Jumuiya ya Kilimo Tanzania

Shirika nchini Tanzania

Tanzania Agricultural Society, pia inajulikana kama Jumuiya ya Wakulima Tanzania (kifupi: TASO) ni shirika la chama cha wakulima kilichopewa jukumu la kuratibu maonesho ya kilimo nchini Tanzania. Ni chama kinachojitegemea ambacho kipo chini ya Wizara ya Kilimo.

Makao makuu yapo eneo la Dodoma Mjini kwenye makutano ya barabara ya Bunge, Mkoa wa Dodoma.

Historia

hariri

Tarehe 20 Oktoba 1992 Wizara ya Kilimo iliitisha Kikao mjini Arusha ambapo iliridhiwa kuanzisha Chama cha Kilimo Tanzania (Tanzania Agriculture Society Organisation - TASO) chombo mahsusi cha kuratibu maonesho ya Kilimo. Wizara ya Kilimo Mifugo na Ushirika ilisimamia kuanzishwa kwa chombo kisicho cha Serikali na kupewa jukumu la kuratibu na kuendesha Maonesho na Mashindano ya Kilimo. Chombo hicho kilijulikana kama “Tanzania Agricultural Society - TASO” na kiliandikishwa Serikalini mwaka 1993.[1]

Katika mwaka 1993 kwa mara ya kwanza, TASO iliratibu maonesho ya kilimo yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Mbeya kwenye uwanja wa Uyole ambao kwa sasa unaitwa Uwanja wa Maonesho ya Kilimo wa John Mwakangale. Vilevile mwaka 1994, TASO iliratibu Maonesho ya Pili ya Kilimo yaliyofanyika Kitaifa yalifanyika Morogoro kwenye uwanja wa Tungi ambao kwa sasa unaitwa Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

TASO kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo, Mifugo na Wadau wengine iliendelea kuratibu Maonesho ya Kilimo Kitaifa katika viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya Kanda. Viwanja hivyo ni Themi - Arusha, Mwl. J.K.Nyerere - Morogoro, John Mwakangale - Mbeya, Nzuguni - Dodoma na Ngongo - Lindi. Viwanja hivyo vilianzishwa kwa lengo la kuwa na uwanja wa Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kila Kanda. Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hufanyika kuanzia tarehe moja Mwezi Agosti na kufikia kilele tarehe Nane ya Mwezi Agosti kila mwaka. Wakati wa Maonesho hayo, wakulima na wadau wengine wanapata fursa ya kuoneshwa teknolojia mbalimbali za uzalishaji na usidikaji wa mazao, mifugo na uvuvi. Washiriki hushindanishwa na kupata Washindi kulingana na makundi ya bidhaa na teknolojia zao wanazoonesha. TASO imekuwa ikitoa zawadi kwa washindi mbalimbali kulingana na uwezo ilionao. Zawadi ambazo zimekuwa zikitolewa kwa Washindi ni Hati, Ngao, Zana za Kilimo, Pembejeo na Fedha taslimu. Serikali iliiwekea TASO utaratibu wa kutekeleza majukumu yake kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuipatia miongozo mbalimbali ili iweze kusimamia vyema Maonesho ya kilimo.[2] [3] [4]

TASO ilikabidhiwa maeneo mbalimbali makubwa kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo, Wizara za Kisekta, Mikoa na Halmashauri za Wilaya zilihusika pia kwa namna moja au nyingine katika kufanikikisha majumuku ya uratibu wa Maonesho kwa kushirikiana na TASO. [5] [6] [7]

Kwa mujibu wa Ibara ya 6 (a) ya Katiba ya TASO ya mwaka 1993 Toleo la mwaka 2009, Waziri wa Kilimo alipewa mamlaka ya kutoa maelekezo mahsusi au ya ujumla kuhusu uendeshaji wa TASO. Katika Wizara, uratibu wa Maonesho ya Kilimo umekuwa ukisimamiwa na Idara ya Maendeleo ya Mazao - Sehemu ya Huduma za Ugani.[8]

Marejeo

hariri
  1. "Maoni ya wadau mbalimbali wa maendeleo Tanzania" (PDF). Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
  2. "Sikukuu ya Wakulima Nane Nane". Mkoa wa Shinyanga. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2023-06-12. Iliwekwa mnamo 2023-06-12.
  3. "Sikukuu ya Wakulima Nane Nane". Wilaya ya Sumbawanga.
  4. "Sikukuu ya Wakulima Nane Nane". Arusha City Council. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2023-06-12. Iliwekwa mnamo 2023-06-12.
  5. "Sikukuu ya Wakulima Nane Nane". Dar es Salaam City Council.
  6. "Makabidhiano ya kiwanja cha TASO Nane Nane Arusha". Mkoa wa Arusha.
  7. Club, Arusha Press (Desemba 21, 2022). "Hatimaye TASO Kanda ya Kaskazini yapata Uongozi" [Hatimaye TASO Kanda ya Kaskazini yapata Uongozi Mpya.]. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2023-05-17. Iliwekwa mnamo 17 Mei 2023.
  8. "Wizara ya Maendeleo ya Mifugo Sera ya Taifa ya Mifugo" (PDF). Tanzania Natural Resource Forum. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2022-12-23. Iliwekwa mnamo 2023-06-12.