Nyotamkia ya Halley
Nyotamkia ya Halley (jina rasmi 1P/Halley, kwa Kiingereza Halley's Comet) ni moja kati ya nyotamkia zinazozunguka Jua letu. Kila baada ya miaka 75 au 76 inapita karibu na Dunia ikionekana vema kwa macho matupu, hivyo ni mashuhuri. Itaonekana tena kwenye mwaka 2061.
Inazunguka Jua kwenye obiti yenye umbo la duaradufu. Wakati wa kuwa karibu na Jua (sehemu inayoitwa "periheli") inaonekana kwa muda wa wiki kadhaa kama nyota inayoota "mkia" yaani mstari mwangavu. Wakati inakwenda mbali na Jua mkia huo unapotea tena na kwa jumla haionekani tena kwa macho matupu ikikaribia "afeli" au sehemu ya mbali na Jua.
Jina na utambuzi
Jina limeteuliwa kwa heshima ya mwanaastronomia Mwingereza Edmund Halley aliyetambua ya kwamba nyotamkia aliyotazama mwaka 1705 ilikuwa ileile iliyowahi kutazamwa tayari katika miaka 1682(na Arnold), 1607 (na Johannes Kepler) na 1531 (na Petrus Apianus). Kwa hiyo alitabiri kurudi kwake mnamo 1758. Kweli ilionekana tena tarehe 25 Desemba 1758, miaka 16 baada ya kifo cha Halley. Katika mwaka uliofuata Mfaransa Nicolas Louis de Lacaille aliiorodhesha kama "comète de Halley".
Katika utaratibu wa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ilipokea jina la 1P/Halley. Namba 1 inataja nafasi yake ya kuwa nyotamkia ya kwanza iliyotambuliwa kisayansi, herufi P (ing. "periodic") inamaanisha ni nyotamkia inayorudi katika muda usiozidi miaka 200, Halley ni jina la mtambuzi. Nyotamkia zote zilizothibitishwa kuwa na obiti ya kurudia zimepokea namba pamoja na herufi P na jina la mtambuzi.
Tabia
Wakati wa kupita karibu na Jua katika mwaka 1987 vipimaanga kadhaa vilirushwa juu na hasa kipimaanga Giotto kilifaulu kupata data nyingi. Halley ni gimba lenye umbo la kufanana na karanga. Urefu wake ni kilomita 15.3, unene kilomita 7.2. Uso unafunikwa na vumbi na rangi ni nyeusi.
Kutoka upande wa uso unaoangzwa na Jua kulikuwa na michirizi ya gesi na vumbi inayounda “mkia” wake. Upande huu kuna barafu iliyoanza kuyeyuka na kufoka nje. Gesi inayotoka ilipimwa kuwa maji 80%, monoksidi ya kaboni 10 %, methani na amonia 2.5% pamoja na viwango vidogo vya elementi nyingine kama feri na natiri.
Mwili wa nyotamkia ni mchanganyiko wa mawe, vumbi na barafu. Ikifuata obiti yake na kukaribia jua kiasi cha kutosha inaanza kuonekana kama nyota ikiakisi nuru ya jua. Ikikaribia jua zaidi sehemu ya barafu yake inaanza kuyeyuka kuwa mvuke unaotoka kwenye kiini cha nyotamkia yenyewe na kuizungusha kama angahewa. Gesi hii inasukumwa na upepo wa Jua (shinikizo ya miale ya nuru itokanayo na Jua) na kuonekana kama "mkia". Mkia huu unaelekea kila wakati upande usio wa jua kwa sababu upepo wa jua unasukuma mvuke upande ule.
Mipito ya Nyotamkia wa Halley kwenye Periheli iliyoripotiwa
Nyotamkia inaonekana kutoka Duniani wakati inakaribia periheli yake, yaani sehemu ya obiti ambayo ipo karibu zaidi na Jua. Tarehe ambazo Halley ilifika periheli zinaweza kukadiriwa kwa kutumia kanuni za fizikia. Taarifa ya kwanza iliyoweza kuthibishwa kuhusu nyotamkia ya Halley inapatikana katika kitabu cha historia ya China kuhusu kuonekana kwake kwenye mwaka 240 KK. Kwa jumla kumbukumbu ya wataalamu wa China inaonyesha taarifa nyingi katika karne za nyuma hadi kuboreka kwa astronomia na kumbukumbu yake katika magharibi yaani Ulaya na katika Mashariki ya Kati. Mipito mingine katika karne kabla ya Kristo iliripotiwa pia kwenye kumbukumbu ya Babeli.
25 Mei 240 KK (taarifa ya China)
13 Oktoba 164 KK (taarifa ya Babeli)
6 Agosti 87 KK (taarifa za Babeli na China)
11 Oktoba 12 KK (Wachina waliiona kwa miezi miwili)
26 Januari 66
22 Machi 141
18 Mei 218
20 Aprili 295
16 Februari 374
28 Juni 451
27 Septemba 530
15 Machi 607
3 Oktoba 684
21 Mei 760
28 Februari 837
19 Juli 912
6 Septemba 989
21 Machi 1066
19 Aprili 1145
29 Septemba 1222
26 Oktoba 1301
11 Novemba 137810 Juni 1456
26 Agosti 1531
27 Oktoba 1607
15 Septemba 1682
13 Machi 1759
16 Novemba 1835
20 Aprili 1910
9 Februari 1986
29 Juli 2061[1]
Marejeo
- ↑ Andreas Rétyi: „Halley - Kometen-Brevier für jedermann“; Franckh'sche Verlagshandlung, W Keller & Co., Stuttgart / 1985, ISBN 3-440-05572-8, Seite 65
Viungo vya nje
- Halley Info, tovuti ya theskylive, iliangaliwa Januari 2018