Hifadhi ya Ziwa Manyara

(Elekezwa kutoka Hifadhi ya Manyara)

Hifadhi ya Ziwa Manyara ni hifadhi ya Taifa ya Tanzania iliyo maarufu sana nchini kwa simba wanaopanda juu ya miti. Aina hii ya simba hupatikana ndani ya hifadhi hii pekee barani Afrika.

Swala kwenye Ziwa Manyara.

Hifadhi hii iko umbali wa kilometa 126 kutoka Arusha mjini ina ukubwa wa kilometa za mraba 325 hivi.

Hifadhi hiyo iko katika Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, lakini mikoa hiyo miwili ya utawala haina mamlaka juu ya hifadhi, bali inasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Tanzania.

Jina la hifadhi hii limetokana na mmea wa mnyaa ambao katika lugha ya Kimasai hujulikana kama Elmanyarai na sehemu kubwa ya hifadhi hii ni ziwa Manyara.

 
Tembo katika hifadhi ya Ziwa Manyara.
 
Pundamilia wa Hifadhi ya Taifa ya Manyara.

Umaarufu wa hifadhi Ziwa Manyara unaongezeka kila siku kutokana na kukua kwa utalii wa ndani, ambapo wananchi wengi kutoka katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania hupenda kutembelea hifadhi hii. Idadi kubwa ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali nchini Tanzania hutembelea hifadhi hii kujionea maajabu ya dunia, hasa viumbe wa porini, wanyama, ndege na mimea. Vilevile, umaarufu wa hifadhi ya Ziwa Manyara unakua kutokana na wingi wa wageni wanaotokea nje ya nchi.

Hifadhi hii ipo ndani ya Bonde la Ufa ambalo kingo zake zinaongeza mandhari zaidi. Ziwa Manyara lililo ndani ya hifadhi ni kivutio kikubwa kwa watalii kutokana na wingi wa ndege aina ya korongo walio na mvuto mkubwa kwa kila mtu. Ndege hao huonekana kama pazia kubwa jeupe nyakati za mchana wanapokuwa ziwani kujipatia chakula na pumziko.

Wanyama wanaopatikana ndani ya hifadhi hii ni pamoja na simba, nyati, tembo, nyani, chui, pundamilia na wanyama wengine wanaokula majani. Hifadhi hii pia inasifika kwa wingi wa ndege, hasa heroe na mnandi ambao huonekana katika makundi makubwa na kufanya eneo hili la utalii kuwa na aina 400 za ndege wanaovutia.

Chemchem za maji moto ni maajabu mengine ndani ya hifadhi hii. Maji hayo yanayobubujika kutoka ardhini huonekana yakitoa moshi kama vile maji yanayochemka jikoni. Chemchem hizi za maji moto ya asili zimekuwa zikibubujika bila kukauka kwa kipindi cha mamilioni ya miaka.

Mji mdogo wa Mto-wa-Mbu ni kituo kikubwa cha biashara kinachotoa huduma kwa wageni wanaotembelea hifadhi ya Ziwa Manyara. Mji huu mdogo upo karibu na lango la hifadhi.

Wakati wa kutembelea

hariri

Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kuanzia mwezi Juni hadi Desemba baada ya mvua za masika.

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri

Majarida ya hifadhi za Taifa Tanzania

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Manyara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Hifadhi ya Ziwa Manyara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.