Nyuki-mchanga
Nyuki-mchanga (Andrena argentata)
Nyuki-mchanga (Andrena argentata)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Hymenoptera (Wadudu wenye mabawa mangavu)
Nusuoda: Apocrita (Hymenoptera wenye kiuno chembamba)
Familia ya juu: Apoidea
(bila tabaka): Anthophila
Familia: Andrenidae
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Nusufamilia 4:

Nyuki-mchanga (kutoka Kijerumani sandbienen) ni nyuki wadogo sana hadi wakubwa kiasi wa family Andrenidae katika familia ya juu Apoidea ya oda Hymenoptera wanaojenga viota vyao katika ardhi, hasa katika udongo mwenye mchanga. Nyuki hawa ni wapweke, lakini spishi kadhaa hujenga viota vyao karibu na kila kimoja. Chache sana hugawana kiota kimoja. Wanatokea maeneo kavu wenye joto kiasi, hasa katika nusudunia ya kaskazini. Afrika ina spishi 28 na Afrika ya Mashariki 4 tu.

Maelezo hariri

Ukubwa wa nyuki hawa ni kutoka wadogo sana hadi wakubwa kiasi: mm 3-25[1]. Wana nywele nyingi, ingawa katika spishi nyingine nywele ni chache. Kwa kawaida uso wao hasa una nywele nyingi. Rangi ya kutikulo mara nyingi ni nyeusi hadi kahawia, lakini kwa kawaida nywele ni nyeupe, hudhurungi au njano na spishi nyingine zina rangi ya machungwa au nyekundu-kahawia. Kama nyuki wengine wengi, spishi nyingi zina nywele maalum kwenye tibia za nyuma kwa kukusanya chavua kwenye madonge madogo. Spishi nyingine pia zina nywele kama hizo kwenye fumbatio. Ulimi ni mfupi. Kwa kuwa wanafanana kijuujuu sana na nyuki wengine, wanatofautishwa kwa urahisi zaidi na tabia ya kuchimba vishimo vya kiota ardhini.

Biolojia[1][2] hariri

 
Chimbo la kiota la nyuki-mchanga.

Majike huchimba mashimo ya kiota katika maeneo ya mimea michache, viwanda vya nyasi vya zamani, mapito kavu ya barabara, njia za mchanga n.k. Kila jike huchimba kiota chake, isipokuwa kwa spishi chache ambazo majike kadhaa hugawana kiota kimoja. Mara nyingi viota huwa karibu na kila kimoja na idadi kufikia zaidi ya elfu katika baadhi ya matukio. Kwa kawaida machimbo hayana kina kirefu, kama sm 5-8, lakini yanaweza kufikia sm 30 na katika hali ya kina kirefu sana hadi karibu m 3. Udongo uliochimbwa umeachwa kwenye kirundo mlangoni. Kila kiota kina matawi kutoka chimbo kuu ambayo kila lina chumba mwishoni. Kunaweza kuwa na vyumba 8 au zaidi (haswa viota vya jumuiya) kwenye kiota. Machimbo na vyumba vimewekwa na dutu isiyoweza kupenywa na maji na kukinga uzao dhidi ya unyevu, bakteria na kuvu. Kila chumba hujazwa na donge dogo la chavua na mbochi na yai hutagwa juu ya kila donge na baada ya hapo jike hufunga kila chumba cha kizazi. Mabuu wanaoibuka hujilisha kwa donge la chavua hadi wawe mabundo. Baada ya mpevu kuibuka hukaa kwenye chumba hadi msimu wa masika au wa mvua.

Nyuki-mchanga hukusanya chavua na mbochi kutoka kwa maua ya ama spishi moja au chache au ya spishi nyingi kulingana na spishi ya nyuki. Hata hivyo, kwa sababu ya ulimi wao fupi, hawawezi kukusanya mbochi kutoka kwa maua ya kina. Spishi fulani ni muhimu sana kwa uchavushaji wa mimea na miti, kama vile miti fulani ya matunda.

Spishi za Afrika ya Mashariki hariri

  • Andrena africana
  • Andrena notophila
  • Andrena somalica
  • Meliturgula scriptifrons

Picha hariri

Marejeo hariri