Mbegha
Kwa habari za mnyama (kima) tazama "Mbega"
Mbegha (pia: Mbega)[1] (* baada ya 1700)[2] ni jina la mtu muhimu katika historia ya Washambaa anayekumbukwa kama mfalme wao au mwene mkuu wa kwanza katika kundi hili. Familia ya watawala iliyoanzishwa naye hujulikana pia kama nasaba ya Kilindi.
Washambaa ni wakazi wa milima ya Usambara katika Tanzania kaskazini-magharibi.
Mtoto kigego anayefukuzwa na ukoo
haririKufuatana na "Habari za Wakilindi"[3] Mbegha kiasili alikuwa mtoto wa Mwarabu aliyetoka Pemba na kuhamia Kilindi na mke wake Mngulu. Inaonekana ya kwamba waliishi baadaye kati ya Wangulu. Mbegha anakumbukwa kama mtoto kigego aliyetangulia kupata meno ya juu iliyotazamiwa kama ishara baya kati ya makabila mbalimbali na mara nyingi waliuawa. Labda kwa sababu babake alikuwa Mwislamu mtoto aliruhusiwa kuishi lakini baada ya kifo cha wazazi na kakaye alinyimwa urithi wake na nduguye waliomkumbuka kama kigego na kumshtaki kuwa ni mchawi.
Mwindaji maarufu
haririMbegha aliamua kuondoka katika ukoo uliomkataa akawa mwindaji aliyeishi msituni. Alikuwa stadi sana kwa sababu alikuwa kati ya watu wa kwanza waliotumia mbwa wa kuwinda akampenda hasa mbwa wake Chamfumu. Alipata umaarufu kwa sababu alifaulu kupunguza nguruwe mwitu waliokuwa tishio kubwa kwa wakulima na mazao kwa hiyo walimheshimu na kumpenda. Vijana walikuja kukaa naye akawafundisha mbinu za uwindaji.
Alisemekana kujua pia mbinu za uganga zilizomsaidia kuwinda, kuwashinda maadui na pia kuponya watu.
Kilindi
haririBaada ya kuondoka katika Ungulu alihamia kwanza Kilindi alipokumbukwa kutokana na babake na pia umaarufu wake kama mwindaji. Chifu wa mji akampatia nyumba akawa rafiki wa mwana wa chifu. Siku moja walipoenda pamoja kuwinda huyu kijana aliuawa na nguruwe mwitu na Mbegha aliona hawezi kurudi Kilindi akiogopa hasira ya chifu akaamua kuhama tena akiongozana na vijana 14 na mbwa zake.
Chifu wa Bumbuli
haririPamoja na kundi lake walizunguka wakapiga kambi huko Zirai kando la Usambara. Wazee wa Bumbuli wakamkaribisha kuja kwao na chifu Mbogho alimpa binti yake kama mke akampandisha kuwa chifu pamoja naye.
Sifa zake zilisambaa kati ya Washambaa. Wakati ule Washambaa wa Vuga walikuwa na vita dhidi ya Wapare wakaona wapate usaidizi wa Mbegha. Kiongozi wa Vuga akamwendea akamwomba kuhamia kwao na kuwa mwene wao. Mbegha aliomba kibali cha mkwe akaongozana na watu wa Vuga pamoja na mke na shemeji yake.
Mwene wa Vuga
haririHuku Vuga alikaribishwa kwa mapigo ya ngoma kubwa watu wengi wakaju kumkaribisha wakamjengea nyumba alipoingia. Mkewe alikuwa mja mzito tayari akamwandaa kitanda kilichofunikwa kwa ngozi ya simba aliyomwahi kuua safarini kuelekea Vuga. Mtoto aliyezaliwa juu ya ngozi ya simba akapokea jina la Simba akawa mrithi wake wa baadaye akipewa pia jina rasmi la Buge. Kutokana na jina hili watawala wa Vuga waliendelea kutumia cheo cha Simba Mwene [4]. Baadaye huyu mwana wa kwanza alikuwa chifu wa Bumbuli kwa kibali cha baba.
Mbegha aliendelea kuoa mabinti kutoka koo za Washambaa mbalimbali na kuweka wanawe kutoka ndohizi kama watawala na wawakilishi wake juu ya vijiji vya mama zao. Kwa njia hii aliunganisha Usambara na koo za Washambaa na kuweka msingi kwa utawala wa kifalme katika Usambara uliosimamia sehemu kubwa ya Tanzania ya kaskazini kabla ya kuja kwa Wazungu. Watawala wa nasaba yake waliomfuata Vuga waliendelea kuoa wake wengi na kuweka wana wao kama watawala wadogo mahali pa mama.
Mzee Mbegha alipongojeka alikaa pamoja na wazee 5 pekee waliomtunza siku tatu hadi alipoaga dunia. Hao wazee hawakutangaza kifo chake waliendelea kuandaa mazishi na ufuasi wake kimyakimya. Walituma ujumbe kwa Buge - Simba aje haraka babake ni mgonjwa. Mbegha alizikwa katika kaburi ndani ya ngozi ya ng'ombe dume mweusi pamoja na paka mweusi. Buga alipofika alitangazwa mara moja kuwa mwene mpya.
Urithi wake
haririHabari za Mbegha zimehifadhiwa katika masimulizi wa watu na kuandikwa mara ya kwanza na Al-Ajemi mwisho a karne ya 19. Wataalamu wa historia waliokusanya historia ya Usambara tangu wakati wa ukoloni walikamilisha historia ya Al Ajemi kwa habari za kieneo.
Hata Mbegha akikumbukwa kama mfalme wa kwanza wa Washambaa kuna wasiwasi kama yeye mwenyewe alitawala kwelikweli au kama alikuwa tu na athira athira kubwa kama mpatanishi na mshauri wa koo mbalimbali.
Lakini kwa hakika alianzisha nasaba ya Kilindi iliyoungansha na kutawala Usambara pamoja na maeneo jirani hadi ukoloni. Wengine wanaona mtawala kamili wa kwanza alikuwa Buga aliyemwua babu yake Mbogho na hivyo kushika utawala kamili juu ya Vuga na Bumbuli[5]. Mwana wa Buge aliyeitwa Kinyashi alianza kupanusha himaya yake kwa njia ya vita, na mtoto wake Kimweri ye Nyumbai alisimamia kilele cha uwezo wa nasaba hii mnamo 1850 akitawala Usambara, Usegeju, Digo na Bondei pamoja na sehemu za Useguha, Upare na tambarare za Maasai. Hata maliwali wa Pangani na Tanga waliokuwa chini ya Sultani wa Zanzibar walilipa kodi za kuthebitishwa vyeo vyao kwa mtawala wa Vuga.[6]. Baadaye biashara iliyopita bondeni iliongeza utajiri wa machifu wa Mazinde waliofaulu kuvunja kipaumbele wa Vuga baada ya 1860.
Marejeo na vyanzo
hariri- ↑ tahajia zote mbili zinapatikana k.m. A. Werner anayeandika Mbega; wenyeji huelekea kutumia "gh" tazama majina mengine ya Kishambala chini
- ↑ Tarehe za kuzaliwa au kufa kwake hazijulikana wala umri wake. Makadirio yanawezekana kutokana na kukadiria umri wa wastani wa watawala waliomfuata hadi Kimweri ya Nyumbai aliyekufa 1862; taz. Iliffe uk 63
- ↑ Historia ya nasaba ya watawala wa Usambara iliyoandikwa na Abdallah bin Hemedi al Ajemi na kutolewa 1895 - 1906; toleo la Nairobi 1962 na East African Literature Bureau, mhariri JWT Allen; sehemu kubwa wa makala hii inafuata taarifa ya A. Werner inayorudisha historia ya Ajemi.
- ↑ A. Werner anaeleza ya kwamba jina alilopewa Mbegha utotoni lilikuwa "Mwene" kwa hiyo kiasili Simba Mwene haikuwa cheo bali jina lenye maana "Simba mwana wa Mwene". Hata hivyo cheo hiki cha Simba Mwene imetafsiriwa kwa Kiingereza kama the Lion King iliendelea kuwa jina la filamu mashuhuri ya Walt Disney
- ↑ ling. Fage/Oliver uk. 510
- ↑ taz. Bückendorf uk.30
- Alice Werner, The Wakilindi Saga; chapter 9 in: Myths and Legends of the Bantu 1933; reprint 2005 ISBN-10: 0404161766 # ISBN-13: 978-0404161767
- http://www.sacred-texts.com/afr/mlb/index.htm inaonyesha maandishi ya kitabu cha A. Werner kwenye intaneti
- J. D. Fage & Roland Anthony Oliver, The Cambridge History of Africa: From c. 1600 to c. 1790; mlango "From Usambara to the coast" uk 510. (kupitia google-books)
- Jutta Bückendorf, "Schwarz-weiß-rot über Ostafrika!", uk 27-30 (kupitia google-books)
- Basil Davidson, East and Central Africa to the late 19th century; London 1967 / reprint 1974, uk. 185-188
- Philip Briggs, Tanzania: With Zanzibar, Pemba & Mafia, uk 226-228 (kupitia google-books)
- John Iliffe, A modern history of Tanganyika, ISBN 9780521296113, Cambridge 1979