Lango:Afrika/Intro
Afrika ni bara la pili duniani kwa ukubwa, likiwa na eneo la kilometa za mraba zipatazo 30,370,000 na kwa idadi ya wakazi, hao wakiwa 1,225,080,510 (mwaka 2016). Asia ndiyo bara pekee la kushinda Afrika.
Neno "Afrika" limetokana na lugha ya Kilatini ya Roma ya Kale. Waroma kwa jina hilo hawakumaanisha bara lote bali eneo katika Tunisia ya leo tu. Asili yake ni kabila la "Afrig" lililoishi sehemu zile. Wakati huo Wagiriki wa Kale walitumia zaidi jina la Libya kwa ajili ya nchi kusini kwa Bahari ya Mediteraneo. Maeneo ya ndani kuelekea kusini mara nyingi yaliitwa kwa jina la "Ethiopia" linalomaanisha nchi ya watu weusiweusi (kwa Kigiriki "aithiops": aliyechomwa na jua).