Nukta za Lagrange (kwa Kiingereza: Lagrange point, Lagrangian point) ni nafasi maalumu zinazopatikana pale ambako gimba kubwa linazungukwa na gimba dogo zaidi, kwa mfano Jua na sayari. Hapo zinatokea nafasi tano ambako kani ya mvutano ya magimba yale mawili inasawazika.

Nukta za Lagrange 1-5
Nukta za Lagrange za Dunia

Kanuni za hisabati kwa hali hii zilitambuliwa na mwanahisabati mwitalia Joseph-Louis Lagrange[1]. Nafasi au nukta hizo tano zinaitwa L1 hadi L5. Tatu (L1, L2, L3) ziko kwenye mstari unaopita kwenye magimba mawili, na mawili (L4,L5) yako kwenye njia ya njiamzingo ya gimba dogo zaidi kwa umbali wa nyuzi 60° kila upande wa gimba dogo zaidi.

Kwenye anga-nje nukta za Lagrange hutokea kwenye njiamzingo za sayari na violwa vingine. Sayari inayozunguka Jua (au nyota nyingine) kwa kawaida hufyeka njiamzingo yake kwa kukusanya magimba madogo yanayoanguka kwake kwa sababu ya mvutano wa sayari. Lakini kwenye nukta za Lagrange, mvutano wa Jua na sayari zinabatilishana.

Nukta za Lagrange hutumiwa kwa vyombo vya anga-nje vinavyotakiwa kuwa na nafasi thabiti angani. Nukta L1, L2 na L3 si thabiti sana katika Mfumo wa Jua kwa sababu kuna athira ya sayari nyingine. Hata hivyo athira hizo si kubwa na hivyo inawezekana kuweka satelaiti kwenye nukta hizi inayohitaji injini yake mara chache tu kusahihisha nafasi yake, kwa hiyo haitumii fueli nyingi.

Nukta L3 haikutumiwa bado maana iko mbali sana upande mwingine wa Jua. L1 (baina Jua na Dunia) inatumiwa kwa satelaiti zinazoangalia na kupima Jua na upepo wa Jua. Nukta ya L2 inafaa kwa darubini za anga-nje; darubini mpya ya James Webb itapelekwa L2 kwenye mwaka 2020.

Nukta za L4 na L5 ni thabiti sana – kama satelaiti inasogezwa kidogo na mvutano wa sayari nyingine itavutwa tena kwenye nafasi hiyo. Huko tunaweza kukuta magimba madogo kama asteroidi zinazozunguka Jua kwa kutumia njia ya njiamzingo ya sayari. Mshtarii ina asteroidi zaidi ya milioni moja zinazopatikana kwa makundi mawili kwenye nukta za L4 na L5 za njiamzingo yake. Asteroidi zinazofuatana na sayari kwenye nukta hizi huitwa “Watroia”. Sayari nyingine za Mfumo wa Jua zina idadi ndogo tu za Watroia.

Marejeo

hariri
  1. Lagrange alikuwa Mwitalia aliyezaliwa kwa jina la Giuseppe Luigi Lagrangia akaishi miaka mingi Ujerumani na Ufaransa; anajulikana zaidi kwa jina lake la Kifaransa

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: