Aktiki (pia: Aktika) ni sehemu ya kaskazini kabisa ya dunia yetu, ikijumlisha nchi na bahari inayozunguka ncha ya kaskazini. Sehemu za kaskazini za Urusi, Alaska (Marekani), Kanada, Greenland (Udani), Skandinavia (Norwei, Uswidi na Ufini) pamoja na bahari ya Aktiki huhesabiwa katika Aktiki.

Mstari wa buluu ni Duara ya Aktiki; mstari mwekundu eneo la Aktiki kufuatana na hali ya hewa kuwa chini ya 10 °C wakati wa Julai.

Zote huwa na hali ya hewa baridi mwaka wote.

Upande wa kusini wa dunia kuna eneo linalolingana na hilo ambalo huitwa Antaktiki.

Tabia za Aktiki hariri

Tabia kuu ya maeneo ya Aktiki ni baridi yake. Sehemu za karibu na ncha za dunia ni baridi kwa sababu zinapokea mwanga wa jua kwa muda wa nusu mwaka pekee na nusu nyingine kuna giza. Majira haya huitwa "usiku wa Aktiki" na "mchana wa Aktiki" na usiku au mchana hudumu miezi kadhaa.

Nchani kamili muda wa mchana huu ni miezi sita na pia muda wa usiku ni miezi sita. Kwa umbali fulani vipindi vya pambazuko vinaongezeka. Kwenye sehemu za kusini za Aktiki vipindi vya mchana ni virefu kuliko usiku, kwa hiyo kuna nafasi kwa mimea kustawi inayolisha pia wanyama mbalimbali.

Kutokana na baridi hiyo bahari ya Aktiki imeganda ikifunikwa na ganda nene la barafu. Kwa hiyo sehemu za Aktiki hufunikwa na barafu tupu mwaka wote na hizi ni sehemu kubwa za Greenland zinazofunikwa na barafuto, halafu Bahari ya Aktiki yenye ganda la barafu. Maeneo mengine yana theluji, lakini theluji hii huyeyuka kwa vipindi vifupi vya joto.

Ardhi imeganda pia yaani maji na unyevu ndani ya ardhi hupatikana kama barafu tu na hii inafaya ardhi kuwa ngumu kama mwamba. Wakati wa vipindi vya joto kwenye mchana wa Aktiki sentimita za juu za ardhi zinapoa na hiki ni kipindi cha mimea kuotea. Lakini chini ya uso wake ardhi bado imeganda na kwa sababu hiyo hakuna miti kwenye Aktikiː hakuna nafasi kwa ajili ya mizizi yao.

Mipaka ya Aktiki hariri

Hakuna mipaka ya Aktiki inayokubaliwa na wataalamu wote.

  • Mara nyingi watu humaanisha maeneo yote upande wa kaskazini wa "duara ya Aktiki" ambayo ni sawa na latitudo wa 66° 33’N. Hii ni latitudo ambako kila mwaka mara moja jua linaonekana angani kwa kipindi cha masaa 24 na vilevile mara moja jua halionekani kabisa kwa muda wa masaa 24. Kuelekea kaskazini ya hapa vipindi vya mchana na giza kabisa hurefuka hadi kufika nchani.
  • Wataalamu wengi hupendelea kuchora mpaka kufuatana na hali ya hewa halisi. Wanatumia kipimo cha halijoto ya wastani katika mwezi wa Julai kuwa chini ya sentigredi 10. Hii ni takriban sawa na mpaka wa miti yaani hakuna miti tena ambako halijoto ni baridi zaidi.

Mimea hariri

Kaskazini kabisa hakuna mimea isipokuwa plankton baharini chini ya barafu. Penye barafu ya kudumu hakuna mimea. Sehemu za kaskazini kwenye nchi kavu ambako theluji huyeyuka kwa siku chache tu mimea ya pekee ni aina za kuvu na kuvumwani. Kusini zaidi kadiri jinsi baridi kali inavyopungua nafasi za mimea huongezeka. Kuna manyasi, majani mbalimbali na hata vichaka vinavyofikia kimo cha mita 2 karibu na duara ya Aktiki.

Wanyama wa Aktiki hariri

Mimea hii inalisha mamalia kadhaa kama aina za sungura, panya, maksai maski au mbawala aktiki. Hao huvindwa na wanyama walanyama kama vile mbweha aktiki na mbwa mwitu. Kando ya bahari pale pasipoganda kuna mamalia wanaokamata samaki kama sili na aina za nyangumi. Dubu aktiki huvinda wanyama wote wengine akipendelea sili na samaki.

Nje ya mamalia kuna wadudu wengi wanaotokea kwenye kipindi cha joto pekee. Hao wanalisha pia ndege zinazokuja hapa wakati wa joto kwa kutaga mayai na kuzaa wadogo wao. Ndege wengine wanaokamata samaki huishi kando ya bahari.

 
Kijiji cha nyumba za barafu za Waeskimo mnamo 1865
 
Familia ya Waeskimo wakikalia sleji

Watu hariri

Kuna vikundi vya watu ambao wameishi katika mazingira ya Aktiki tangu karne nyingi. Wenyeji wa nchi za Aktiki ni Waeskimo wanaoishi Greenland, Kanada, Alaska na Siberia (Urusi). Kiasili ni wawindaji na wavuvi; walijenga nyumba za barafu wakati wa baridi na hema kwenye kipindi cha joto, lakini siku hizi huishi katika nyumba za kawaida. Kwa usafiri walitumia sleji zilizovutwa na mbwa.

Vikundi vingine vilivyoingia katika nchi za Aktiki ni pamoja na Wasami wa Skandinavia ya kaskazini na watu mbalimbali wa Siberia ya kaskazini ambao waliishi kama wawindaji au wafugaji wa mbawala aktiki.

Teknolojia ya kisasa imewezesha watu kutoka nje, kuhamia sehemu za Aktiki wanapofanya kazi kama wafanyabiashara, wachimba madini, wanajeshi au wanasayansi wanaochungulia mazingira hii ya pekee. Ni hasa madini kama vile dhahabu, mafuta ya petroli, makaa, shaba na chuma yaliyovuta watu wa nje kuja hapa.