Vigae vya mwandiko wa kikabari

mfumo wa uandishi, hasa wa maandishi ya kikabari

Vigae vya mwandiko wa kikabari vilikuwa njia ya kuhifadhi habari kimaandishi katika utamaduni wa Mesopotamia ya Kale (takriban Iraki ya leo) na nchi jirani.

Vigae vya mwandiko wa kikabari.
Vigae vidogo vyaa mwandiko wa kikabari, takriban mwaka 2052 KK.

Ni vipande bapa vya udongo wa mfinyanzi ambamo alama za mwandiko wa kikabari zilichorwa na baadaye vipande vilikaushwa. Kama mwandishi alikosea, ilikuwa rahisi kusahihisha maandishi kwenye udongo mbichi. Vingine vilichomwa pia motoni na hivyo kuwa gumu kama matofali. Vigae elfu kadhaa vya mwandiko wa kikabari vilivyochomwa vimedumu miaka elfu na elfu hadi leo ni chanzo kikuu cha habari za kihistoria kuhusu tamaduni za kale.

Mifano ya kale kabisa iliyohifadhiwa ilitengenezwa mnamo mwaka 3000 KK[1].

Mesopotamia ilikuwa kitovu cha ustaarabu wa mapema wa kilimo wa miji kama Sumeri, Akkadi, Babeli na Ashuru. Mwanzo wa maandishi ilikuwa nia ya kushika kumbukumbu tu kuhusu akiba, idadi ya mazao, mifugo na bidhaa nyingine. Polepole waandishi wa Sumeri na Babeli walibuni mwandiko wa picha ulioendelea kuwa mwandiko wa alama zilizowakilisha maneno au silabi. Baada ya maendeleo hayo kuna pia matini marefu yaliyoandikwa kwa njia hii, kwa mfano Utenzi wa Gilgamesh.

Matumizi ya vigae hivi yalikwisha pamoja na matumizi ya mwandiko wa kikabari katika karne za mwisho kabla ya Kristo.

Marejeo

hariri
  1. Historic writing - The earliest form of writing Ilihifadhiwa 2 Mei 2017 kwenye Wayback Machine., Tovuti ya British Museum, London, iliangaliwa Machi 2017

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: