Kivuli
Kivuli ni eneo lenye nuru kidogo katika mazingira yenye nuru zaidi. Kinapatikana nyuma ya kitu kinachoangazwa upande mmoja lakini kinazuia nuru kuendelea na hivyo kuunda eneo lenye giza au nuru kidogo nyuma yake.
Kila kitu kisichopitisha nuru ndani chake kinaweza kuwa na kivuli kikiangazwa upande mmoja. Mfano wa gimba ambalo halina kivuli ni hewa au pia kioo safi dirishani.
Kwa maana pana zaidi kuna pia kivuli cha mnururisho usio nuru ya kuonwa kwa macho; mata ogania ndani ya mwili unapitisha au kuzuia mnururisho wa eksirei kwa viwango tofauti na kuonekana baadaye kwenye picha kwa rangi tofauti kutokana na "kivuli" dhidi ya mionzi hiyo.
Ukubwa na umbo la kivuli
haririUkubwa wa kivuli unategemea umbali wa gimba lenye kivuli na chanzo cha nuru. Kama gimba liko karibu na chanzo cha nuru kivuli huwa kikubwa zaidi, kama liko mbali kivuli huwa kidogo. Ukiweka mkono karibu na tochi kivuli chake huwa kikiubwa, kadiri unavyopeleka mkono mbali na tochi kivuli chake kinapungua.
Vilevile umbo la kivuli unategemea pembe ya kijiometria kati ya chanzo cha nuru na gimba. Hii inaonekana kwa kuzatama kivuli cha mtu au nyumba wakati wa mchana na wakati wa jioni. Jioni jua linaonekana chini zaidi angani, hivyo pembe ya nuru yake ni ndogo na kivuli kirefu. Kama jua liko juu kabisa angani kivuli huwa kidogo maana nuru inafika kutoka pande nyingi, hivyo kivuli kina nafasi ndogo tu, ni "fupi". Kama jua liko "chini" wakati wa asubuhi au jioni linaangaza upande mmoja tu, hivyo nafasi ya kivuli inakua.
Aina za vivuli
haririKama chanzo cha nuru kinafanana na nukta, kivuli ni kikali yaani kuna kivuli kamili tu kinachokaribia rangi nyeusi. Tofauti kati ya kivuli na eneo lenye nuru ni kali kama mstari uliochorwa. Lakini kama chanzo cha nuru ni kipana zaidi kuna ngazi mbili za kivuli yaani kivuli kamili (en:umbra) na nusu kivuli (penumbra). Kati ya nusu kivuli na maeneo yenye nuru mpaka si mkali tena.
Hali ya nusu kivuli inatokea pia kama gimba lilelile linaangazwa na vyanzo viwili vya nuru.
Kama chanzo cha nuru ni kipana sana kama anga lililofunikwa na mawingu kivuli kinaweza kupotea kabisa. Maana kiasi cha nuru kinatokea kote angani.
Kivuli na sanaa
haririTangu kale watu walitumia kivuli kwa mchezo na kutumia matokeo yake katika uchoraji.
Mchezo unaopendwa ni kupeleka mkono mbele ya chanzo cha nuru kama mshumaa au taa na kuunda kivuli kinachofanana na uso au mnyama fulani.
Katika nchi nyingi wasanii waliendelea kutumia maumbo ya watu, wanyama na vitu vingine vilivyokatwa katika karatasi na kuleta sura ya umbo kwenye kitambaa cheupe yakiangaziwa na nuru kwa nyuma.
Picha za vivuli
hariri-
Kivuli cha maandishi kinageuza mwelekeo wake.
-
Wakati wa mchana: kivuli kifupi
-
Kivuli kamili na nusukivuli chumbani kutokana na kipande cha pazia dirishani
-
Mchezo wa kivuli unaoonyesha picha ya ndege
-
Mchezo wa kivuli nchini Indonesia