Kiwavijeshi wa Afrika

Kiwavijeshi wa Afrika
Viwavijeshi chanjari (Spodoptera exempta)
Viwavijeshi chanjari (Spodoptera exempta)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Lepidoptera (Wadudu walio na mabawa yenye vigamba)
Nusuoda: Glossata {Lepidoptera wenye ulimi unaoweza kuviringwa)
Familia ya juu: Noctuoidea (Nondo kama nondo wa nyanya)
Familia: Noctuidae (Nondo walio na mnasaba na nondo wa nyanya)
Nusufamilia: Hadeninae (Nondo wanaofanana na viwavijeshi)
Jenasi: Spodoptera (Viwavijeshi)
Guenée, 1852
Spishi: S. exempta
Walker, 1856

Viwavijeshi wa Afrika ni viwavi wa nondo Spodoptera exempta katika familia Noctuidae. Wakiwa wengi sana viwavi hawa hutembea chanjari na kwa hivyo wanafanana na sufa ya jeshi. Baada ya kuwa wapevu hujikusanya katika makundi makubwa na kuhama mbali kubwa.

Viwavi hawa wana rangi zinazotegemea idadi yao (polyphenism) ambapo lava wanaokua kwa upweke ni kijani, wakati wale wanaokua katika vikundi ni weusi. Awamu hizi zinaitwa “solitaria” na “gregaria”, mtawalia. Viwavi wa gregaria wanachukuliwa kuwa wadudu waharibifu sana wenye uwezo wa kuharibu mazao yote katika wiki kadhaa. Lava hujilisha kwa kila aina ya nyasi: hatua za mwanzo za mazao ya nafaka (k.m. muhindi, mpunga, ngano, mwele na mtama) na za muwa. Mara kwa mara hula mnazi pia. Viwavi wa solitaria hawafanyi shughuli sana na hupitia maendeleo polepole.

Spishi hii hupatikana kwa kawaida katika Afrika lakini pia inaweza kuonekana huko Yemen, visiwa kadhaa vya Bahari ya Pasifiki na sehemu za Australia. Milipuko ya viwavijeshi wa Afrika huwa waharibifu kwa mashamba na malisho katika maeneo haya, na milipuko ya idadi za juu hujitokeza wakati wa mvua baada ya vipindi vya ukame wa muda mrefu. Wakati wa viangazi virefu, idadi za wadudu ni chini sana na milipuko haionekani.

Mzunguko wa maisha

hariri

Majike wanaweza kutaga kiwango cha juu cha takriban mayai 1,000 katika maisha yao. Wanaweza kutaga mayai 100-400 kwa usiku na wastani wa 150. Idadi ya mayai ambayo majike wanaweza kutaga inaunganishwa vyema na uzito wa mabundo yao. Viwavijeshi wa Afrika hutaga mayai yao kwa vishada kwenye pande za chini za majani. Mayai haya ni madogo kiasi yenye kipenyo cha mm 0.5. Ni meupe mwanzoni wakitagwa, lakini huwa meusi kabla viwavi hawajatoka. Viwavi hutoka ndani ya siku mbili hadi tano.

Viwavi

hariri

Spishi hii hupitia hatua sita za viwavi ambazo pamoja zinaweza kudumu kati ya siku 14 na 22 kulingana na nyuzijoto na uoto katika mazingira. Viwavi waliokomaa wa hatua ya sita wana urefu wa mm 25-33.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, rangi ya viwavi inategemea idadi ya wadudu. Viwavi wanaokua baina ya wadudu wachache ni kijani wenye mlia wa hudhurungi kupitia urefu wa mgongo wao na huitwa "solitaria". Wale wanaokua baina ya wadudu wengi ni weusi wenye milia myembamba njano kwenye mwili wao na huitwa "gregaria". Tofauti za muonekano kati ya awamu za solitaria na gregaria huonekana dhahiri katika hatua ya tatu na zinabaki hadi hatua ya mwisho. Spishi hiyo inaharibu mazao sana wakati wa awamu yake ya gregaria kwa sababu viwavi wenye mwili mweusi hukiakia zaidi na kujikusanya pamoja zaidi kuliko viwavi wa solitaria. Viwavi wa solitaria hawakiakii sana na huwa wanakaa chini ya mazao wakijikunja, na hivyo hawapati mionzi mingi ya jua. Kwa sababu viwavi wa gregaria huwa na rangi nyeusi na kudumisha mahali pa juu ya mazao, wanaongeza mfiduo kwa jua, ambayo inaleta ukuaji wa haraka zaidi kuliko viwavi wa solitaria. Kwa ujumla, viwavijeshi wa Afrika hawatambuliwi na wakulima hadi viwavi wana umri wa siku kumi na kuanza kuonyesha awamu ya gregaria.

Mabundo

hariri

Badiliko katika mabundo hufanyika takriban sm 2-3 chini ya uso wa ardhi katikati ya vimelewa na mbali na ardhi tupu. Kisa hiki cha kuwa mabundo husababisha kutoweka ghafla kwa viwavi wote pamoja, haswa ikiwa udongo ni mnyevu.

Wadumili

hariri

Wadumili huibuka katika siku 7 hadi 10 na huweza kuishi hadi siku 14. Upana wa mabawa ya nondo mpevu ni mm 20-37. Mabawa ya mbele ni kahawiakijivu na mabawa ya nyuma ni meupe yenye vena zinazoonekana. Majike na madume wanaweza kutofautishwa na idadi ya manyoya magumu kwenye kulabu ya kupashia mabawa, ambapo madume huwa na unyoya mmoja wakati majike huwa na kadhaa. Majike pia hutambulika kwa sababu ya ncha ya fumbatio yenye umbo la raketi na vigamba vyeusi. Madume wamezingatiwa kukomaa mapema kuliko majike.

Uhamiaji na milipuko

hariri

Wakati viwavijeshi wa Afrika wanapotoka katika mabundo yao, kwanza wanangojea mwili wao ukauke na mabawa yao yawe magumu kabla ya kupanda miti. Kisha nondo huruka mamia ya mita juu ya ardhi na hutegemea pepo kuwabeba mpaka mahali pengine. Kwa hivyo uhamiaji hutegemea pepo zinazoletwa na Ukanda wa Makutano wa Kati ya Tropiki, ambao husonga kaskazini au kusini kulingana na msimu. Nondo husafiri tu wakati wa mchana na hushuka wakati wa jioni ili kujificha kwenye nyasi hadi alfajiri. Wendo huu unarudiwa kwa siku kadhaa hadi kufika mwisho ukubalikao wa safari au mpaka nondo wanakuta mvua. Kwa sababu mvua husababisha nondo kushuka, haielekei kwamba watahama wakati wa kunyesha mara kwa mara. Baada ya kutua ardhini, nondo hunywa maji, kupandana na kutaga mayai yao. Uhamiaji ni mzuri kwa sababu unaruhusu spishi kusafiri kwenda mahali papya penye mbuai wachache na uwezekano mdogo wa udusio na maambukizo.

Spishi hii ni msumbufu mbaya wa mazao. Mara nyingi hustawi wakati wa majira ya mvua na kusababisha milipuko. Hiyo inatukia baada ya vizazi kadhaa vilivyofanikiwa. Wakati wa milipuko hiyo viwavi wa gregaria hutoka ardhini wote pamoja na idadi yao inaweza kuzidi 1,000 kwa . Viwavi hawa huonyesha tabia nyamilifu ya kujilisha, ambayo husababisha ulaji mkubwa sana wa uoto ulio karibu, haswa majani ya nyasi na mazao ya nafaka. Wakiwa na njaa sana viwavi wa gregaria wanaweza kula mashina na maua ya mimea pia. Baada ya kumaliza uoto wa mahali fulani idadi kubwa ya viwavi huandamana chanjari kama jeshi ili kupata uoto mpya. Wakati viwavi hawa huwa wadumili, hawa huenda katika makundi makubwa lakini kejekeje juu ya upepo.

Udhibiti

hariri

Awamu ya gregaria ya kiwavijeshi wa Afrika inachukuliwa kuwa wadudu wasumbufu kwa kilimo kwa sababu ya idadi kubwa na tabia yao ya kujilisha. Zamani dawa za kiuawadudu za bei rahisi zinazoua wadudu aina nyingi, kama DDT, BHC na dieldrin, zilitumika kulenga viwavi, lakini njia hizi zinategemea kipimo na zina athari mbaya kwa afya ya binadamu na mazao. Siku hizi viuawadudu vipya vinapulizwa mara nyingi, kama vile azadirakhtini na maji yenye uto wa mbegu za mwarobaini (Azadirachta indica). Sasa njia ya udhibiti wa kibiolojia inapatikana pia katika umbo la nucleopolyhedrovirus wa S. exempta (African armyworm#SpexNPV), ugonjwa wa asilia ambao huambukiza spishi hii. Virusi hii huzalishwa nchini Tanzania, lakini matumizi yake hadi sasa imekuwa ya kukatisha tamaa. Mawakala wa serikali wanapendelea kutumia dawa za kikemikali zilizoingizwa kutoka nje, ambayo huwaruhusu kuweka mfukoni asilimia fulani.