Ashura ni sikukuu ya kiislamu inayosheherekewa na Washia hasa wakiadhimisha kifo cha Hussein mjukuu wa Mtume Muhammad kwenye siku ya kumi ya mwezi wa Muharram katika kalenda ya Kiislamu.

Sherehe ya Ashura huko Iran: wanaume wamekusanyika wakisikia habari za kifo cha Imamu Husayn, kuimba sala pamoja na kupiga kifua kwa makofi kama ishara ya huzuni

Asili ya jina ni neno la Kiarabu "ashara" (عَشَرَة) yaani kumi, maana tarehe yake ni siku ya kumi kwenye mwezi wa kwanza katika kalenda ya kiislamu na mwezi huu huitwa Muharram. Kutokana na tabia ya kalenda ya kiislamu kufuata uonekanaji wa mwezi angani Muharram na siku ya Ashura hubadilika kila mwaka kulingana na kalenda ya Gregori ambayo ni kawaida.

Washia hukumbuka hapo kifo cha Hussein ibn Ali, mjukuu wa mtume Muhamad, aliyekuwa kwao imamu na mfuasi halali wa mtume katika uongozi wa umma wa Waislamu. Hussein alikufa kwenye Mapigano ya Karbala siku ya 10 Muharram, mwaka 61 BH (=10 Oktoba 680 BK).[1]

Wasunni kwa kawaida hawashiki kumbukumbu ya kifo cha Husseintahajia ibn Ali bali hukumbuka hadithi moja inayosema Mtume Muhamad alifunga chakula siku ya Ashura, hivyo kuna Wasunni wanaofunga pia siku hiyo.[2][3]

Katika nchi zenye Washia wengi, kama vile Iran, Iraq, Lebanoni na katika sehemu za Afghanistan na Uhindi, hii ni sikukuu muhimu ya kitaifa.

Marejeo

hariri