Myeyungano wa kinyuklia

(Elekezwa kutoka Nuclear fusion)

Myeyungano wa kinyuklia (pia: Uyeyunganishaji wa kinuklia[1]; kwa Kiingereza: Nuclear fusion) ni mchakato ambamo viini 2 au zaidi vya atomu vyepesi zaidi vinaungana kuwa kiini kimoja kizito.

Jua linazalisha nishati yake kwa njia ya myeyungano nyuklia wa viini vya hidrojeni kuwa heli. Kila sekunde Jua linayeyunganisha tani milioni 610 za hidrojeni kuwa tani milioni 606 za heli. Halijoto ya sentigredi milioni inahitajika kwa myeyungano.
Myeyungano wa hidrojeni - deuteri-triti (D-T) unaachisha nishati.
Myeyungano D-T kuwa heli.

Masi ya kiini cha atomu kinachotokea ni ndogo kuliko jumla ya viini viwili vilivyoshiriki mle. Tofauti ya masi inabadilishwa kuwa nishati. Albert Einstein alionyesha nishati inayotokana na badiliko hilo katika fomula yake E=mc2. Hivyo myeyungano wa kinyuklia unazalisha kiasi kikubwa cha nishati.[2].

Myeyungano wa kinyuklia unatokea kiasili ndani ya nyota kama Jua letu. Katika kitovu cha Jua shinikizo kubwa la masi yake linasababisha kutokea kwa mamilioni ya nyuzijoto.

Katika Jua letu atomi za hidrojeni zinayeyunganishwa katika mazingira ya shinikizo na joto kuu kuwa heli. Nishati inayopatikana hapo ni chanzo cha joto na nuru ya Jua. Kadiri hidrojeni inavyopungua ndani ya nyota heli itayeyunganishwa.

Myeyungano hauwezi kutokea na elementi zote. Kadiri elementi za kuyeyunganiwa ni nzito zaidi mchakato huwa mgumu kutendeka na hukomea hadi chuma (Fe).

Kuanzia uzito wa chuma myeyungano unahitaji nishati zaidi kuliko kuzalisha. Elementi nzito kuliko chuma zinatokea tu katika milipuko ya nyota za nova na supanova kwenye joto na shinikizo kubwa mno katika milipuko hiyo.

Mara nyota inapoishiwa elementi nyepesi kuliko chuma sehemu yake ya ndani inajikaza kuwa nyota kibete nyeupe ilhali sehemu za nje zinarushwa nje kwenye anga kama mawingu ya gesi ya ioni. Mabaki ya nyota yataendelea kupoa na mchakato wa myeyungano utakwisha polepole: nyota "inakufa". [3]

Kama masi yake ni kubwa, angalau mara kumi kuliko Jua letu, mlipuko na kutokea kwa nyota ya nova inaweza kupatikana.

Kuna majaribio ya binadamu ya kuiga mchakato huo katika mitambo lakini hadi sasa haijawezekana kufikia teknolojia inayoruhusu kuzalisha umeme kwa njia hiyo.

Hapa duniani ni vigumu kupata myeyungano kwa sababu viini vya atomu huwa na chaji chanja na chanja - chanja huwingana. Hapo nguvu kubwa inahitajika kushinda kizuizi hicho kama vile joto na shinikizo kali ndani ya Jua. Hadi sasa imekuwa vigumu kujenga mitambo inayoweza kuzalisha na kutunza joto ya nyuzi mamilioni pamoja shinikizo linalohitajika kuanzisha na kudumisha myeyungano wa nyuklia.

Lakini inawezekana kusababisha myeyungano wa kinyuklia kwa matumizi ya silaha katika bomu la hidrojeni. Katika bomu hilo mlipuko wa bomu atomia ndogo (yaani nishati ya mwatuko nyuklia) unatumiwa ili kugonganisha viini vya atomu na kuanzisha myeyungano.

Marejeo

hariri
  1. "Uyeyunganishaji wa kinuklia" ni pendekezo la kamusi ya KSBFK, "myeyungano wa kinyuklia" ni pendekezo la KAST
  2. "FusEdWeb | Fusion Education". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-01-01. Iliwekwa mnamo 2017-10-14.
  3. "Progress in Fusion". ITER.
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Myeyungano wa kinyuklia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.