Umwagiliaji

njia ya umwagiliaji wa maeneo yanayolimwa
(Elekezwa kutoka Kilimo cha umwagiliaji)

Umwagiliaji (ing. irrigation) ni mtindo wa kilimo wa kupeleka maji kwa mimea shambani pasipo mvua ya kutosha.

Shamba la ngano lililojazwa maji huko Arizona (Marekani)
Umwagiliaji wa njia ya matone; kwa wakulima wadogo kuna mbinu rahisi za kutumia mipira iliyotobolewa
Milango kama hii inatawala ugawaji wa maji katika mifereji ya umwagiliaji
Vinyunyizo vikubwa vinatupa maji mashambani
Umwagiliaji katika Sahara (Misri) kwa macho ya ndege: kila duara ina kipenyo cha kilomita moja
Umwagiliaji wa pamba kwa njia ya kinyunyizo kikubwa kinachozunguka nchani

Hutumiwa katika maeneo yabisi au wakati mvua ni kidogo. Katika nchi baridi unatumiwa pia kwa kusudi la kulinda mazao dhidi ya jalidi.

Ni kilimo ambacho kinasaidia sana, kwa mfano nchi ya Misri tangu zamani inategemea mto Naili katika shughuli zake za umwagiliaji wa mazao.

Chanzo cha maji

Umwagiliaji hutumia maji kutoka vyanzo mbalimbali:

Mbinu za umwagiliaji

Kuna mbinu nyingi za kumwagilia mazao. Tangu kale watu walichimba mifereji wa kupeleka maji mashambani. Mashamba yazungukwa kwa ukuta mdogo wa udongo na eneo la shamba lajazwa maji. Kujazwa kwa shamba kunarudiwa hadi mazao (kwa mfano ngano) yamekua. Mazao mengine kama mpunga hukuzwa mara nyingi ndani ya maji yanayofunika shamba kwa miezi kadhaa. Mtindo huu unaendelea kutumiwa hasa katika nchi nyingi za Asia na sehemu kubwa ya mchele duniani inapatikana kwa njia hii.

Mitambo kama pampu imewezesha wakulima kuachana na mifereji na kazi ya kugawa maji. Vinyunyizo vinamwaga maji kwa mashamba. Kuna mashine kubwa zenye matairi zinazozunguka kwenye ncha na kumwagilia duara. Nyingine zinazungushwa kwa nguvu ya maji na kutupa maji hadi umbali wa mita 500.

Katika nchi zenye uhaba wa maji kuna mbinu mpya ya umwagiliaji wa matone; mabomba au mipira yenye matundu madogo yanapelekwa shambani. Mimea inapandwa karibu na tundu la mpira. Wakati wa usiku pasipo joto kali maji yanatoka tone kwa tone kwenye bomba au mpira, hivyo yanafika moja kwa moja kwenye mizizi. Mbinu hii inatumia maji kidogo kulingana na umwagiliaji wa kawaida. Nchi ya Israeli imetangulia kulima mashamba makubwa upande wa kusini kwa njia hii, pamoja na kuwa na ukame sana.

Matatizo

Umwagiliaji huongeza mavuno kiasi kikubwa. Lakini kuongezeka kwa umwagiliaji duniani kumeleta matatizo mengi.

  • Matumizi ya maji yanazidi akiba yake; mito imekauka kwa sababu watu wengi mno wamechukua maji mle. Mfano mbaya sana ni ziwa Aral iligeuzwa kuwa jangwa kwa sababu maji ya mito yake yametumiwa kwa miradi mikubwa ya pamba katika mazingira ya joto kali tena kwa teknolojia isiyofaa kama mifereji iliyo wazi
  • Maji mengi yanapotea hasa pale ambako maji hupitishwa kwenye mifereji au na kujaza shamba kumwagiliwa kwa vinyunyizo. Sehemu kubwa inapotea kwa njia ya uvukizaji kuliko kulisha zao.
  • Pampu zimesababisha kushuka kwa uwiano wa maji chini ya ardhi. Hi ni hofu kubwa kwa umwagiliaji katika jangwa Sahara unaotumia akiba ya maji iliyojengwa na mvua wa milenia nyingi lakini inayopungua haraka tangu kuanzishwa kwa miradi ya umwagiliaji kwa pampu kubwa zinazovuta maji ya chini.
  • uharibifu wa mashamba ka kuongeza kiwango cha chumvi ardhini; katika mazingira ya joto uvukizaji wa maji unapeleka chumvi iliyoko ardhini juu; maji yavukiza lakini chumvi inabaki. Kuna mifano mingi ambako mashamba yameshaharibika kutokana na kuongezeka kwa chumvi. Maeneo yaliyolisha watu tangu kale yamekuwa jangwa kabisa.

Matatizo haya yote yanaonyesha ya kwamba haitoshi kumwagilia mashamba tu na kufurahia mazao mazuri kwa sababu matatizo yataongezeka baada ya miaka kadhaa. Kwa hiyo ni lazima kuangalia vema mbinu za uimwagiliaji inayolingana na mazingira na kutumia maji kidogo kama vile umwagiliaji wa matone.