Mkuu wa dola

(Elekezwa kutoka Head of state)

Mkuu wa dola (pia: Mkuu wa nchi) wa nchi ni kiongozi mwenye cheo kikuu. Lakini si lazima ya kwamba mkuu wa dola ana madaraka mengi sana. Hali inategemea na katiba ya nchi na utaratibu wake wa kisiasa. Pia si lazima ya kwamba nafasi ya mkuu wa dola inashikwa na mtu mmoja kwa sababu madaraka yake yanaweza kukabidhiwa pia kwa kamati ya viongozi.

Mkuu wa Dola katika Jamhuri

hariri

Katika mfumo wa jamhuri ya kisasa mkuu wa dola mara nyingi ni rais aliyechaguliwa na wananchi wote au na bunge.

Kimsingi kuna aina mbili za wakuu wa dola katika mfumo huu

Katika mfumo wa pili rais anaweza kuwa na madaraka muhimu hasa wakati waziri mkuu au serikali iko matatani au baada ya uchaguzi. Mara nyingi rais huwa na kazi ya kumkabidhi kiongozi wa chama kikubwa wajibu wa kuanzisha serikali na kutafuta kibali cha wabunge. Lakini kama hakuna chama kikubwa baada ya uchaguzi au ahieleweki kiongozi yupi atafaulu kukusanya wabunge wengi kwa kuunda serikali kuna nafasi ya rais ya kumteua kiongozi na kumpa nafasi.

Mfumo wa tatu ulipatikana zaidi katika historia ni kamati kama mkuu wa dola. Siku hizi inapatikana katika Uswisi (viongozi 7 wa serikali wanaobadilishana kila baada ya mwaka), Bosnia na Herzegovina (marais 3 kutoka kila dola la shirikisho wanaobadilishana baada ya miezi 8) na jamhuri ya San Marino (maraisi 2 kwa pamoja wanoitwa "capitani reggenti"). Umoja wa Ulaya si dola kamili kwa hiyo hakuna mkuu wa dola lakini kuna uraisi unaoshikwa na serikali za mataifa wanachama yote kwa kubadilishana zamu za miezi 6.

Katika nchi nyingi rais ana pia nguvu ya veto juu ya sheria zilizopitishwa na bunge. Hii ni pamoja na nchi ambako sheria zote au sheria kadhaa zinapaswa kutiwa saini na rais baada ya kupitishwa na bunge. Rais akikataa azimio la bungo haiwi sheria. Ama inarudi bungeni au mahakama kuu inapaswa kutoa azimio.

Mkuu wa Dola katika Ufalme

hariri

Katika nchi zilizo chini ya muundo wa ufalme (pamoja na emirati, usultani au utemi) mkuu wa dola anaitwa mfalme au sultani n.k.

Hapa kuna pia viwango vya madaraka kwa mfalme vinavyofanana na nafasi ya rais katika jamhuri.

Katika historia mara nyingi wafalme walikuwa na madaraka makubwa sana wakiunganisha uongozi wa serikali pamoja na nafasi ya hakimu mkuu na pia madaraka ya kidini.

Siku hizi kuna wafalme wachache tu ambao ni watawala wanaoshika madaraka yote ya serikali na hawabanwi na katiba katika utekelezaji wa utawala wao. Mifano yake ni wafalme au masultani wa Saudia, Omani, Qatar, Eswatini, Brunei na Papa kama mkuu wa Dola la Vatikani.

Lakini wafalme wengi wako chini ya utaratibu wa katiba ya nchi na mara nyingi wana nafasi inayolingana na rais katika mfumo wa serikali ya kibunge. Katika nchi hizi sheria na maazimio ya mahakama yanaweza kutangazwa kwa "jina la mfalme" lakini hali halisi kiongozi mwenye madaraka makubwa ni waziri mkuu kama kiongozi wa serikali aliyechaguliwa au kuthebitishwa na wabunge wengi. Katika Ufalme wa Maungano (Uingereza) malkia inatangaza kila mwaka shabaha za serikali bungeni lakini hali halisi anasoma tu hotuba iliyoandikwa na waziri mkuu.