Uchaguzi wa Kura Tatu

(Elekezwa kutoka Kura Tatu)

Uchaguzi wa Kura Tatu ulikuwa uchaguzi wa kwanza Tanganyika uliofanyika mnamo mwaka wa 1958 ambapo serikali ya kikoloni baada ya kushindwa ilikubali ufanyike uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya rangi. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi maalum.

Baraza la Wazee wa TANU Sheikh Suleiman Takadir wa pili chini kulia, wa pili waliosimama Dossa Aziz, wa sita Julius Nyerere, wa saba John Rupia, wa tisa Said Chamwenyewe, anayefuatia Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate.
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza kukubalika na TANU. TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari, 1958 kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya haya masharti ya kibaguzi yaliyowekwa au isusie uchaguzi.

Mkutano wa Tabora hariri

Mkutano wa Tabora ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao makuu, Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU, kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama mapande mawili kama isingelikuwa busara ya Mwalimu Nyerere, Abdallah Rashidi Sembe, Hamisi Heri na viongozi wa TANU wa Tanga ambao walipanga mkakati wa kuwashinda 'siasa kali' katika chama.

Mgogoro wa Kura Tatu hariri

Ili kuzielewa hisia za wanachama wa TANU, uongozi wake na nguvu zilizokuwa zikidhibiti siasa Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa kwa nini Kura Tatu ilizua mgogoro na kutoelewana katika uongozi. Shida ilianzia Tanga mahali ambapo Mwalimu Nyerere na uongozi wa TANU Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa Tabora. Baada ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika mkakati wa Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Mwalimu Kihere na Mwalimu Nyerere uliofanya wafuasi wa siasa za wastani wawashinde wale waliokuwa na msimamo mkali. Inasikitisha kuwa kisa hiki cha ujasiri na mbinu za hali ya juu kama zilivyoonyeshwa na watu wa Tanga hadi leo kimebaki siri kuu. Wanaokifahamu kisa hiki wengi wao wameshakufa.

Baraza la Wazee wa TANU hariri

Sehemu kubwa ya wanachama wa TANU walikuwa Waislamu; kwa hiyo ilikuwa ni dhahiri kuwa kuyakubali masharti yale ya kibaguzi ya upigaji kura ilikuwa sawa sawa na kuwasukuma Waislamu ambao ndiyo walikuwa wafuasi wakubwa wa TANU nje ya wigo wa siasa. Ujumbe wa Mwalimu Nyerere mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na wajumbe wengi ambao wasingeweza hata kidogo kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao Makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na Mwalimu Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Azizi, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani.

Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislamu kule Dar e Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyika usingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Baraza la Wazee wa TANU likiwa na wajumbe takriban mia mbili na sabini Waislamu watupu, walikuwa hawawezi kupiga wala kupigiwa kura. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi.

 
Kushoto: Mwalimu Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Clement Mtamila, Bi. Titi Mohamed, Nyuma ya Sheikh Takadir ni Mama Maria Nyerere, Rajab Diwani na John Rupia

Serikali ya kikoloni, ikishirikiana na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislamu elimu, sharti lile lile ambalo sasa linawekwa kuwazuia Waislamu kushiriki katika siasa. Hakuna kumbukumbu zozote zinazoeleza mawazo ya Mwalimu Nyerere katika suala la Kura Tatu wala hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa faragha pale Makao Makuu na washirika wake wa karibu kama Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz Mafongo, Haidar Mwinyimvua, Dossa Azizi au Bibi Titi Mohamed.

Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani Mwalimu Nyerere alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika Kura Tatu katika masharti yale. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya hewa ya siasa kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu kuona kwa nini Mwalimu Nyerere ilibidi afiche msimamo wake katika suala la Kura Tatu kama TANU ilivyotwishwa na serikali. Mwalimu Nyerere alikuwa anafahamu hatari iliyokuwa ikinyemelea TANU kutokana na Kura Tatu. Alijua wazi ili kukinusuru chama na mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi haraka na kwa makini kabla ya kwenda kwenye mkutano Tabora.

Safari ya Tanga ili kujenga mkutano salama wa Tabora hariri

 
Kushoto: Iddi Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu.

Siku chache kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU, Mwalimu Nyerere na Amos Kisenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga, kuhusu matatizo yaliyoletwa na uchaguzi wa Kura Tatu. Mkutano huu baina ya Mwalimu Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa na Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Ng'anzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta. Mwalimu Nyerere alizungumza waziwazi na kwa dhati ya moyo alikiambia kikao kile kuwa amekwenda Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa Kura Tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje. Mwalimu Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa uwezo wa kuzungumza vizuri. Mwalimu Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora. Mwalimu Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima ishiriki katika uchaguzi kwa sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu UTP ushindi bila jasho kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika maamuzi yatakayotolewa na seriakli katika siku zijazo.

Kufichuka kwa msimamo wa Mwalimu Nyerere wa kutaka TANU iingie katika Kura Tatu kulishtua uongozi wa Tanga. Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa msimamo wa Mwalimu Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi wote wawili Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa Mwalimu Nyerere na uchaguzi wa Kura Tatu. Mwalimu Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya Kura Tatu itakapokuja anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe, TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP iliyokuwa na nguvu Tanga kwa sababu ya walowezi waliokuwa wakimiliki mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii akina Rashid Sembe walikuwa wameelemewa na mashambulizi kutoka kwa wapinzani.

Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lillilokuwa na nguvu sana likiongozwa na Mmaka Omar kama mwenyekiti na Akida Boramimi bin Dai akiwa katibu. Hawa wote ni marehemu na mchango wao hadi leo haujathaminiwa. Mwalimu Nyerere na Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani ili ifanyike tawaswil. Waliohudhuria kisomo hicho walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu, Akida Boramimimi bin Dai na Mmaka Omari.

Abdallah Rashid Sembe na mjadala wa Kura Tatu hariri

Wakiwa Tanga walipiga dua nzito ya kutakia heri mkutano wa Tabora, huku Mwalimu Nyerere akiongoza ujumbe mkubwa sana kutoka makao makuu. Ile agenda ya uchaguzi wa Kura Tatu ilipoanza kujadiliwa, mkakati wa Tanga uliofanyiwa dua maalum kwa Mwenyezi Mungu katika kijiji cha Mnyanjani ukaanza kutekelezwa. Mwalimu Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano aliomba amwachie kiti Mwalimu Kihere ili apate fursa ya kushiriki katika mjadala na kutoa mchango wake. Mara tu baada ya Mwalimu Kihere kuchukua kiti aliutuliza mkutano na akamchagua Sheikh Abdallah Rashid Sembe kuwa msemaji wa kwanza kama vile walivyopanga kule Tanga majuma machache yaliyopita.

Sembe alihimiza TANU kushiriki katika uchaguzi. Kama vile Baba wa Taifa alivyotabiri mapema, zogo kubwa lilizuka. Wajumbe walipiga makelele, wakagonga meza kwa hasira, wengine wakawa wanaburuza meza na viti kwa makelele kudhihirisha hamaki zao. Jumanne Abdallah, Bhoke Munanka kutoka Jimbo la Ziwa walisimama na kumlaani Abdallah Rashid Sembe wakimwita msaliti. Sheikh Sembe alishikilia msimamo wake kuwa TANU ni lazima iingie uchaguzi unaokuja ili ishinde uchaguzi na katika ushindi huo iwe na uwezo wa kufutilia mbali mfumo huo wa dhulma. Mwalimu Nyerere alisimama na akamuunga mkono Sheikh Sembe. Mwalimu Nyerere alitoa hoja katika misingi hiyo hiyo kuwa ili TANU iweze kuondoa Kura Tatu ni lazima kwanza iingie kwenye Kura Tatu. Wajumbe hawakuafiki hoja ya Mwalimu Nyerere. Wote walishikilia msimamo wa TANU kususia uchaguzi. Hamaki za watu zilikuwa wazi ndani ya ukumbi wa mkutano wa Mwalimu Kihere aliahirisha kikao hadi siku ya pili ili kuwapa wajumbe muda wa kutuliza hamaki zao.

Siku iliyofuata ustadi wa Mwalimu Nyerere katika mjadala ulitumika. Mwalimu Nyerere akizungumza kwa vitendawili na methali, aliwauliza wasikilizaji wake, je, ingewezekana kwa mkulima mwenye busara, aliyelima na kupanda shamba lake kwa taabu, angesita kuvuna mazao yake kwa kuhofia kuchafua nguo zake, kwa sababu tu, ili afike shambani kwake itabidi avuke mto wenye matope. Watu wangelimuonaje mkulima kama huyo? Mwalimu Nyerere aliwaeleza wale wajumbe kuwa, TANU iko njia panda, ingekuwa kazi bure kwa wakati huu kwa TANU kususia uchaguzi baada ya kufanya kazi yote ile kwa shida kubwa hadi kufika hapo walipofika. Kususia uchaguzi ingekuwa ni kujiingiza katika mtego. Adui angefurahi kuona imenasa katika mtego, TANU ikisimama pembeni na UTP ikiingia katika uchaguzi na kuchukua viti vyote katika Baraza la Kutunga Sheria. Serikali ya kikoloni ingefurahi sana kuona kitu hiki kinatokea.

Mwalimu Nyerere na Sheikh Abdallah Rashid Sembe ambaye alihatarisha uhai wa yeye kuwapo katika TANU katika suala la uchaguzi wa Kura Tatu walikuwa washindi. Hata hivyo agenda ya Kura Tatu ilibidi ipigiwe kura. Kura ilipopigwa kundi la akina Sheikh Suleiman Takadiri waliotaka kuususia uchaguzi walishindwa: kura 37 zilipigwa kuunga mkono kushiriki uchaguzi wa Kura Tatu dhidi ya 23 zilizotaka ususiaji. Mwalimu Nyerere alitia sahihi Azimio la Tabora ambalo baadaye lilikuja kujulikana kama 'Uamuzi wa Busara.'

Siku ile Mwalimu Nyerere alipokuwa akiweka sahihi yake watu hawa wafuatao ndiyo walikuwa wamemzunguka: kwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere alikuwa amesimama makamu wa rais wa TANU, John Rupia; upande wake wa kushoto alikuwepo Amos Kissenge, aliyekuwa kakaa nyuma ya Mwalimu Nyerere akiwa amevaa kofia ya mkono, koti na kanzu alikuwa Mzee Jumbe Tambaza mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU, upande wake wa kulia alikuwa kijana Juma Selemani maarufu kwa jina la lake la utani, 'Juma Mlevi', katibu wa Bantu Group. Mwisho wa meza wakitazamana alikuwa Bibi Titi Mohamed kwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir kwa upande wake wa kushoto.

 
Mohamed Jumbe Tambaza, Mjumbe Baraza la Wazee wa TANU

Baada ya kutia saini kwa Azimio la Tabora Mwalimu Nyerere alimpigia simu Zuberi Mtemvu makao makuu Dar es Salaam kumuagiza awatangazie wananchi kuwa TANU imepiga kura kuingia katika uchaguzi wa Kura Tatu. Siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma simu ya maandishi kwa rais wa TANU, Mwalimu Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujiuzulu kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama chake cha upinzani - African National Congress (ANC) Chama cha Mtemvu kilikuja kujulikana kama 'Congress' neno ambalo kwa mtazamo wa vyama hivyo pinzani lilikuja kunasibishwa na usaliti. Mtemvu akimshutumu Mwalimu Nyerere kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na TANU na wananchi kwa kuwatumbukiza katika Kura Tatu; na Mwalimu Nyerere akimshutumu Mtemvu kwa kujitenga na mapambano na kujiunga na upinzani ili kudhoofisha TANU, na hivyo kusaliti harakati za kudai uhuru. Hadi leo Mzee Mtemvu na wazee wengi wa TANU hawafahamu kuwa mkakati wa Tabora ulipikwa Mnyanjani.

 
Kushoto: John Rupia, Julius Nyerere, Zuberi Mtemvu. Waliosimama nyuma yao ni BANTU Group Vijana Walinzi wa Viongozi wa TANU.

Kabla ya kuondoka Tabora Mwalimu Nyerere lifanya mkutano wa hadhara soko kuu la Tabora na kuelezea maamuzi ya mkutano mkuu. Hotuba ya Mwalimu Nyerere ilijaa hisia kali. Aliwaambia wasikilizaji wake kuwa endapo Waingereza watakaidi kutoa uhuru basi wananchi wataelekeza kilio chao kwa Mwenyezi Mungu. Wakati ule TANU ilikuwa na dini hakukuwa na lugha ya sasa ya 'chama chetu hakina dini'. Mwalimu Nyerere alipotamka maneno haya hakuweza kujizuia, akaangua kilio na vilio vya wananchi waliouelewa uchungu wa dhulma vikatanda uwanja mzima. Baada ya hotuba hii iliyowaliza watu, wananchi wengi ambao walisita kujiunga na TANU sasa waliingia kwa wingi. Ni vigumu kuamini lakini watu huko Tabora walisimama msururu usikukucha kukata kadi za TANU.

Huyu ndiye Sheikh Abdallah Rashid Sembe, muasisi wa TANU ambae amekufa akiwa mwanachama mtiifu wa CCM na kwa viongozi wake. Mkutano wake wa mwisho aliohudhuria wa CCM ulikuwa Mkutano Mkuu uliofanyika Dodoma Novemba, 1997 ambao alihudhuria kama mwalikwa. Kwa bahati mbaya sana mkutano huu ulimalizika kwa fedheha kwa upande wa Sheikh Rashid Sembe. Bila ya kujali umri wa Sheikh Sembe na nafasi yake ya usheikh, msichana mcheza ngoma akiwa nusu uchi alikwenda kucheza ngoma mbele yake na huku akinengua alimkalia Sheikh Sembe mapajani. Gazeti moja la kila siku bila ya tafakuri ikachapisha picha ile ya Sheikh Sembe akiwa katika mavazi yake ya Kiislamu ya kanzu, koti, kofia na kilemba katika ukurasa wake wa mbele. Waislamu wengi walikasirishwa na kuhuzunishwa na picha ile. Wapo waliomlaumu Sheikh Sembe kwa kuhudhuria mikutano ya kitwaghut na wapo walioilaumu CCM kwa kuachia Sheikh Abdallah Rashid Sembe avunjiwe heshima na halikadhalika wapo waliolilaumu gazeti.

Wengi wa wanasiasa wa sasa katika ukumbi ule wa mkutano walikuwa wakimpita Sheikh Sembe bila ya kujua kwa hakika yule mzee aliyevaa Kiislamu katika ukumbi ule alikuwa nani na nini ulikuwa mchango wake katika siasa za Tanganyika. Hata hivyo historia ya uhuru wa Tanganyika na hata maisha ya Mwalimu Nyerere yatakapoandikwa hayatakamilika bila ya kumtaja Sheikh Abdallah Rashid Sembe.[1]

Tazama pia hariri

Marejeo hariri

  1. Habari kamili kuhusu Azimio la Tabora katika Wavuti ya Mohamed Said. Jalada kutoka ya awali juu ya 2018-07-13. Iliwekwa mnamo 2016-09-12.

Viungo vya Nje hariri