Eric Shigongo

Muandishi, mwanasiasa na mbunge wa Tanzania

Eric James Shigongo (alizaliwa wilayani Buchosa, zamani Sengerema, mkoa wa Mwanza, 10 Agosti 1969) ni mbunge wa Buchosa katika Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania (kuanzia tarehe 25 Novemba 2020) na mjasiriamali ambaye amejikita zaidi katika uandishi wa hadithi na vitabu.

Mpaka sasa ana vitabu vingi kama Malkia wa Masokwe, Damu na Machozi, Raisi Anampenda Mke Wangu, Siri Iliyotesa Maisha Yangu, Sheria 10 za Mafanikio na mwisho Maisha ya Mike.

Shigongo ni mwanzilishi na mmiliki wa makampuni ya Global Group ambayo ni: Global Publishers & Ent. Ltd, Global Printways Ltd, Wezesha Mzawa Microfinance Ltd, Dar Live Company Ltd, Shigongo Oil Company Ltd na Blue Mark Real Estate Company Ltd (Kampuni zote hizi zipo Tanzania).

Shigongo ni mmiliki wa vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo televisheni maarufu ya mtandaoni, Global TV Online na Global Radio. Global Publishers ndiyo inayochapisha magazeti ya Uwazi, Amani, Risasi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Championi na Spoti Xtra.

Shigongo pia ni mhamasishaji na mwalimu wa masuala ya ujasiriamali, amesaidia vijana wengi kuwafundisha mbinu mbalimbali za kuyatafuta mafanikio kwa kufanya biashara na kujiingizia vipato halali.

Maisha

hariri

Eric Shigongo ni mtoto wa James Bukumbi na Asteria Kahabi Kapela ambao wote wameshafariki dunia. Mara zote Shigongo amekuwa akisema wazi kwamba wazazi wake walikuwa watu maskini, hakupata bahati ya kusoma sana shuleni (alikomea darasa la saba) lakini alijituma katika biashara zake hadi akafanikiwa.

Licha ya kufeli darasa la saba, Eric Shigongo amefanikiwa kuhitimu chuo kikuu akiibuka mwanafunzi bora aliyefaulu kwa kiwango cha juu zaidi.

Kabla ya kwenda chuo kikuu, alijifunza lugha ya Kiingereza mtaani, kama wengine wanavyojifunza lugha ya makabila. Shigongo aliibuka mwanafunzi bora Chuo Kikuu cha Tumaini alikohitimu shahada yake baada ya kupata GPA ya 4.8.

Shigongo alifeli mara mbili darasa la saba na akadhani hiyo itakuwa mwisho wa safari yake kielimu. Lakini, alipata bahati ya kwenda kusoma kozi ya mwaka mmoja ya unesi msaidizi wilayani Sikonge mkoani Tabora, lakini kutokana na mshahara kuwa mdogo anasema aliacha kazi na kukichana cheti alichokuwa nacho.

Shigongo alijifunza Kiingereza mtaani. “Kiukweli sikufundishwa, naongea Kiingereza kama lugha ya kikabila, ukiniambia adjective nini sijui, sijui adverb yale mambo mimi siyajui kabisa mimi naongea kama kabila.

Shigongo alikutana na kijana anaitwa Jesse alikuwa mtoto wa daktari anaitwa Camstra, ambaye ni surgeon (daktari wa upasuaji) aliyetokea Uholanzi. Jesse alikuwa hajui Kiswahili akawa rafiki yake, yeye akawa anamfundisha Jesse Kiswahili yeye anamfundisha Kiingereza, kwa hiyo akashika pale lugha.

Alifundishwa namna ya kuzungumza siyo kujua hii ni adverb au adjective. Baadaye alipojua Kiingereza akaanza kuwa anasikiliza redio na kusoma gazeti la Sunday News. Akawa anajifunza Kiingereza, akisoma Sunday News na ‘dictionary’ (kamusi) lazima iwe pembeni. Alikuwa napenda sana kusoma safu za Wilson Kaigarula. Alikuwa akisikiliza BBC English Service, nasikiliza KBC ya Kenya ya Kiingereza.

“Kama unaweza kujifunza Kisukuma bila kufundishwa darasani ni hivyohivyo, sasa nikaanza kusoma ‘noval’ (riwaya) za Sidney Sheldon, kitabu chake cha ‘The other side of midnight’. Sidney akanimeza, yaani ikawa mimi nasoma riwaya za Sidney mpaka nikawa naweza kukesha nasoma kitabu.

"Yaani sisi tulikuwa vijana wa mwanzo tukitembea na ‘noval’ mtaani. “Nikajenga utamaduni wa usomaji wa vitabu. Sidney ndiye aliyeniathiri mimi style (mtindo) yake ya kuandika, nikawa napenda anavyoandika ‘flashback style’ anaanzia mwisho wa story, halafu anakuja kukupitisha,” anasema Shigongo.

Shigongo alianza darasa la kwanza mwaka 1977 Shule ya Msingi Gembe iliyopo jimbo la Solwa mkoani Shinyanga.

Baadaye familia yao ilihamia mkoani Mwanza, eneo la Nyakato, ambako aliendelea darasa la pili mpaka alipohitimu elimu ya msingi.

“La saba nikafeli na wala sikushangaa kwa sababu nilikuwa sijawahi kufaulu mtihani wowote huko chini, mimi sikuwa mjinga ila mazingira niliyokulia nyumbani maskini, tumezungukwa na matajiri, kila ninakopita najiona kama fukara, hakuna mtu ananithamini, shuleni walimu wananigombeza, kwa hiyo nilikuwa nimejikatia tamaa.

“Hata wakati wa mtihani sifanyi juhudi yoyote ile, yaani kama niliwahi kupata maksi nzuri sana darasani ni asilimia 25, sijawahi kufaulu zaidi ya maksi hizo.

“Siku nilipopata asilimia 25 mwalimu alishangaa. Akaja kaka yangu mmoja akasema lazima usome, akanichukua na kunipeleka Buchosa kule tuliotoka kwenda kurudia shule.

Zamani ulikuwa unaweza kufeli halafu ukarudia. “Nikaenda kurudia shule moja inaitwa Luhama nikasoma pale la saba nikafeli tena. Nilipofeli nikasema shule itakuwa imeshindikana hapa, la muhimu ni kufanya biashara,” anasema Shigongo.

Baadaye alisikia taarifa kuhusu chuo cha uuguzi kilichopo Sikonge mkoani Tabora, akaamua kwenda kusoma kozi ya mwaka mmoja.

Alipomaliza kozi hiyo, Shigongo alirudi kijijini alikoanza kufanya kazi kwenye moja ya zahanati zilizopo lakini aliokuwa akilipwa akilinganisha na umasikini uliopo kwenye familia yake akaona hautoshi kukidhi mahitaji yake, hivyo akaacha kazi.

“Mimi mshahara ule bwana ulinishinda, nikasema familia yangu ni maskini, wanalala chini na wanalala njaa, wazazi wangu wanadharauliwa na kila mtu na pale tunapokaa matajiri ni wengi wanatupa takataka kwetu kwa sababu kulikuwa na nafasi wanapafanya dampo.

“Nikasema lazima nifanye kitu, kile cheti cha nesi nilikichana nikaamua kwenda machimboni,” anasema Shigongo.

Kuhusu alivyoingia chuo kikuu ilhali yeye ni mhitimu wa darasa la saba, tena aliyefeli, Shigongo anasema hiyo ilitokana na kipaji chake cha kuandika.

“Mwaka 2017 nikasikia hiyo habari ya Recognition of Prior Learning (RPL) kutoka kwa Godwin Gondwe (aliyekuwa mtangazaji wa Radio One na ITV kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni). Na mimi kwa wakati huo nilikuwa nimeshaandika kwa miaka mingi sana.

“Nimeandika kwa zawadi ya Mungu bila kufundishwa na mtu yeyote wala mahali popote. Sasa nilikuwa nimeandika vitabu vingi sana, na kumiliki kampuni ya habari. Lakini, wakati wote huo sikuwahi kusoma ‘mass communication’ mahali popote na elimu yangu ikiwa bado ni ya darasa la saba.

“Sijawahi kusoma sekondari mahali popote duniani, mtu ambaye haamini anaweza kwenda kule baraza la mitihani kama kuna mtu anaitwa Shigongo amewahi kusoma sekondari mahali popote. Nilipopata taarifa zile mimi nikachukua vitabu vyangu nikaenda pale TCU (Tanzania Commission for Universities) nikamkuta Profesa Mwesiga Baregu na nikaweka vitabu vyangu mezani nikamwambia vitabu vyote hivi nimeviandika mimi bila elimu rasmi, ni vitabu vyenye kurasa 500.

“Akashangaa na akaniambia hapa kwetu kuna mfumo unaitwa RPL unaweza ukafanya mtihani wewe, ukipasi unaingia kusoma shahada chuo kikuu. Nikaufanya ule mtihani mwaka wa kwanza nikafeli, ilikuwa 2016, mwaka 2017 nilipofanya ule mtihani nikafaulu. Nilipofaulu nikajiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam Turdaco (Tumaini University Dar es Salaam College).

“Nikaanza kusoma shahada ya kwanza ya mawasiliano ya umma, kutoka darasa la saba kwenda chuo kikuu. Nimesoma kwa miaka mitatu. Nimemaliza pale nikiwa ‘one of the best students’ mwenye GPA ya 4.8 yaani nilipata B tatu katika muda wote niliosoma shuleni,” anasema Shigongo.

Shigongo baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza alitamani kusoma shahada ya uzamivu, lakini alipopeleka maombi yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walimtaka apeleke cheti cha kidato cha nne ambacho hakuwa nacho.

Kiuhalisia hana kabisa cheti hicho. Anasema aliwaambia hakuwahi kusoma sekondari wakamkatalia, akaenda TCU wakamwandikia barua kwenda UDSM wakishauri Shigongo aruhusiwe kuendelea na shahada ya pili licha ya kukosa cheti hicho cha kuhitimu kidato cha nne lakini hawakukubali.

“Yaani mimi nataka nisome masters (shahada ya uzamili). Nataka nisome tu nipate elimu halafu wananiambia lete cheti cha form four, sina hicho cheti.

Nikaenda TCU wakaniandikia barua kwamba huyu mtu amefaulu vizuri, nikapeleka UDSM wakasema hawataki,” anaeleza Shigongo jinsi safari yake ya elimu ilivyokwamia UDSM anakotamani kujiunga.

Kifo ni Haki Yangu

hariri

Katika hadithi inayosikitisha mojawapo ni kitabu "Kifo ni Haki Yangu" ambacho kinamzungumzia binti ambaye aliteseka sana katika maisha yake. Binti huyo aliokotwa na bibi mmoja aliyekuwa na vijana wawili; kwa bahati mbaya bibi huyo alisafiri, basi binti huyo alibakwa na vijana wawili kwa mkupuo.

Tokea hapo binti huyo alitokea kuwachukia wanaume; haikutosha, binti huyo alisaidiwa na mchungaji mmoja ambaye naye lengo kuu ni kumwingilia binti huyo kimwili. Siku moja mchungaji alimwambia binti huyo atengeneze juisi ya matunda, basi binti huyo akatengeneza juisi kama mchungaji alivyosema. Kumbe mchungaji alimwekea madawa ya usingizi kwenye glasi. Baada ya binti huyo kunywa hiyo juisi, mchungaji akamwingilia kimwili. Binti huyo alivyogundua ameingiliwa kimwili na mchungaji huyo, basi tokea hapo hakumwamini mwanamume yeyote, kwani aliamini kila mwanamume ni mdanganyifu na ni mkatili.

Lengo la kitabu ni kwamba tubadilikeː je, wewe ungekuwa mwanadada huyo ungefanya nini?

Vyanzo

hariri
  • Newspaper serials in Tanzania: the case of Eric James Shigongo (with an interview) / Uta Reuster-Jahn. In: Swahili Forum 15 (2008), S. 25-50. (Online hapa)
  Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Eric Shigongo kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.