Kwa "wali" kama chakula tazama wali (chakula)

Liwali wa Dar es Salaam mnamo 1961.

Liwali au wali ni cheo cha msimamizi wa eneo fulani.

Cheo cha Kiarabu

hariri

Asili ni neno la Kiarabu "الوالي" al-wali linalomaanisha mtawala wa mahali au eneo asiyejitegemea bali aliyeteuliwa na serikali kushughulikia mambo ya utawala katika eneo fulani. Mara nyingi katika nchi za utamaduni wa Uislamu Wali alisimamia "wilaya". Kazi yake ililingana na "gavana".

Cheo cha Uswahilini

hariri

Katika eneo la Waswahili neno al-wali lilikuwa "liwali"[1] na lilimtaja mkuu wa mahali au wa mji. Masultani wa Zanzibar waliteua maliwali kwa ajili ya miji ya pwani waliokuwa wawakilishi wa sultani mahali walipo.

Mwaka 1886 kulikuwa na maliwali wafuatao wa Zanzibar kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki: Tungi, Mikindani, Lindi, Kilwa Kivinje, Kikunye, Kisiju[2]

Cheo cha kikoloni

hariri

Katika mfumo wa utawala wa Kiingereza katika Afrika ya Mashariki liwali ilikuwa cheo cha afisa wa ngazi ya juu zaidi kilichopatikana kwa wazawa katika utawala wa miji.

Cheo hiki kiliendelezwa kwenye pwani ya Kenya baada ya Uingereza kuchukua mamlaka juu ya pwani kutoka Sultani wa Zanzibar; liwali alipaswa kuwa Mwislamu. Alisimamia mahakama ya liwali iliyokuwa ngazi ya juu za mahakama za Kiislamu zilizoamua kesi za mali, ndoa na urithi baina ya Waislamu waliokuwa Waafrika wazalendo au kutoka nchi nyingine, Waarabu au Wahindi[3].

Katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani Wajerumani waliendelea mwanzoni na maliwali waliorithi kutoka kwa Sultani lakini baadaye nafasi yao ilichukuliwa na afisa Mjerumani. Baada ya eneo kutekwa na Uingereza na kuitwa Tanganyika cheo cha liwali kilirudishwa mwaka 1921 kama cheo cha "native administration" ya miji. Kwa mfano mjini Dar es Salaam liwali alikuwa daima Mwislamu kutoka ukoo wa Kiarabu hadi uhuru. Aliwajibika na usimamizi wa mahakama yake alikoshika pia nafasi ya jaji akasimamia pia ukusanyaji wa kodi[4]. Alikuwa na haki ya kuamulia adhabu ya kiboko "hadi viboko sita"[5].

Tanbihi

hariri
  1. Krapf 1882, A dictionary of the Swahili language, uk. 189: Liwali "liwali pro el wali" ("liwali badala ya "el wali")
  2. Kutokana na taarifa ya Lord Salisbury, taz. Jutta Bückendorf: „Schwarz-weiß-rot über Ostafrika!“ Münster, 1997
  3. Anderson, Islamic Law in Africa, uk. 89 "Liwalis' Court ... Full jurisdiction over Arabs, Baluchis and Africans (including Somalis, Malagasies and Comoro Islanders), in all matters in which the value of the subject-matter in dispute does not exceed one thousand five hundred shillings"; online kupitia google books
  4. Brennan 2007, Dar es Salaam uk. 38, online kupitia google books, iliangaliwa Julai 2018
  5. Brennan 2012, Taifa, uk. 67 f, online kupitia google books, iliangaliwa Julai 2018

Marejeo

hariri
  • James Norman Dalrymple Anderson, Islamic Law in Africa, reprint Routledge, 2008, ISBN 0415426006, 9780415426008
  • James R. Brennan & alii, Dar es Salaam. Histories from an Emerging African Metropolis, African Books Collective, 2007, ISBN 9987449700, 9789987449705
  • James R. Brennan, Taifa: Making Nation and Race in Urban Tanzania, Ohio University Press, 2012, ISBN 0821444174, 9780821444177