Kilima cha Mrima (pia: Kichakasimba, kwa Kiingereza: Mrima Hill) ni kilima chenye mwinuko wa mita 323 upande wa kusini wa Hifadhi ya Shimba Hills kwenye Kaunti ya Kwale, Kenya. Miguuni pake kuna kijiji cha Mrima. Jina la Mrima kwa kawaida linataja sehemu ya pwani inayoanza karibu na kilima hicho na kuelekea kusini hadi sehemu za Kilwa, Tanzania.

Kaya ya Mrima

hariri

Kilimani ipo moya ya kaya (misitu mitakatifu) za Wamijikenda iliyohifadhiwa chini ya sheria ya nchi[1]. Misitu ya kaya imeonekana kuwa maeneo muhimu ya bioanwai kwa sababu imani ya wenyeji ilizuia kukatwa kwa miti, kwa hiyo spishi nyingi za uoto asilia pamoja na wanyama zimehifadhiwa hapa ambazo zimeshapotea kwingineko[2]; hata hivyo sehemu ya Mrima Hill haikutajwa na UNESCO katika orodha ya Urithi wa Dunia[3].

Madini

hariri

Tangu mwaka 1919 iligunduliwa kwamba kuna akiba kubwa ya madini ya ardhi adimu katika kilima hiki. Utafiti huu ulithibitishwa baadaye na watafiti Wakenya na Waaustria [4]. Tangu mwaka 1990 inajulikana kwamba kuna pia madini yanayotoa kiwango kidogo cha unururifu kama vile thori, aktini na urani inayohatarisha afya ya wakazi wa karibu[5].

Mipango ya kuanzisha migodi

hariri

Mwaka 2013 kampuni ya Cortec Mining Kenya (inayomilikiwa na kampuni ya Kanada) ilipata kibali cha kuanzisha migodi ya kuchimba madini hasa niobi na ardhi adimu nyingine. Akiba za niobi zilikadiriwa kushika nafasi ya tano kwa wingi duniani [6].

Leseni hii ilibatilishwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2013 kwa shaka ya kupatikana kwa njia ya rushwa[7] [8].

Mwaka 2018 Serikali ya Kenya ilishinda kesi dhidi ya malalamiko ya kampuni ya Cortec.

Utajiri wa madini huko Mrima hutazamiwa kama nafasi ya kiuchumi lakini pia kama hatari kwa urithi wa kiutamaduni na wa kimazingira. [9]

Marejeo

hariri
  1. Mrima Hill sacred grove, Kenya Gazette 18 Mar 1994, uk 391
  2. linganisha utafiti kuhusu ndege wa Mrima Hill Britton, Britton & Coverdale: The Avifauna of Mrima Hill, South Kenya Coast; Scopus 4, Dec 1980, ilitolewa na Nairobi :East Africa Natural History Society's Ornithological Sub-committee.; tovuti ya Biodiversity Heritage Library
  3. Sacred Mijikenda Kaya Forests, tovuti ya UNESCO
  4. A. D. HORKEL: Notes on the Geology and Mineral Resources of the Southern Kenyan Coast, Mitt, österr. geol. Ges. Mo. 77/1984, pp. 151-15, Wien Dezember 1984
  5. Traveling the radioactive road, Kenyans live exposed to radiation from building material Archived 12 Septemba 2019 at the Wayback Machine., tovuti ya CNN November 4, 1999
  6. Kenya’s $100 billion hidden mineral deposits, The East African, Saturday July 20 2013
  7. Balala cracks the whipp, cancels 31 mining permits, tovuti ya Nation.co.ke ya Monday August 5 2013
  8. On Kenya’s Coast, a Struggle for the Sacred Jun 23 2015 (IPS)
  9. On Kenya’s Coast, a Struggle for the Sacred, IPS News, Jun 23 2015