Kamerun ya Kiingereza
Kamerun ya Kiingereza (British Cameroons) ilikuwa sehemu ya magharibi ya koloni ya awali ya Ujerumani iliendelea kama eneo la kudhaminiwa chini ya Uingereza kuanzia mwaka 1922 hadi 1961.
Wakati wa mwisho wa ukoloni wananchi wa sehemu ya kaskazini walipiga kura ya kuunganika na Nigeria, ilhali watu wa sehemu ya kusini waliamua kujiunga na Kamerun.
Kamerun ya Kiingereza ilikuwa sehemu ya koloni la Kamerun ya Kijerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Mwaka 1914 koloni hili lilivamiwa na Uingereza kutoka Nigeria, Ufaransa kutoka maeneo yao ya Afrika ya Kifaransa na Ubelgiji kutoka Kongo. Mwaka 1916 jeshi la Kijerumani ilisalimu amri na koloni liligawiwa baina ya Uingereza na Ufaransa.
Mwaka 1922 Shirikisho la Mataifa lilikubali rasmi ugawaji huu na kukabidhi Kamerun kwa Ufaransa na Uingereza kama maeneo ya kudhaminiwa. Sehemu ya Uingereza ilikuwa takriban asilimia 20 za Kamerun ya Kijerumani ya awali. Waingereza waligawa sehemu yao katika mikoa miwili: ya kaskazini na kusini na kuitawala kama sehemu ya Nigeria.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia usimamizi wa maeneo ya kukabidhiwa ulihamia mikononi mwa Umoja wa Mataifa ulioamua ya kwamba maeneo hayo yapewe uhuru kuanzia mwaka 1960. Ilhali Kamerun ya Kiingereza ilitazamiwa kuwa ndogo mno kwa kuanzisha nchi ya pekee, pia haikuwa na eneo mfululizo, wananchi walipewa chaguo cha kujiunga na nchi jirani.
Wakazi wa mkoa wa kaskazini walipoishi Waislamu wengi walipiga kura kuwa sehemu ya Nigeria (kwa 60%) lakini wananchi wa mkoa wa kusini waliamua kujiunga na Kamerun ya Kifaransa katika Shirikisho la Jamhuri ya Kamerun [1].
Tangu 1972 muundo wa nchi ulibadilishwa kuacha mfumo wa shirikisho na kuwa jamhuri ya muungano inayokazia zaidi matumizi ya lugha ya Kifaransa ingawa Kiingereza bado ni moja ya lugha rasmi. Hapo sehemu ya Wakamerun wanaotumia lugha ya Kiingereza walijisikia kuwa wananyimwa haki zao.[2]
Tangu mwaka 2016 upinzani wa watu wa magharibi ulijibiwa kwa ukali zaidi na hii imeleta upinzani wa wanamgambo wenye silaha wanaoshambulia polisi na jeshi la serikali kuu. Tangu mwaka 2017 wapinzani wamedai uhuru wa sehemu yenye lugha ya Kiingereza wakidai kuundwa kwa nchi ya Ambazonia.
Marejeo
hariri- ↑ 1961 British Cameroons Plebiscite, kwenye tovuti ya africanelections.tripod.com/referenda, iliangaliwa Januari 2019
- ↑ Anglophone crisis: Cameroon must return to federal system abolished under Ahidjo, Abdur Rahman Alfa Shaban kwenye tovuti ya africanews.com tar. 11/03/2018
Viungo vya Nje
hariri- British Cameroon Archived 9 Julai 2017 at the Wayback Machine., sehemu ya histori kwenye tovuti ya cameroonweb.com
- Harry R. Rudin, Germans in the Cameroons 1884-I914, A Case Study in modern imperialism, Yale University Press 1938 (online hapa kwa archive.org)
Tazama pia
haririMakala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kamerun ya Kiingereza kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |