Mtaguso wa pili wa Nisea

Mtaguso wa pili wa Nisea uliitishwa na malkia Irene wa Bizanti mwaka 787, ili kujadili matumizi ya picha takatifu na sanamu katika Ukristo, kutokana na ombi la Papa Adrian I (772-795).

Mtaguso wa pili wa Nisea.

Wakristo wengi wanauhesabu kuwa wa saba kati ya Mitaguso ya kiekumeni. Ni wa mwisho kufanyika wakati wa mababu wa Kanisa.

Historia

hariri

Mtaguso mkuu huo ulihitajika ili kumaliza mabishano makali kuhusu sanamu za Kikristo yaliyochukua zaidi ya miaka 100 hasa katika Dola la Roma Mashariki yakimalizika mwaka 843 tu.

Chanzo ni uamuzi wa kaisari Leo III wa Bizanti (717-741) wa kuteketeza sanamu zote ili kujilinganisha na Waislamu waliotishia utawala wake na kujenga uhusiano mzuri nao.

Ndio mwanzo wa mabishano makubwa yasiyoishia katika hoja na maandishi, bali yalichukua uhai wa watu, hasa waliodhulumiwa na serikali.

Patriarki wa Konstantinopoli alilazimika kujiuzulu, lakini uamuzi wa kaisari ulizidi kupingwa na Wakristo wengi, hasa wamonaki na mwanateolojia Yohane wa Damasko. Mapapa wa Roma pia walipinga uamuzi huo.

Sera ya dola ilibadilika aliposhika uongozi Irene kwa niaba ya mtoto wake mdogo Konstantino VI wa Bizanti.

Mtaguso ulianza Konstantinopoli mwaka 786, lakini ulipoingiliwa na jeshi waliowaunga mkono maaskofu wengi waliopinga sanamu, Irene aliuhamishia Nisea ambapo vilifanyika vikao 7 kuanzia tarehe 28 Septemba 787. Cha mwisho kilifanyika katika ikulu tarehe 23 Oktoba 787.

Pamoja na maaskofu 300 hivi wa dola hilo, walihudhuria wamonaki wengi. Papa alituma mabalozi wake wawili na barua moja.

Mtaguso ulitofautisha heshima inayokubalika kwa sanamu na ibada isiyovumilika. Hoja kuu ni kwamba sanamu si kitu, ila inamwakilisha yule aliyechorwa ndani yake. Kimsingi sanamu zinakubalika kutokana na umwilisho wa Mwana wa Mungu uliomfanya atwae sura na kuonekana.

Mtaguso ulichukua pia maamuzi mbalimbali ili kurekebisha Kanisa.

Viungo vya nje

hariri
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtaguso wa pili wa Nisea kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.