Kimetameta (mbawakawa)

Familia ya mbawakawa
(Elekezwa kutoka Phengodidae)
Kimetameta
Kimetameta wa Kanada (Proturis sp.) akitoa nuru.
Kimetameta wa Kanada (Proturis sp.) akitoa nuru.
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Elateroidea
Leach, 1815
Ngazi za chini

Familia 4:

Vimetameta au vimulimuli ni mbawakawa wa familia mbalimbali za familia ya juu Elateroidea. Majina hayo yanaweza kutumiwa pia kutaja spishi za visubi-kuvu za familia Keroplatidae (Diptera: Nematocera), lakini spishi hizo hazipatikani katika Afrika. Vimetameta wanaoruka huitwa fireflies kwa Kiingereza na wale wasioweza kuruka huitwa glowworms. Wao wa mwisho ni ama lava au majike bila mabawa wanaofanana na lava.

Maelezo hariri

Spishi za Elateroidea zina umbo la kawaida la mbawakawa na hutofautiana kwa saizi kuanzia mm chache hadi mm 25 au zaidi. Madume wanaweza kuwa na vipapasio vyenye kufafanua sana. Katika spishi nyingi majike hawana mabawa na hufanana na lava. Kwa kweli, takriban spishi zote za vimetameta zina majike walio na umbo la lava. Mara nyingi wanaweza kutofautishwa na lava tu kwa macho yao ya kuungwa, ingawa hayo ni madogo kuliko macho ya madume.

Mara nyingi lava huwa warefu sana na wembamba na hao huitwa "wireworms" (minyoo ya waya) kwa Kiingereza[1]. Wanaweza kufanana na viwavi lakini wanajulikana kwa ukosefu wa miguu bandia kwenye fumbatio.

Sifa kuu ya vimetameta ni uwezo wao wa kutoa nuru (bio-uangazaji). Ogani zinazotoa nuru zinaweza kuwa kwenye sehemu tofauti za mwili, ingawa ncha ya fumbatio na kichwa ni sehemu za kawaida.

Lava wa vimetameta ni mbuai wanaojilisha kwa wadudu wengine, konokono na nyungunyungu. Wapevu ni ama mbuai au hula mbelewele na mbochi. Vimetameta fulani hukamata spishi nyingine za vimetameta. Spishi nyingine, kama kimetameta wa kawaida wa Ulaya, hazina kinywa na kwa hivyo haziwezi kujilisha[1].

Bio-uangazaji hariri

Utaratibu hariri

Bio-uangazaji ni mchakato mfanisi sana na haitoi joto. Inajumuisha protini inayoitwa lusiferini na kimeng'enya kinachoitwa lusiferase. Kile cha mwisho hufanyiza lusiferini kwa uwepo wa ioni za magnesiamu, ATP na oksijeni ili itoe nuru[2]. Kulingana na muundo wa lusiferase nuru hii ni njano, kijani au nyekundu isiyoiva yenye lukoka kati ya nm 510 na 670[3]. Vimetameta kadhaa huweza kutoa nuru njano na nyekundu katika sehemu tofauti za mwili. Mahali pa kawaida pa ogani za kutoa nuru ni kwenye ncha ya fumbatio.

Shughuli hariri

Inaaminika kwamba bio-uangazaji katika vimetameta ilianza kwenye lava. Shughuli yake inaonekana kuwa kuonya mbuai watakaoweza kushambulia kuwa lava wana ladha mbaya au hata sumu[4]. Wakati wa mageuko, uwezo huu ulihifadhiwa kwenye wapevu, kwanza katika majike wanaofanana na lava na baadaye katika madume. Wapevu hutoa nuru ili kuvutia wenzi[5]. Katika spishi ambazo jike wao tu hutoa nuru, anafanya hii karibu kila wakati au kwa mimweko. Ikiwa jinsia zote mbili hutoa nuru, madume huanza kumweka kwa kawaida na majike kisha hujibu. Katika spishi tofauti mimweko ina muda na marudio tofauti, ili madume waweze kutambua majike wa spishi yao. Spishi fulani za vimetameta zina uwezo wa kuiga msimbo wa spishi nyingine ili kuivutia na kuila[4]. Kwa kawaida mbuai ni mkubwa kuliko mbuawa.

Picha hariri

Marejeo hariri

  1. 1.0 1.1 Chisholm, Hugh, ed. (1911) "Wireworm", Encyclopaedia Brittannica, 28: 739.
  2. Hastings, J. W. (1983). "Biological diversity, chemical mechanisms, and the evolutionary origins of bioluminescent systems". Journal of Molecular Evolution 19 (5): 309–21. Bibcode:1983JMolE..19..309H. ISSN 1432-1432. PMID 6358519. doi:10.1007/BF02101634.  Unknown parameter |s2cid= ignored (help)
  3. HowStuffWorks "How do fireflies light up?". Science.howstuffworks.com (19 January 2001). Retrieved on 22 June 2013.
  4. 4.0 4.1 Lewis, Sara M.; Cratsley, Christopher K. (January 2008). "Flash Signal Evolution, Mate Choice, and Predation in Fireflies". Annual Review of Entomology 53 (1): 293–321. ISSN 0066-4170. PMID 17877452. doi:10.1146/annurev.ento.53.103106.093346.  Unknown parameter |s2cid= ignored (help)
  5. Martin, Gavin J.; Branham, Marc A.; Whiting, Michael F.; Bybee, Seth M. (February 2017). "Total evidence phylogeny and the evolution of adult bioluminescence in fireflies (Coleoptera: Lampyridae)". Molecular Phylogenetics and Evolution 107: 564–575. ISSN 1055-7903. PMID 27998815. doi:10.1016/j.ympev.2016.12.017.  Unknown parameter |doi-access= ignored (help)