Hekalu la Kihindu au Mandir ni mahali ambapo Wahindu huenda kuabudu miungu kwa namna ya murti (sanamu) mbalimbali. Mandir ni mahali pa kiroho kwa Wahindu ambako wanadamu na miungu hukutana kwa njia ya ibada na dhabihu. [1] [2] Katika imani ya Kihindu hakuna sharti la kusali hekaluni, maana ibada zote zinaweza kutekelezwa pia nyumbani.

Hekalu ya Uhindi Kusini
Mahekalu ya Kihindu huko Yogyakarta, Indonesia

Mahekalu ya Kihindu hupatikana katika mitindo mingi. Yapo katika maeneo mbalimbali yakitumia mbinu tofauti za ujenzi yakilingana na miungu tofauti na imani za kimaeneo. Hata hivyo, karibu yote yanashiriki dhana fulani za kimsingi, ishara na mandhari.

Kimapokeo mahekalu hayo yanapatikana katika Asia ya Kusini, hasa Uhindi na Nepal, Bangladesh, Pakistan, Sri Lanka, katika nchi za Kusini-mashariki mwa Asia kama vile Kamboja, Vietnam, Malaysia, na visiwa vya Indonesia.

Kutokana na kuhama kwa Wahindi kote duniani yanapatikana sasa pia nje ya Asia, kama vile huko Afrika ya Mashariki, Afrika Kusini, Amerika Kaskazini na Kusini, nchi kadhaa za Ulaya na kwenye maeneo ya Pasifiki.

Usanifu wa Hekalu hariri

Usanifu wa mahekalu ya Kihindu ulibadilika kwa kipindi cha zaidi ya miaka 2,000 na kuna aina kubwa katika usanifu huu.

Mahekalu ya Kihindu yana maumbo na ukubwa tofauti - mstatili, pembenane, nusuduara - na aina tofauti za kuba na milango. Mahekalu yaliyo kusini mwa Uhindi yana mtindo tofauti kuliko yale ya kaskazini. Ingawa kuna usanifu wa mahekalu ya Kihindu tofautitofauti, kimsingi yana mambo mengi yanayofanana.

Mahekalu mengi huwa na sehemu 6 zifuatazo[3]:

1. Kitovu cha hekalu mara nyingi ni chumba kidogo penye murti (sanamu) ya mungu mkuu wa hekalu hiyo. Wageni hawawezi kuingia humo bali ni makuhani wa hekalu pekee wanaoruhusiwa.

2. Juu ya chumba hicho paa huwa na umbo la kuba, na juu ya kuba kuna namna ya mnara au kilele. Kilele huwezi kuwa na umbo la piramidi au pia. Mnara huu ni mfano wa mlima mtakatifu Meru ambao huaminiwa ni makazi ya miungu.

3. Njia ya kuzunguka: hekalu kubwa huwa na njia ya kuzunguka chumba cha katikati kwa waumini wanaosali wakitembea na kukizunguka. Menginevyo njia hiyo inaweza pia kuzunguka hekalu kwa jumla.

4. Ukumbi wa Hekalu: Mahekalu mengi makubwa yana ukumbi. Waumini hutumia ukumbi kuketi, kutafakari, kusali, kuimba au kutazama makuhani wakifanya matambiko. Ukumbi huo kwa kawaida hupambwa kwa michoro ya miungu na miungu ya kike. Waumini wanaweza kupita hapa kusali mbele ya sanamu mbalimbali.

5. Baraza ya mbele: Eneo hili la mahekalu huwa na kengele kubwa ya metali inayoning'inia kutoka kwenye dari. Waumini wanaoingia na kutoka kwenye ukumbi hugonga kengele hii kutangaza kuwasili na kuondoka kwao.

6. Bwawa la maji: Ikiwa hekalu haliko karibu na eneo la asili la maji, beseni ya maji safi hujengwa kwenye eneo la hekalu. Maji hayo hutumika kwa matambiko na pia kusafisha sakafu ya hekalu au hata kuoga kiibada kabla ya kuingia katika makao matakatifu.

Marejeo hariri

  1. Stella Kramrisch (1946). The Hindu Temple. Motilal Banarsidass. ku. 135, context: 40–43, 110–114, 129–139 with footnotes. ISBN 978-81-208-0223-0. 
  2. George Michell (1977). The Hindu Temple: An Introduction to Its Meaning and Forms. University of Chicago Press. ku. 61–62. ISBN 978-0-226-53230-1. 
  3. "Everything You Need to Know About Hindu Temples". Learn Religions (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2023-03-21. 

Kujisomea hariri