Mageuko ya spishi

(Elekezwa kutoka Kubadilika wa viumbe hai)

Mageuko ya spishi (kwa Kiingereza: evolution) ni nadharia ya kisayansi iliyobuniwa na kutumiwa na wataalamu wa biolojia, hasa tawi la jenetikia.

Mti wa uhai huonyesha mabadiliko wa spishi tangu mwanzo wa uhai

Inasema ya kwamba spishi za viumbehai zilizopo duniani leo zimetokana na spishi zilizokuwa tofauti za zamani.

Nadharia hii inategemea hoja ya kwamba awali uhai wote ulitokana na maumbo asilia.

Katika wazo hili spishi zote jinsi zilivyo sasa zinaendelea kubadilika kutoka mifumo rahisi ya maisha kuelekea mifumo kamili zaidi.

Mabadiliko hayo huonekana hasa pale ambapo viumbe vizalia huwa na sifa tofauti na zile za wazazi wao. Sifa hizi ni ishara za jeni ambazo hupitishwa kutoka kwa mzazi kwenda kwa watoto wakati wa uzazi. Tabia tofauti huwa zinapatikana ndani ya makundi ya viumbe kutokana na mabadiliko katika jeni za viumbe hao, mabadiliko ya maumbile na vyanzo vingine vya mabadiliko ya maumbile.

Mageuko hufanyika wakati michakato ya mageuko kama vile uteuzi wa asili (pamoja na uteuzi wa kijinsia) na mabadiliko makubwa ya mkondo wa jeni huchangia katika mabadiliko haya, na kusababisha tabia nyingine kuwa za kawaida au nadra katika kundi la viumbe hai. Ni mchakato huu wa mageuko ambao umetoa mabadiliko ya bioanuwai katika kila kiwango cha asasi ya biolojia, pamoja na viwango vya spishi, kiumbe mmojammoja na molekuli.

Msingi wa nadharia hii ni mabaki ya kisukuku ya viumbehai ambao hawapo tena duniani lakini wanafanana kiasi na viumbehai wa leo, pamoja na ulinganifu wa spishi za karibu na za mbali zaidi. Nadharia ya mageuko ya spishi inalenga kueleza mabadiliko hayo.

Leo hii ndiyo nadharia ya kibiolojia inayokubaliwa na wataalamu wengi hata kama kuna wapinzani kadhaa, hasa upande wa wenye imani kali ya dini, lakini pia wachache kwa sababu za kitaalamu.

Mchango wa Darwin

hariri

Mtaalamu Mwingereza Charles Darwin anajulikana kama mvumbuzi wa nadharia hii.

Kadiri yake, mageuko hayo hufuata uteuzi asilia yaani viumbehai wanaolingana vizuri zaidi na mazingira wanaishi na kuzaa kushinda viumbehai wasiolingana nayo.

Kwa njia hiyo tabia za viumbehai wanaofaa zaidi zinazidi kuendelezwa kwa sababu watoto wao hurithi tabia hizo. Lakini tabia za viumbehai wasiofaa sana zinaweza kutoweka kwa sababu wanakufa mapema na hawana watoto wengi wanaoendeleza tabia zao.

Darwin alishambuliwa mara nyingi kwa hoja ya kwamba mafundisho yake yanapinga taarifa ya uumbaji katika Biblia. Lakini hiyo inategemea jinsi masimulizi yake yanavyosomwa: si lazima mwamini achukue kila kitu kama ilivyoandikwa, kwa sababu Biblia hailengi kutufundisha sayansi, bali njia ya wokovu.

Marejeo

hariri

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mageuko ya spishi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.