Kuelea hewani
Kuelea hewani (kwa Kiingereza: levitation, kutoka Kilatini levitas, yaani wepesi), kinyume cha kawaida inayotokana na sheria ya mvutano, ni hali inayoweza kusababishwa duniani na kuelezwa na sayansi kwa namna mbalimbali.
Kunaweza pia kufanyika kwa mazingaombwe.
Wanaomuamini Mwenyezi Mungu wanaweza kukubali hali hiyo itokee kama muujiza wake, inavyosemekana iliwatokea baadhi ya watakatifu (kama Thoma wa Akwino, Katerina wa Siena, Filipo Neri, na hasa Yosefu wa Kopertino). Tukio hilo ni la mwili kuinuka juu mbali na ardhi bila sababu yoyote ya kueleweka, hivi kwamba unabaki hewani pasipo kutegemezwa na kitu chochote. Kinyume chake kuna matukio ya mwili kuwa na uzito mkubwa usio wa kawaida.
Papa Benedikto XIV alidai kwanza tukio liwe limethibitika, ili kukwepa ujanja wowote. Halafu alionyesha kwamba tukio hilo halielezeki kisayansi kwa sababu ya elekeo la mvutano, lakini halipiti uwezo wa kuinua miili walionao malaika na shetani; kwa hiyo ni lazima kulichunguza vizuri upande wa mwili, maadili na dini lisiwe limesababishwa na ibilisi; mambo yote yakilingana tunaweza na kupaswa kuliona limesababishwa na Mungu au na malaika kwa kuijalia miili ya watakatifu utangulizi fulani wa wepesi wa miili mitukufu mbinguni.