King Kikii
King Kikii (jina la asili kwa Kilingala: Kikumbi Muanza M'pango, kwa Kiswahili: Kikumbi Mwanza Mpango: 1 Januari 1947 - 15 Novemba 2024) alikuwa msanii mkongwe wa muziki wa dansi Mtanzania mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kikii alijizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki kupitia sanaa yake ya muziki.
Akiwa mtunzi, mwimbaji, mpangaji muziki na mwenye ujuzi wa ujasiriamali wa kimuziki (alianzisha King Kikii Double O katikati ya miaka ya 1980), alitunga na kuimba vibao vingi sana vilivyokuwa gumzo miongoni mwa wapenzi wa muziki wa dansi. Mifano ya vibao vilivyompa umaarufu ni pamoja na Nimepigwa ngwala, Krismas - Bonne Année, Kasongo, Yoka mateya ya baboti, Mokili, Kyembe, (akiwa na Maquis du Zaire ya Kamanyola bila jasho) Mwaka wa watoto, Mimi msafiri, Haruna kaka, Ni kweli, Krismas Noelle, Mama Kabibi, (akiwa na Safari Sound ya Masantula ngoma ya mpwita) Salamule, Kitoto chaanza tambaa, Dodoma capitale, Kibwanange, na nyingine (akiwa na King Kikii Double O, ya 'Embala sasa') na kinachofahamika sana kwa sasa; Kitambaa cheupe.
Maisha
haririKing Kikii alizaliwa katika jiji la Lubumbashi kwenye mkoa wa Katanga (sasa Shaba) wa iliyokuwa Zaire [1]. King Kikii alielezea kuhusu kuzaliwa kwake na asili ya jina lake kwa kusema kuwa jina Kikii ni ufupisho wa jina 'Kikumbi' ambalo lilikuwa ni jina la [babu yake] mjomba wa mama yake aliyekuwa Chifu, Kikumbi Mwanza Mpango. Mwanza Mpango ndilo lililokuwa jina la kijiji cha Chifu Kikumbi Mwanza Mpango.
Wakati mama yake akiwa na ujauzito kabla yeye kuzaliwa, ilimjia ndoto. Aliyemtokea kwenye ndoto alikuwa yule mjomba wake Chifu Kikumbi. Akamwambia: "nimerudi, utanizaa. Ujauzito ulionao ni mimi, utakapojifungua umpe jina langu huyo mtoto."
Akiwa na umri wa miaka 6, Kikii akiwa anaishi kwenye mji wa Likasi na wazazi wake, alisikia kuwa kuna tamasha la muziki litakalotumbuizwa na wasanii kutoka Afrika Kusini. Yeye na kaka yake walihudhuria tamasha hilo. Lilikuwa kundi la Manhattan Brothers. Miongoni mwa wasanii wake alikuwa Miriam Makeba, Mama Africa.
Kikii alivutiwa sana na uimbaji wa kundi hilo hususan uimbishaji wa Makeba. Alizielezea sauti zao kuwa 'ni kama za malaika'. Naye alikariri baadhi ya mashairi ya nyimbo zao na kuishi nayo miaka yote.
Safari yake ya muziki
haririTamasha walilohudhuria lilikuwa chachu kwa Kikii na kaka yake (Jerome) kutaka kuwa wanamuziki. Kaka yake na marafiki zake wakaunda kikundi chao walichokiita Super Vea. Kikii na marafiki zake wakaunda kikundi chao walichokiita Bantu Negroes. Muda mfupi baadae baba yake alihamishwa kikazi kwenda Kolwezi. Waliishi kambini Musonoi iliyokuwa chini ya Union Miniére de Haut Katanga (Umoja wa Madini wa Mkoa wa Katanga) kwa sasa Gécamines (Générale des Carrières et des Mines).
Kutokana na uwezo wake katika kuimba, wanakikundi wenzake wakampachika jina la mwanamuziki maarufu wa iliyokuwa South Rhodesia na sasa Zimbabwe, Albert Ntindo Magaisa No.Two. Vijana hao aliokuwa nao walikuwa akina Izala Baignoire, Fessa Mumbunda na Malabane Store. Katika bendi hiyo, Kikii alikuwa mwimbaji pekee na alikuwa hodari wa kucheza. Akiwa na kikundi hicho alitunga wimbo Katanga.
Baba yake Kikii hakupenda mwanae afanye shughuli za muziki huku akiwa mwanafunzi tena wa shule ya msingi. Ili kuwa huru, Kikii alitoroka nyumbani kwao na kuishi na rafiki zake na kuendelea na muziki kadhalika shule.
Kutokana na uwezo wake wa kiakili, alifaulu vizuri mtihani wa la saba na kushika nafasi ya pili kwenye matokeo hayo. Taarifa hizo ziliwafurahisha wazazi wake ambao waliamua kumtafuta kwa udi na uvumba na kumpata. Wakamsamehe na kumrejesha nyumbani. Hiyo ilikuwa 1958, miaka 2 kabla ya Kongo kupata uhuru wake.
Kijana huyu aliendelea na muziki huku akisoma sekondari. Mnamo 1962, yeye na wenzake walikuwa kama waanzao rasmi kufanya kazi kiushindani na majina makubwa kama Joseph Tshamala Kabasele (Grand Kalle) wa African Jazz. Vile vile kulikuwa na shinikizo la namna fulani kutoka kwenye bendi ya Katanga Jazz (ya akina Jerome) la kutaka awe mwanamuziki wao. Kikii hakupenda kuwaacha wenzake. Aliwakatalia baada ya kujaribu kuwa nao kwa wiki moja.
Siku si nyingi, alitokea tajiri mmoja aliyekuwa na vyombo na kuingia mkataba na akina Kikii (ambao hawakuwa na vyombo bora) wa kuwakodisha vyombo. Wakapiga muziki kwa mara ya kwanza chini ya mkataba huo kwenye baa ilijulikana kama Quatre Vingts Possible. 'Mambo yalikuwa moto', alielezea Kikii. Na wakaendelea kupigia hapo mpaka wakafanikiwa kujilimbikizia fedha za kutosha na kuamua wafunge safari kwenda kununua vyombo vyao wenyewe.
Safari hiyo ilikuwa ya kuelekea Zambia. Huko ndiko ambako wangeweza kupata vyombo. Safari yao ilikuwa ya tabu. Wakati mwingine walilazimika kulala na njaa, wakati mwingine kujidhiki: watu wawili kula mkate mmoja kwa kinywaji cha maji yaliyoungwa sukari. Mji wa kwanza kufika ulikuwa Sakania ['Sakanya', Kongo ya kusini kabisa, kwenye mpaka na Zambia], wakalala, Kisha wakavuka mpaka wakaenda Ndola na kisha Mufulira na baadae Kitwe. Wakati huo huko kulikuwa na kampeni kali za kisiasa. Kenneth Kaunda akichuana na Umbula. Wakaulizwa; nyie mko upande gani, wa Umbula au Kaunda? Wao wakajibu: tupo upande wa UNIP, wa Kaunda. Wakapigiwa makofi kwa uchaguzi mzuri. Wakawachukua, wakawapatia chakula na sehemu ya kulala.
Kutokana na changamoto za kutomudu kununua mahitaji yao, akina Kikii walipitia wakati mgumu wakiwa Zambia lakini Mungu aliwasaidia na kuzishinda changamoto hizo na hatimae walipata vyombo walivyovitaka, ambavyo vilikuwa ni magita mawili, ngoma moja, amplifier mbili na vipaza sauti vyenye stendi, viwili.
Pamoja na kupata vyombo hivyo, bado kulizuka changamoto nyingine: hawakuwa na nauli ya kurudia. Uamuzi waliouchukua ukawa ni kurudi nyumbani kwa miguu. Wakaianza safari taratibu huku wakiwa wamevibeba vyombo vyao kichwani. Akili waliyotumia ni ya kubuni njia ya mkato kupitia mji wa Mokambo. Njiani, walimkuta mama mmoja atokae shambani akiwa kabeba mahindi mabichi na mihogo. Wakamtua mzigo huo na kuanza kuvila. Yule mama alishangaa na kuwasamehe.
Walipofika Mokambo (DRC), pale kuna stesheni ya reli na treni ingeweza kuwachukua hadi Lubumbashi. Lakini changamoto yao ilibaki kuwa ni ile ile: hawakuwa na nauli. Wakakuna vichwa wakapata suluhu ya tatizo: wafanye vibarua vya kupandisha na kushusha mizigo stesheni hapo ili wapate pesa. Wakawa wanajipikia wenyewe, ugali na mlenda pori. Vyombo vya kupikia walivipata kwa kuazima. Wakaendelea kudunduliza hadi nauli zilipotimia.
Wakasafiri hadi Lubumbashi na kushuka wakiwa wachafu hasa, lakini wamebeba vyombo vya muziki. Wakaulizwa: nyie akina nani? Wakajibu, sisi ni wanamuziki. Wakaambiwa, nyie ni wanamuziki gani wachafu namna hii? Kwa bahati, kulikuwa na bwana mmoja aliyepata kuwaona Kolwezi. Akasema: Ah - ah - ah, hawa watoto ni hodari sana. Ngoja niwachukue niwapeleke Katuba (wilaya).
Huko akawapeleka kwenye baa iliyoitwa Katuba Premiere ya bwana mmoja aliyeitwa Richard. Hapo kulikuwa na bendi kubwa iliyopiga muziki iliyoitwa Orchestra Bantu, iliyokamilika kivyombo. Mmiliki wa bendi hiyo nae alikuwa mwanamuziki. Kundi hilo liliwadharau akina Kikii. Lakini aliyewapeleka akamsisutiza mwenye baa awajaribishe. Wakapewa nafasi. Wakaenda kuoga na kujiweka watanashati. Wakati huohuo liliandaliwa pambano kati ya kundi la Kikii na bendi mwenyeji na majaji wa kuamua waliitwa.
Kilichoongeza ladha siku hiyo ni kuwa, mmoja wa majaji alikuwa mzee Bosco Mwenda wa Bayeke. Ikumbukwe kuwa hadhi ya Bosco kimuziki ni ya ngazi ya bara la Afrika. Muda ukawadia, wenyeji walianza kutumbuiza, wakafuatia akina Kikii. Wimbo wao wa kwanza ulikuwa 'Marie Shekita', Kikii aliuimba kwa ustadi sana kiasi kwamba baa nzima ilisisimka. Kwa ufupi walishinda na Bosco Mwenda alimsisitiza mwenye baa kuwa asiwaache watoto hao. Wakati huo mwenye baa mwenyewe alisha changanyikiwa.
Wiki iliyofuata, ile bendi 'ya wajivuni' ilikimbia (kwenda kwenye baa nyingine ya mjini hapo). Walijiepusha na aibu kwani kwenye mapambano, mashabiki walipaza sauti kwa kusema: tunawataka hao watoto. Hivyo walibaki wao wakilimiliki hilo eneo kama afanyavyo simba mtemi anapoteka eneo na kubaki na himaya yenye majike na kujisimika kuwa 'rais mpya' wa eneo hilo. Hiyo ilikuwa 1963.
Kikii na wenzake walifanya kazi kwenye eneo hilo kwa takriban mwaka mmoja na kujizolea sifa kemkem. Kufikia mwaka 1964 wakaona wabadilishe mazingira. Wakaondoka mkoa wa Katanga na kuelekea mkoa wa Kasai. Sababu ya kuichagua Kasai ni umaarufu wake kwenye biashara ya muziki. Kulikuwa na hela hasa. Changamoto iliyowakuta kwenye kipindi hicho ni ubadhirifu wa mwenzao aliyeshika fedha. Licha ya utafunaji fedha, pia aliviandikisha vyombo vya ubia kwa jina lake peke yake. Wakamtimua. Na, kwa bahati walipofika mjini Mbujimayi, walikuta baa iliyokuwa na vyombo full set na inatafuta wanamuziki. Baa hiyo iliitwa Mapumba Bar.
Wakati mwingine bahati huwa zinaongozana hadi unajiuliza Mungu ulimfurahisha wapi hasa na ukakosa jibu. Hilo liliwatokea akina Kikii. Mkataba walipata na wakapata wanamuziki wengine wakali wa kuongezea nguvu. Wakafanya nao mazoezi na kuibua vibao vizuri sana. Bosi akafurahi na kuwatafutia maskani mazuri. Shughuli za utumbuizaji zilipoanza, ukawa ni moto wa kuotea mbali. Wakapata mashabiki wengi sana.
Wakati huohuo ilikuja bendi nyingine ya akina Kasongo Mpinda Clayton wakitokea mji wa Kananga (Kasai ya pili). Walikuwa na wanamuziki wakali sana na wakawa wanatumbuiza mkabala na ilipokuwa Mapumba Bar. Jina la bendi hiyo lilikuwa Santa Fe. Ikawa pande zote zilijaza mashabiki na hao mashabiki walitaka kuingia kote; wakitoka kule wanaingia huku. Baada ya dansi, wanamuziki wa pande zote walikutana na kusalimiana na kufahamiana.
Mambo yaliendelea vizuri hadi mwaka 1967 ambapo Kikii alianza kuugua. Wakati akiugua, moto ulishuka kiasi, lakini kwa bahati akatokea tajiri mmoja aliyewahitaji. Wenzake Kikii wakamwambia, huyu mwezetu mwimbaji, anaumwa. Yeye akawaambia angewachukua na angebeba gharama zote za matibabu yake. Na ndivyo ilivyokuwa. Katika kipindi hiki, kundi lao liliongezewa nguvu na Celio kutokea Belabela ambaye aliacha uimbaji na kuwa mpiga sax (safu yao ya uimbaji ilishafikia watatu), jina la kundi lao likiwa ni Super Norvella. Kipindi hicho bendi nyingi kubwa zilikuwa zikienda Mbujimayi zikiwemo African Jazz, OK Jazz, Orchestre Nègro Succès, Conga Succès na nyingine. Hao walikuwa wakubwa sana na mkakati wa akina Kikii ukawa: walipokuja wao walipumzika na kwenda kuwasikiliza. Bendi ambayo aliikubali sana Kikii kati ya hizo ilikuwa African Fiesta Vita (Lililowaweka pamoja Tabu Let Rochereau na Dk. Nico Kasanda).
Tajiri aliyewahitaji alitekeleza ahadi yake. Alichukua jukumu la kumtibu Kikii kisha akawapeleka kwenye kijiji kulikokuwa kukichimbwa almasi kilichoitwa Tshaba. Huko alikuwa na baa yake ambapo akina Kikii walipigia muziki na Kikii alikuwa akiendelea kupata nafuu. Lakini katika 1967 hiyo hiyo, Kikii aliamua kurudi nyumbani kwao, mkoani Katanga kwenda kujiangalia kiafya na ni kipindi hicho ambapo alikutana na Bavon Marie-marie (Kiongozi wa Nègro Succès) na Bavon alimpenda na kutaka kumchukua akapige nae muziki. Kwa sababu ya kuugua kwake, haikiwezekana. Akabaki akitibiwa nyumbani kwao Likasi.
Wakati akiendelea kupata nafuu kiafya kwao Likasi (1968), ndipo bendi ya Vedette Jazz iliyokuwa imeenda Zimbabwe na kukaa huko miaka mingi, ilikuwa imerudi Kongo na kupitia Likasi. Kundi hilo lilikuwa na magwiji kama Mpudi Decca, Papito Fukiao na wengine wakiongozwa na muimbaji maarufu, Gabriel Talany almaarufu 'Bagueth' aliyekuwa na asili ya Congo Brazzaville. Kikii alimuweka muimbaji huyo daraja moja na Joseph Kabasele. Kikii alienda kwenye kundi hilo kuomba kazi. Mpudi Decca alipinga lakini Papito alimpigania ili apate kazi kwani naye alikuwa kijana kama Kikii na alitaka awe nao ili wapeane kampani ndani ya kundi lililosheheni watu wazima. Katika vuta nikuvute, Papito akakimbilia kwa kiongazi wa bendi, Bagueth, na kumtaka amsikilize kwanza. Kikii alipoimba mbele yake, palepale alisema: unaingia kwenye bendi. Papito aliruka kwa furaha. Ndani ya bendi hiyo, Kikii alifundishwa kuziimba nyimbo zao kumi ndani ya wiki moja. Alipoanza kuimba na Papito mambo yalikuwa bam bam. Baadae walimruhusu naye kutunga nyimbo zake (mfano, Anna) Ilikuwa hatari, na Mpudi Decca akampenda.
Wakati akifanya vizuri na Vedette, wenzake wa Super Gabbie waliokuwa Kalemie wakapata taarifa hizo. Wakamtuma Mwema Mujanga kwenda kumchukua. Awali, Kikii alikataa. Mujanga akaenda 'kuwalilia' wazazi wa Kikii ambao walifanikiwa kumshawishi Kikii kurudi kwa wenzie na kuwaacha Vedette. Bendi yote ya Vedette walisikitika sana. Super Gabbie inayozungumziwa hapa ni ile ya akina Mwema Mujanga, Tshimanga Kalala Assossa, Mbuya Makonga Adios na Mutombo Lufungola Audax(waimbaji). Wengine walikuwa ni mpiga solo Lubaba Maniola (Ilunga Lubaba), mpiga ridhim Bizos baadae akawa mpiga tarumbeta. Chinyama Chiyaza alikuwa akipiga marakas (manyanga) hakuwa akipiga sax, Tshibangu Paul Katai alikuwa akipiga tumba. Hawa alikuwa akipiga nao Likasi kabla Vedette hawajafika. Wakati huo Super Gabbie walikuwa wakiongozwa na Singa wa Singa (mpiga bezi).
Alipofika Hotel Palace (hoteli pamoja na baa), Kalemie, bendi ilisimamisha huduma zake kwa wiki moja ili ifanye mazoezi na Kikii. Wakafanya vizuri sana. Baadae wakapata mwaliko wa kwenda Kamina. Kamina ni mji wa nne kwa ukubwa huko Katanga. Hata Nguza Viking anatokea huko. Pia Kikii ameufungua masikio umma wa mashabiki wa dansi kuwa Singa wa Singa na Ilunga Ngoy Bizos ni ndugu wa kuachiana ziwa.
Walipofika Kamina, kwa bahati mbaya, dada yao akina Singa wa Singa, Kasongo Charlotte, alifariki kwa ajali Lubumbashi. Dada huyo alikuwa maarufu sana. Akina Singa wakaenda msibani. Wakati huohuo Nguza na mwenzie mmoja waliwaambia akina Kikii, 'nyimbo zenu zote tunazijua'. Wakaomba kazi. Walipojaribiwa wakaonekana wanafaa. Nguza akawa anapiga bezi na mwenzie ridhim. Waliporudi akina Bizos wakawashukuru na kutaka kuwaacha. Kikii akafanya utetezi kwa kusema tumchukue mmojawapo, na kupendekeza awe Nguza. Akachukuliwa. Baadae walibaini kuwa Nguza alikuwa na uwezo wa kupiga solo pia.
Wakarudi Kalemie. Pale, yule mmiliki wa Hotel Palace, bwana Yamba Yamba, alikuwa mkorofi, mwenye tabia ya kikoloni. Yeye alikuwa anataka mara dansi likiisha, isisikike sauti ya aina yoyote. Amri hiyo ilikuwa ngumu kwa Kikii na Ilunga Bizos. Siku moja aliwakemea wakati wakipata vinywaji baada ya dansi. Kikii alichukia na kumkunja shati (kumkaba) na kumwambia 'hey, hiyo si tabia nzuri'. Yule bosi alichukia sana kiasi cha kumnyatia na chuma Kikii akiwa amelala. Alitaka ampige nacho kichwani. Kwa bahati njema, mwimbaji Kasilembo Freddie alimwona na kupiga kelele zilizomshtua Kikii na ndio ikawa salama yake. Vinginevyo Kikii angepoteza maisha siku hiyo.
Maamuzi ya bosi huyo baada ya tukio hilo, yakawa ni kuwafukuza yeye na Bizos. Kwa bahati Kikii alikuwa na kaka yake aliyekuwa gavana mdogo wa Kalemie. Kikii alikimbilia kwake. Hiyo ilikuwa ni bahati nyingine kwani bwana mkoloni alishatuma watu wakawapige. Kwa bahati mbaya Bizos yalimfika, lakini Kikii alinusurika. Akiwa kwa bw. gavana, Kikii alipata barua toka kwa Kasheba aliyekuwa Tanzania wakati huo, akimtaka aende huko (Tz) wakashirikiane kwenye masuala ya muziki. Hiyo ilikuwa Juni, 1970. Akawataarifu wenzake wa Super Gabbie juu ya nia yake ya kumfuata Freddie Ndala Kasheba wa L'Orchestre Fauvette. Nao wakamruhusu kwani walifahamu machafuko yaliyotokea. Kwa ufahamisho tu, ni kwamba Kikii, Kasheba na Kabeya Badu, wote walitokea Likasi.
Kwa mujibu wa Kikii, yeye alikuwa akiisikia sana Dar Es Salaam na Tanzania kwa ujumla na alikuwa akitamani afike. Haja hiyo iliongezeka zaidi kipindi Mwalimu Nyerere alipozuru Kongo, enzi za Mobutu. Kikii alimpenda sana Mwalimu na kujiuliza: huko [Tanzania] nitapakanyaga lini? Ikawa ni fursa, na waliomletea barua wakawa wanamsubiri waende nae. Hao walikuwa Paul na Chinyama (ambao walijifunza kupiga sax baada ya ule mwaliko wa Kamina)
Walisafiri kwenda Tz kwa kupanda meli na kuvuka ziwa Tanganyika. Alipofika Kigoma, mshangao wake wa kwanza juu ya tamaduni za Tz ni vazi la baibui. Aliona akina mama wakiwa wamejitanda mavazi myeusi. Kisha wakasafiri kwa treni hadi Dar. Akina Kasheba walimpokea kwa furaha sana.
Wakiwa Dar, wanamuziki wote wa Fauvette walikuwa wakikaa Whitehouse, Ubungo. Bendi hiyo iliyokuwa na wanamuziki hodari kama Kikii, Kasheba, Johnson, Kabala Jojo, Mubaya Kikii na wengine, walizikonga sana nyoyo za mashabiki wa Dar na kukubalika. Baadhi ya mashabiki wao walikuwa watu mashuhuri kama mzee Kessy Mjinga, Wilfred Mwabulambo, Bhoke Munanka, na wengine.
Mwaka 1971 Atomic Jazz ya Tanga waliwaalika Fauvette wakatumbuize mkoani humo. Walifanya hivyo na Kikii alisema, Atomic ndio waliowafungulia njia ya kwenda Kenya kurekodi nyimbo zao zilizokuwa zikitamba kama Jacqueline, Zula, Voyage Emonani, Vivi, Maria Na Kampala, na nyingine. Kisha walirejea na kuendelea kupiga dansi.
Mwishoni mwa 1972, Fauvette waliondoka Dar na kuelekea magharibi mwa Tanzania. Mwaka huohuo bendi hiyo ilibadili jina na kujiita Orchestre Safari Nkoy. Walianzia Bujumbura, Burundi, ikiwa imeshaingia 1973; kisha wakaingia Bukavu mkoani Kivu (Kongo), wakaenda mpaka Goma na Luchuru na baadae Kishasha (sio 'Kin' ). Kisha wakaingia Uganda wakianzia na Kasese, karibu na ziwa Edward, kisha Mbarara, Masaka hadi Kampala. Walipotoka Kampala wakaenda Jinja.
King Kikii aliachana na Safari Nkoy mwaka 1974. Kati ya mwaka huo na 1977 Kikii alifanya kazi Kinshasa na Kalemie.
Bila shaka, mtu angependa kujua alijiungaje na Maquis du Zaire mwaka 77 hiyo hiyo. Inabidi kurudi nyuma kidogo: wale akina Chimbuiza Chinsese Nguza Mbangu Viking (Babu Seya) aliowaacha Kalemie wakati akienda Dar (Juni 1970) walibadilisha jina la bendi kutoka Super Gabbie na kuwa Maquis du Zaire [Makyii du Zaire]. Ilikuwa 1972 na mwaka huohuo Maquis walihamia Dar, na kuweka makazi yao Kinondoni. Mtindo waliotumia ulikuwa Chakula kapombe.
Maquis walifanya kazi Dar bila Kikii kwa miaka mitano. Wakahitaji kuongezea nguvu, na walisikia kuwa wakati huo Kikii alikuwa Kalemie. Ndipo walipoituma mashine, Paul Tshibangu Katai, akamchukue. Pia walikuwa na hoja ya msingi: Kikii alikuwa na hisa Maquis. Chifu Kikumbi Mwanza Mpango Mwema alikubali wito huo na pamoja naye, aliongozana na akina Banza Mchafu, Mutombo Sozy, Kanku Kashama na Ngalula Tshandanda, kwenda kuipiga jeki Maquis.
Akiwa na Maquis du Zaire, Kikii alifanya kazi kubwa iliyotukuka ikiwemo na kuanzisha mtindo mpya wa Kamanyola bila jasho. Mifano ya kazi alizong'ara nazo zimetajwa kwenye sehemu tangulizi ya makala. Ilipofika tarehe 25 Julai 1979, nguli huyo aliondoka Maquis du Zaire na baadae kuibuka kwa kishindo akiwa na kundi la Orchestra Safari Sound aliloliongoza mwenyewe na kuanzisha mtindo 'uliosumbua' sana wa Kamanyola bila jasho. Baadhi ya vibao alivyotamba navyo vimetajwa pia. Ni katika kipindi hicho ambapo mashabiki walimpachika jina la King na alibaki nalo maisha yake yote ya mbele.
Mwaka 1982 King Kikii alirejea Maquis du Zaire kwa muda. Moto wake ulikuwa uleule. Mwaka 1983, King alianzisha bendi yake aliyoiita 'Orchestra King Kikii Double O.' Mtindo wa bendi hiyo ulikuwa Embala sasa. Mirindimo ya bendi hiyo ilikuwa mitamu na tofauti kabisa na ya bendi yoyote ile. Bendi hiyo ilipofikia ukingoni, King alipumzika kidogo kisha akafanya kazi na Zaita Musica, Sambulumaa Band na hasa La Capitale Wazee Sugu wa Kitambaa cheupe.
Mungu amlaze pema peponi King Boniface Kikumbi Mwanza Mpango Mwema.
Kuugua na kufariki
haririKifo chake kilichotokea akiwa na umri wa miaka 77 (sababu ikiwa ni saratani ya ini)[2], kimesababisha huzuni nyingi kwa wapenzi na wadau wa muziki wa dansi wa kada zote. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia ukurasa wake wa Instagram [3]ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu na Watanzania kwa ujumla na sehemu ya maelezo yake yasomeka:
"Kwa zaidi ya miaka 50, King Kikii ametoa burudani kwa mamilioni ya Watanzania na amekuwa mlezi na mwalimu wa wengi katika tasnia ya muziki. Tutamkumbuka na kumuenzi kwa kazi zake nyingi na nzuri ikiwemo wimbo wake maarufu wa 'Kitambaa Cheupe' ambao umeendelea kuwa sehemu ya burudani kwenye maeneo na shughuli mbalimbali za burudani nchini"
Kabla ya kulazwa kwake katika awamu hii iliyoambatana na msiba, yaya kulutu (kaka mkubwa) Kikii, amekuwa akiugua kwa kipindi cha takriban miaka mitano na kushindwa kuendelea na shughuli zake za muziki. Miongoni mwa matibabu aliyopitia ni pamoja na upasuaji kwenye eneo la shingoni la mwili wake.
Marejeo
hariri- ↑ http://basahama.blogspot.com/2014/09/ujue-safari-ya-muziki-ya-king-kiki.html
- ↑ https://www.ippmedia.com/nipashe/habari/kitaifa/read/hii-hapa-sababu-kifo-cha-king-kikii-samia-amlilia-2024-11-15-114212
- ↑ https://www.ippmedia.com/nipashe/habari/kitaifa/read/hii-hapa-sababu-kifo-cha-king-kikii-samia-amlilia-2024-11-15-114212