Devil Kingdom ni filamu yenye hadithi ya kufikirika ya mwaka 2011 kutoka Tanzania iliyoongozwa na kutayarishwa na Steven Kanumba. Nyota wa filamu ni Steven Kanumba, Ramsey Nouah, Kajala Masanja, Fatuma Makongoro, Patcho Mwamba na wengine. Muswada andishi umeandikwa na Ally Yakuti kutoka kwenye hadithi iliyoandikwa na Steven Kanumba.

Devil Kingdom

Posta ya Devil Kingdom
Imeongozwa na Steven Kanumba
Imetayarishwa na Steven Kanumba
Imetungwa na Ally Yakuti
Nyota Steven Kanumba
Ramsey Nouah
Kajala Masanja
Fatuma Makongoro
Patcho Mwamba
Imehaririwa na Zakayo Magulu
Imetolewa tar. 26 Aprili, 2011
Ina muda wa dk. 120
Nchi Tanzania
Lugha Kiswahili
Kiingereza

Filamu iliingia mitaani rasmi tarehe 26 Aprili 2011.[1]

Filamu inamhusu Ambrose Mapalala, kijana fukara mwenye shauku ya kuishi kwa fahari; baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, anajikuta akijiunga na jamii ya siri ya kishetani inayompa nafasi ya kutimiza ndoto zake kwa malipo ya kafara za watu. [2]

Hadithi hariri

Hadithi inaanza na Ambrose Mapalala, anayetamani sana kuishi maisha ya kitajiri kwa lengo la kumridhisha mpenzi wake mwenye tamaa, Tracy. Tracy anafanikiwa kumshawishi Ambrose kuiba kiasi kikubwa cha pesa kwenye kampuni anayofanyia kazi. Wizi huo unapogundulika, Ambrose anafilisiwa mali zake zote na kufukuzwa kazi huku Tracy akimuacha baada ya kupata mpenzi mwingine tajiri.

Kupambana na ugumu wa maisha, Ambrose anaamua kufungua kanisa dogo linaloshindwa kujiendesha kutokana na idadi ndogo ya sadaka. Pita pita za barabarani zinamkutanisha na rafiki yake wa utotoni Tony.Tony anamuunganisha kwa kiongozi wake anayejulikana Kwa jina la Jerome au "The masterpiece " baada ya Ambrose kutaka kujua ni kwa njia gani naye anaweza kupata mafanikio ya mda mfupi kama aliyomkuta nayo Tony.

Mafundisho mageni ya Jerome yaliyojikita kwenye kukosoa usahihi wa Biblia, ukomo wa nguvu za Mungu na kuonyesha utukufu wa Ibilisi, unamfanya Ambrose apoteze imani yake na kujiunga na jamii yao ya siri inayoabudu na kuchukua maagizo kutoka kwa shetani mwenyewe.

Katika ibada ya utambulisho, Ambrose anapokea nguvu za kishetani zinazo mpa uwezo wa kutenda miujiza na kuponya watu hali inayofanya jina na kanisa lake kuwa kubwa,ndani ya mda mfupi, anafanikiwa kuishi maisha ya ndoto yake na kurudiana na Tracy.

Ili kutunza nguvu hizi, Ambrose anaingia maagano ya kutoa kafara ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wanaolelewa na NGO's zinazo fadhiliwa na kanisa lake. Baada ya serikali kutilia mashaka vifo hivyo vya kila mwaka, Ambrose anapewa amri ya kutoa kafara ya mama na dada yake kama mbadala. Ambrose anapinga amri hii bila mafanikio yoyote mbele ya Jerome anayeonekana kuwa Shetani mwenyewe kwenye mwili wa binadamu.

Baada afya ya Mama na dada yake kuwa mbaya hospitali, Ambrose anatafuta msaada wa maombi kutoka kwa Mchungaji (wa kweli) na kufanikiwa kuwaponya dada na Mama yake. Hadithi inaisha tukimuona Ambrose akilia mbele ya madhabahu kujutia alichofanya.

Washiriki hariri

  • Steven Kanumba kama Ambrose Mapalala, kijana fukara anayejikuta akiingia kwenye jamii ya siri ya kishetani kwa tamaa zake za kutaka kuishi maisha ya kifahari.
  • Ramsey Nouah kama Jerome au "The Masterpiece", huyu ni kiongozi wa ngazi ya juu kwenye chama, mwalimu wa Ambrose kuhusu mafundisho ya kishetani, na mwishoni anagundulika kuwa Shetani mwenyewe kwenye mwili wa binadamu.
  • Kajala Masanja kama Tracy, mpenzi wa Ambrose Mapalala, mwenye tamaa ya kuishi na wanaume wenye maisha ya kitajiri.
  • Fatuma Makongoro kama mama yake, Ambrose mapalala, aliyejaa hofu kubwa ya Mungu (Mcha Mungu)
  • Patcho Mwamba kama Tony, rafiki wa utotoni wa Ambrose, anayemkutanisha Ambrose na Jerome.
  • Bakari Makuka, kama rafiki mwingine wa Ambrose Mapalala, pamoja na Tony.

Falsafa ya Dini hariri

Filamu ya Devil Kingdom imejaribu kugusa dhana tata kwenye falsafa ya dini kupitia mfululizo wa mafundisho ya Jerome kwa Ambrose.

Katika sehemu ya pili ya hadithi, Jerome anamuuliza Ambrose, iwapo Mungu wake anaweza kuumba kiumbe chenye nguvu kuliko yeye: swali hilo kwenye falsafa ya dini linajulikana kama "Fumbo la jiwe". Jibu lolote la Ndiyo au Hapana linafanya Mungu wa Ambrose awe na ukomo kwenye nguvu zake, aidha kwa kushindwa kuumba kiumbe chenye nguvu kuliko yeye au kushindwa nguvu na kiumbe hiko.

Hadithi pia inagusia kisa cha Lilith, ambaye maandiko mengine ya Kiyahudi, ukiacha Torati, yanamtambua kama mke wa kwanza wa Adamu, aliyefukuzwa kwenye bustani kwa kudai haki sawa na mumewe.

Filamu pia inahoji usahihi wa Biblia, pale ambapo Jerome anajaribu kuthibitisha mbele ya Ambrose kuwa mpangilio wa matukio ya uumbaji hauendi sambamba na ukweli unaosemwa na sayansi.

Jerome anarejea Mwanzo 1:5, ambayo inataja kuwepo kwa usiku na mchana siku ya kwanza ya uumbaji, wakati Jua lenyewe kama chanzo kikuu cha usiku na mchana, likiumbwa siku ya nne kulingana na Mwanzo 1:14.

Utata hariri

Devil Kingdom ni moja kati ya kazi za mwisho za Steven Kanumba, iliyowachanganya watazamaji wengi haswa kutoka Tanzania, kiasi cha kuibua maswali mengi kuhusu imani yake ya dini.

Ndani ya hadithi tunaona wanachama wa jamii hii ya siri, wakivaa mavazi na kufanya ibada ambazo zinafananishwa, kwa mujibu wa watazamaji walio wengi kutoka Tanzania, na ibada au mavazi ya wanachama wa Wamasoni.

Tunamuona Ambrose Mapalala, akitoka kwenye shimo la ufukara mpaka kuwa mchungaji mwenye mafanikio na ushawishi mkubwa kwenye jamii. Wapo baadhi ya watu wanaoamini (kimakosa) kuwa mafanikio ya nyota wengi haswa wa muziki na filamu yanatokea mara ya baada ya nyota hao kujiunga na Wamasoni.

Steven Kanumba mwenyewe alikataa katakata alipoulizwa iwapo yeye ni mwanachama wa Wamasoni au ana mahusiano ya aina yoyote ile na chama hicho.

Utayarishaji hariri

Devil Kingdom ni filamu iliyochukua muda mwingi kuiandaa kuliko filamu nyingine zote za Steven Kanumba, huku watu zaidi ya 200 wakishiriki zoezi hilo. Pia ni filamu iliyogharimu bajeti kubwa kwani ilihitaji vifaa vya ziada vya kisasa, ikiwemo jenereta kubwa kutokana na changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme.

Marejeo hariri

  1. Devil Kingdom yaingia mtaani rasmi Ijumaa Aprili 26, 2011. Katika Kanumba the Great Blogu.
  2. Devil Kingdom Archived 22 Juni 2017 at the Wayback Machine. katika Bongo Cinema.com

Viungo vya nje hariri