na uondolewe dhambi zako kwa kuliungama jina lake.`

17 "Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali Hekaluni, niliona maono.

18 Nilimwona Bwana akiniambia: `Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa binadamu hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.`

19 Nami nikamjibu: `Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini.

20 Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.`

21 Naye Bwana akaniambia: `Nenda; ninakutuma mbali kwa mataifa mengine."`

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri
  1. Greek lexicon G367, Hebrew lexicon H2608
  2. F. F. Bruce, Commentary on the Book of the Acts (Grand Rapids: Eerdmans, 1964), 199.
    also found on page 189 of the 1988 edition, ISBN 0-8028-2505-2.
  3. St. Ananias II
  4. Martyrologium Romanum, 2004, Vatican Press (Typis Vaticanis), page 116.
  Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Anania wa Damasko kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.