Diwani
Diwani nchini Tanzania ni mwakilishi wa wananchi wa kata yake, pia ni mwakilishi wao katika vikao vya baraza la madiwani la halmashauri anayoitumikia (halmashauri ya wilaya/manispaa/jiji/mji) kama ilivyoridhiwa katika sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa ya mwaka 1977 sura No.292-14(1)[1].
Diwani pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (ward development committee, WDC) kama ilivyoandikwa katika sheria ya serikali za mitaa No.7(31) ya mwaka 1982, iliyofanyiwa marekebisho na sheria No.6 ya mwaka 1999.
Diwani pia ni mtunzi, mpitishaji, mwidhinishaji na msimamizi wa sheria ndogondogo zinazotungwa kwenye kata yake kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo kama ilivyoridhiwa katika sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1977 sura No.287-153(1) [mamlaka ya mji] na katika sura No.288-89 na 122(1) (d) [mamlaka ya wilaya].
Majukumu ya Diwani kwa ujumla
haririPamoja na hayo yaliyoainishwa hapo juu, kwa ujumla diwani anapaswa kuhakikisha anatekeleza yafuatayo [2].
1. Kuwakilisha wananchi katika Halmashauri. Diwani huwakilisha wakazi wote wa kata yake, hivyo anatakiwa kuwa karibu na wapiga kura wake na kufikisha mbele ya Halmashauri na kamati zake vipaumbele vya wananchi ili vijadiliwe na kutolewa maamuzi.
2. Kuhamasisha wananchi katika kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri. Kusimamia matumizi ya fedha za Halmashauri. Diwani anatakiwa kuhakikisha fedha za Halmashauri zinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
3. Kuwa kiungo kati ya Halmashauri na ngazi za msingi za Serikali za Mitaa. Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Atumie mamlaka hiyo kuwasilisha kwenye Halmashauri maamuzi ya kata yake na vilevile kuwasilisha kwenye kata maamuzi ya Halmashauri.
4. Kuhamasisha wananchi kuhusu vita dhidi ya umaskini. Katika kulitekeleza hili ni lazima ajue kwa ufasaha hali ya kiuchumi na ya kijamii inayowakabili wananchi wake na kushirikiana nao ili kupanga mipango endelevu ya kujikwamua.
5. Kufuatilia utekelezaji wa mipango yote ya wananchi na ya Halmashauri. Ili kutimiza jukumu hili ipasavyo, Diwani anatakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ndani ya kata yake ambalo ni jimbo lake la uchaguzi bila kudai malipo yoyote toka kwenye Halmashauri au wadau wengine. Kimsingi hii ndiyo kazi ambayo Diwani aliahidi kuitekeleza wakati wa kampeni.
6. Kutetea maamuzi ya Halmashauri. Wakati wa majadiliano ndani ya Halmashauri, Diwani ataelekeza na kutetea maoni yake au ya wakazi wa eneo lake. Hata hivyo, iwapo uamuzi utakaofikiwa na wengi utakuwa kinyume na matarajio yake, atalazimika kuunga mkono maamuzi ya wengi yaliyofikiwa kidemokrasia.
7. Kuzingatia misingi yote ya Utawala Bora wakati wa kutekeleza majukumu yote ya Udiwani.
Marejeo
haririMakala hii kuhusu mambo ya sheria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Diwani kama historia yake au uhusiano wake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |